'
Tuesday, January 5, 2016
YANGA, AZAM ZASHINDWA KUTAMBIANA KOMBE LA MAPINDUZI
Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
YANGA SC imeshindwa kuifunga Azam FC pungufu, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Sasa timu zote za Bara, Mtibwa Sugar na Yanga SC zinafungana kwa pointi nne nne kila moja baada ya mechi mbili, wakati Azam ina pointi mbili baada ya mechi mbili oia, huku Mafunzo ikishika mkia haina pointi. Yanga itamaliza na Mtibwa, wakati Azam itamaliza na Mafunzo kuwania nafasi mbili za Nusu Fainali keshokutwa.
Azam FC ilimpoteza Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyeonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Mfaume Ali Nassor dakika ya 62, lakini ikamudu kumaliza mechi kwa sare.
Katika mchezo huo uliotawaliwa na undava na matukio ya ubabe na utovu wa nidhamu, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao, ingawa Yanga SC walitawala na kutengeneza nafasi kadhaa walizoshindwa kutumia.
Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi katika lango la Azam dakika ya tatu kupitia kwa mshambuliaji wake, Donald Ngoma ambaye alipiga shuti pembeni na kupoteza nafasi hiyo ya kupata bao la mapema.
Dakika ya 18 Azam walijibu shambulizi hilo, winga Ramadhani Singano ' Messi' akitia krosi nzuri, lakini Bocco aliyekuwa jirani alishindwa kuunganisha.
Dakika 34 kipa wa Azam, Aishi Manula alipangua shuti la kali la Ngoma aliyemtoka kali beki Serge Wawa.
Sekunde chache kabla ya mapumziko, Manula alidaka tena shuti la Simon Msuva na kuikosesha Yanga nafasi nyingine ya kufunga.
Mapema kipindi cha kwanza, beki Muivory Coast, Serge Wawa wa Azam FC alitembezeana undava na mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga SC, Ngoma kabla ya baadaye kuamua kutulia na kucheza mpira.
Beki wa kulia wa Yanga SC, Juma Abdul naye alileteana tafrani mara kadhaa na Bocco, wakati Himid Mao naye alichimbiana mkwara na Ngoma.
Wakati wa mapumziko makomandoo wa Yanga SC na Azam FC walitembezeana mikwara kwenye kibaraza cha kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) waliingia kwenye Uwanja uliosaza mashabiki mwanzoni mwa kipindi cha pili kuimarisha ulinzi kuwasaidia askari Polisi, ambao walikwishaanza kuelemewa.
Kipindi cha pili, Yanga SC waliendelea kushambulia zaidi, ingawa ni Azam FC waliofanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 58 baada ya shambulizi la kushitukiza.
Sifa zimuendee mfungaji wa bao hilo, Kipre Herman Tchetche raia wa Ivory Coast aliyewakokota mabeki watatu wa Yanga SC hadi karibu kabisa na boksi na kufumua shuti lililompita kipa Deo Munishi ‘Dida’.
Beki Mtogo, Vincent Bossou aliisawazishia Yanga SC dakika ya 83 akimalizia mpira ulioparazwa kwa kichwa na Malimi Busungu baada ya kona ya Simon Msuva.
Hata hivyo, beki Shomary Kapombe aliokoa mpira huo kuurudisha uwanjani ukiwa umekwishavuka mstari wa lango, lakini refa hakudanganyika na Yanga wakapewa haki yao.
Donald Ngoma alikuwa mwenye bahati kwa kutoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumsukuma kabla ya kumkita kiungo Himid Mao kipindi cha pili.
Na refa alipuuza malalamiko ya Bocco kutemewa mate beki wa Yanga SC, Kevin Yondan licha ya kuuona uchafu huo kwenye uso wa Nahodha wa Azam FC.
Baada ya mchezo, beki Msenegali wa Azam FC, Racine Diouf alitaka kuzichapa na beki wa Yanga SC, Mwinyi Hajji Mngwali kabla ya kuamuliwa na wachezaji wenzao.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi itaendelea kesho kwa mechi za Kundi A, JKU wakimenyana na Mafunzo na URA ya Uganda ikimenyana na mabingwa watetezi, Simba SC.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Pato Ngonyani/Vincent Bossou dk62, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk71, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Malimi Busungu dk76.
Azam FC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Abdallah Kheri, Racine Diouf/David Mwantika dk90, Serge Wawa, Jean-Baptiste Mugiraneza, Ramadhani Singano ‘Messi’/Frank Domayo dk66, Himid Mao, John Bocco, Ame Ali ‘Zungu’/Mudathir Yahya dk46 na Kipre Tchetche/Didier Kavumbangu dk71.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment