KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 13, 2011

HILI NI BAO LA MWAKA

Mshambuliaji Wayne Rooney akiifungia timu yake ya Manchester United bao la pili kwa njia ya tiktak jana wakati ilipomenyana na Manchester City na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1. Wachambuzi wengi wa masuala ya soka wamelielezea bao hili kuwa ni la mwaka.

Thursday, February 10, 2011

Dakore afunga ndoa na Akande


BAADA ya usiri wa muda mrefu, hatimaye mwigizaji Dakore Egbuson amefunga ndoa na rafiki yake wa karibu, Olumide Akande, ambaye ni mtoto wa mwanasiasa, Harry Akande.
Habari za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na Dakore zimeeleza kuwa, wapenzi hao walifunga ndoa rasmi Januari 16 mwaka huu mjini Lagos.
Kwa mujibu wa habari hizo, sababu kubwa ya kuchelewa kufungwa kwa ndoa hiyo ni wazazi wa Akande kumwekea masharti mkwe wao, wakimtaka aachane na kazi ya uigizaji.
Kufuatia masharti hayo, Dakore alikubali kuachana na kazi hiyo ili kutimiza nadhiri yake ya kufunga ndoa na Akande na pia kupata baraka za wakwe zake.

MWANAHAWA: Mimi ni mzee, lakini bado nipo juu


"Sifurahishwi na mwenendo wa baadhi ya viongozi na waimbaji wa kikundi cha taarab cha Jahazi," ndivyo anavyosema mwimbaji mkongwe wa muziki huo, Mwanahawa Ally alipozungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Dar es Salaam juzi.
Mwanahawa, ambaye katika siku za hivi karibuni imekuwa ikivumishiwa kwamba amelihama kundi hilo na kujiunga na East African Melody, alisema taarifa hizo si za kweli.
Alisema kilichomfanya ajitenge kwa muda na kundi hilo lenye mashabiki wengi hivi sasa nchini ni ubinfasi uliokithiri kwa baadhi ya viongozi na waimbaji wenzake.
Mkongwe huyo alisema, kutokana na kukithiri kwa tabia hiyo, ameamua kujiengua kwa muda hadi pale hali itakapokuwa shwari.
"Mimi ni mtu mzima, roho yangu inaniuma sana ninapotolewa maneno na mtu, ambaye naweza kumzaa kwa jambo, ambalo halina maana," alisema.
Mwanahawa alisema ndani ya kundi la Jahazi, hakuna upendo na umoja miongoni mwa wasanii wake na baadhi ya waimbaji hujiona bora kuliko wenzao licha ya ukweli kuwa bado ni wachanga katika fani.
Alisema kundi hilo kwa sasa linaendeshwa katika misingi ya chuki, uhasama na majungu, hali inayosababisha baadhi ya wasanii wake kujifanya 'Miungumtu'.
Mwimbaji huyo mwenye sauti mithili ya 'tirihanga' aliwataja baadhi ya viongozi waliojenga chuki dhidi yake kuwa ni pamoja na Hamisi Boa, ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi wa bendi na mtunza fedha, aliyemtaja kwa jina moja la Seif.
Mkongwe huyo wa mipasho hakusita kumtaja mwimbaji machachari, Isha Mashauzi, kuwa ni mmoja wa waimbaji wanaoongoza kwa kumchukia na kujenga chuki dhidi yake na wasanii wengine ndani ya kundi hilo.
“Kwa kweli, kuwa muwazi ni kwamba hawa ndio waliosababisha mimi nijitoe kwa muda ndani ya kundi hili kutokana na kuniandama kwa chuki,”alisema.
Mwanahawa alisema, ulifika wakati Isha alikuwa akijifanya mtu wa kuabudiwa ndani ya kikundi na hata alipofanya ‘madudu’ na kuonyesha utovu wa nidhamu, hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake.
"Namshangaa sana Isha kujifanye yeye ndiye kila kitu katika lile kundi na hajawahi kufanywa chochote," alisema.
Kinachomshangaza zaidi Mwanahawa ni kwamba, kila alipokuwa akimsalimia mwimbaji huyo, haitikii, hali inayojenga taswira kwamba kuna uhasama na chuki kati yao.
Mwimbaji huyo anayetamba kwa kibao chake cha 'Wema hazina kwa Mungu' alisema, Isha ni mwimbaji anayechipukia na hawezi kujilinganisha na yeye kwa namna yoyote.
"Nipo kwenye fani hii takribani miaka 44 iliyopita, nimejifunza mengi na sijawahi kugombana na mtu yeyote, kwa hiyo namshangaa sana anajilinganisha na mimi," alisema.
Mwanahawa alisema licha ya umri wake mkubwa, bado anajiona yupo juu katika fani hiyo na hamuoni msanii anayeweza kumfikia ama kumzidi.
Akiwazungumzia Boa na Seifu, alisema binafsi anashangazwa na tabia zao, ambazo alizielezea kuwa ni nadra kwa watoto wa kiume.
“Sijawahi kuona mtoto wa kiume akimchukia mtu, ambaye anaweza kuwa sawa na mama yake bila sababu yoyote. Kama kuna tatizo ni bora wanieleze,”alisema.
Mwanahawa alibainisha kuwa, tayari hivi sasa amesharekodi kibao kipya ndani ya kundi la East African Melody, kinachokwenda kwa jina la ‘Rabi niepushe na wenye roho mbaya kwangu’, ambacho kimeshaanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya radio nchini.
Mwimbaji huyo aliyewahi kutamba kwa vibao kadhaa kama vile, ‘Kinyago cha mpapure’, ‘Mwanamke hulka’ na ‘Roho mbaya sio mtaji’, alisema kwa sasa anafanyakazi na Melody kama mwimbaji mwalikwa.
Amewashauri waimbaji wenzake wa muziki huo kuachana na tabia ya majungu, badala yake waendeleze vibaji vyao. Alisema majungu hayawezi kuwafikisha mbali kiusanii zaidi ya kushusha vipaji vyao na kuwafanya wazidi kujengeana chuki.
"Binafsi sina bifu na mtu yeyote, nawaona waimbaji wa sasa kama wanangu na wengine ni wajukuu zangu, kwa hiyo nitaendelea kushirikiana nao hata wakinisusia, mimi bado nipo juu," alisema.

Judith Gamba kazini

Mwamuzi Judith Gamba (katikati) kutoka Arusha akiwapa onyo kwa maneno wachezaji wa timu za JKT Ruvu na African Lyon baada ya kuonyeshana ubabe, wakati timu hizo zilipomenyana mwanzoni mwa wiki hii katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Lyon ilishinda mabao 2-1.

Taifa Stars yaichakachua Palestina

MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars, Mrisho Ngassa (kushoto) akijaribu kumtokabeki wa Palestina, Shadi Alisat wakati timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tuesday, February 8, 2011

KONYAGI ILIVYOWAZAWADIA MASHABIKI WA SIKINDE

Wanamuziki wa bendi ya Mlimani Park wakiimba wakati wa onyesho la kutangaza kinywaji cha Konyagi lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ofisa Mauzo wa Konyagi, Sankey Mbuji (kulia) akimpatia mshindi wa kujibu maswali kuhusu Sikinde zawadi ya chupa na pakiti za konyagi wakati wa onyesho hilo.

Sankey Mbuji akimpatia mshindi mwingine wa shindano hilo zawadi ya konyagi.

Mashabiki wa bendi ya Mlimani Park wakijimwayamwaya wakati wa onyesho hilo.

Kikosi kamili cha waimbaji wa Sikinde kikilishambulia jukwaa wakati wa onyesho hilo kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Waimbaji wa Sikinde wakifanyakazi ya kuimba na kutangaza Konyagi wakati wa onyesho hilo.Thursday, February 3, 2011

Yanga hoi kwa Mtibwa

KASI ya Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara jana ilipunguzwa baada ya kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Bao pekee na la ushindi la Mtibwa lilifungwa na Hussein Javu, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Yusuf Mgwao. Alifunga bao hilo dakika ya 70 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Juma Abdul.
Kipigo hicho kilionekana kuwakera mashabiki wa Yanga, ambao mara baada ya mchezo, walimzonga Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga na kumtaka awatimue wachezaji wanaoshiriki kuihujumu timu.
Pamoja na kupata kipigo hicho, Yanga bado inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi nne kati yake na Simba, ambayo leo itacheza na African Lyon kwenye uwanja huo.
Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi kwa kufanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Mtibwa, lakini mashuti ya washambuliaji wake, Jerry Tegete na David Mwape yaliokolewa na kipa Shabani Kado.
Mtibwa ilijibu mashambulizi hayo kwa wachezaji wake, Omary Matuta kuingia na mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Dakika tano baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Mtibwa nusura ipate bao wakati Ally Mohamed, alipounasa mpira ndani ya eneo la hatari la Yanga, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Nelson Kimathi.
Dakika ya 54 beki Fred Mbuna wa Yanga alipanda mbele na kumimina krosi iliyomkuta Nurdin Bakari, aliyejitwisha mpira kwa kichwa, lakini ulipaa sentimita chache juu ya lango.
Matuta alipoteza nafasi nyingine nzuri ya kuifungia bao Yanga dakika ya 55 baada ya kupewa pasi na Yusufu Mgwao, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Wachezaji wa Yanga, hasa safu ya kiungo walionekana kuchoka katika kipindi cha pili na kutoa mwanya kwa Mtibwa kutawala. Kocha Fred Felix Minziro alisema kipigo hicho kilitokana na bahati mbaya.

Makocha wanne walilia kibarua Jangwani

MAKOCHA wanne wa soka kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya wamewasilisha maombi ya kutaka kuinoa Yanga.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Llyod Nchunga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, makocha hao wanataka kurithi mikoba ya Kostadin Papic, aliyetangaza kujiuzulu wiki iliyopita.
Nchunga alisema miongoni mwa makocha waliowasilisha maombi hayo ni pamoja na Sam Timbe kutoka Uganda.
Alisema tayari wameshafanya mazungumzo ya awali na Timbe na kuongeza kuwa, yamefikia hatua nzuri na wanatarajia kumalizana naye hivi karibuni.
Mwenyekiti huyo alisema makocha wengine waliowasilisha maombi hayo wanatoka katika nchi za England, Jamhuri ya Czech na Slovenia, lakini hakutaja majina yao.
Lakini uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, makocha hao ni Roy Barreto kutoka England, Simeon Efremon kutoka Jamhuri ya Czech na Ivo Von kutoka Slovenia.
Barreto aliwahi kuwa kocha mkuu wa Zimbabwe na kwa sasa anaishi nchini Afrika Kusini. Kocha huyo ametuma wasifu wake kwa njia ya mtandao.
Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umemtangaza Mwesingwa Celestine kuwa kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo.
Celestine anachukua nafasi ya Lawrence Mwalusako, aliyetangaza kujiuzulu wadhifa huo wiki iliyopita.

PAPIC AITOROKA YANGALICHA ya kuwekewa vikwazo vya kumfanya ashindwe kusafiri, Kocha Mkuu wa zamani wa Yanga, Kostadin Papic amefanikiwa kuondoka nchini kwa kutoroka.
Papic aliondoka nchini juzi saa moja usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Swiss Air baada ya kiongozi mmoja wa klabu hiyo kufanikisha safari yake.
Awali, mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji alikuwa amemzuia kocha huyo kuondoka ili ajibu tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili kuhusu ulaji wa fedha za usajili.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Llyod Nchunga alikiri jana kuwa, kocha huyo aliondoka kwa kutoroka na kurejea kwao Serbia.
Nchunga alisema Papic aliondoka baada ya kumuaga Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo,Davis Mosha na kusindikizwa uwanja wa ndege na mdau mmoja wa klabu hiyo.
Aliongeza kuwa, yeye alikuwa safarini kikazi nje ya mkoa wa Dar es Salaam na baada ya kurudi usiku wa Jumanne, alipata taarifa za kutoroka kwa kichwa huyo.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, Papic alifanikiwa kuondoka baada ya kutegua vikwazo alivyokuwa amewekewa na uongozi ili asiondoke.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baadhi ya wanachama wenye uadui na Nchunga walitengua vikwazo hivyo na kumwezesha kocha huyo kuondoka bila Manji na viongozi kuwa na taarifa.
Mbali na kufanikisha safari ya Papic, wanachama hao pia wamepanga kuihujumu Yanga katika mechi zake zijazo za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwa lengo la kumshinikiza Nchunga ajiuzulu.
Hata hivyo, tayari Nchunga ameshapata taarifa hizo na jana alikuwa akihaha kuhakikisha timu hiyo inashinda mechi yake dhidi ya Mtibwa Sugar. Wakati hayo yakiendelea, Nchunga amekiri kuwa wanaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu mkataba wa kipa Ivan Knezevic, aliyesajiliwa na Yanga kutoka Serbia.
Nchunga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepitia mkataba huo na kubaini kasoro kadhaa zikiwemo tofauti za malipo ya fedha.
Kwa mujibu wa Nchunga, mkataba wa kipa huyo unaonyesha kuwa alilipwa dola 3,000 za Marekani na Manji, lakini pesa alizopewa na viongozi ni pungufu.
Mwenyekiti huyo aliutaja mkataba mwingine wenye utata kuwa ni wa kiungo Omega Seme, ambao unaonyesha kuwa alilipwa sh. milioni 15 kutoka kwa Manji wakati fedha halisi alizopata ni sh. milioni 10.
Nchunga alisema uongozi umeamua kuingia mkataba na kampuni moja kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

WACHEZAJI GHALI ENGLAND


Khadija Kopa aichanachana JahaziMOJA ya matatizo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya muziki wa taarab hapa nchini ni kuwepo kwa chuki, uhasama na kupigana vijembe miongoni mwa wasanii wa fani hiyo.
Matatizo hayo kwa kiasi kikubwa yamesababisha wanamuziki wengi washindwe kupiga hatua mbele kimaendeleo, badala yake huishia njiani.
Hali hiyo imesabisha waimbaji wengi wa muziki huo waliowahi kutamba hapa nchini miaka ya nyuma hivi sasa kutoonekana tena kwenye tasinia hiyo.
Mbali na kutoweka kwa baadhi ya wasanii, matatizo hayo yamesababisha soko la muziki huo kushuka kadri siku zinavyosonga mbele. Umaarufu wa wasanii wa muziki huo umekuwa ukibaki na kuishia hapa hapa nchini.
Hali hiyo imeonekana kumgusa na kumkera sana mkongwe wa muziki huo nchini, Khadija Omar Kopa, ambaye ameeleza kinagaubaka sababu zinazochangia kuzorota kwa maendeleo ya muziki huo.
“Hakuna kingine zaidi ya waimbani kujengeana chuki, majungu na kupigana vijembe,”alisema Khadija wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Ladha za Pwani, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha C2C.
Khadija alisema katika siku za hivi karibuni, kumezuka baadhi ya waimbaji, ambao wamekuwa wakipika majungu kwa wenzao kwa lengo la kuwadhoofisha, hali inayorudisha nyuma maendeleo na maudhui ya muziki huo.
Mwanamama huyo aliyejengeka kimwili alisema, lengo la muziki wa taarab ni kuelimisha, kufurahisha na kutoa ujumbe kwa jamii na si kujengeana chuki, fitina na majungu kama ilivyozoeleka hivi sasa.
Mkongwe huyo wa mipasho aliyewahi kujizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchini alisema, kinachoshangaza ni kwamba tabia hiyo hufanywa na waimbaji chipukizi na baadhi ya vikundi vilivyoibuka hivi karibuni.
"Nawasikitikia sana hawa waimbaji chipukizi kwa kujiingiza kwenye matatizo. Badala ya kuendeleza vipaji vyao, wao wanaendeleza malumbano," alisema.
Mwimbaji huyo mwenye macho yenye mvuto na sauti ya kubembeleza alisema binafsi ameshangazwa na kukerwa zaidi na kikundi cha taarab cha Jahazi Modern kutokana na vitendo wanavyomfanyia.
Alisema baadhi ya waimbaji na viongozi wa kundi hilo wamejenga chuki za waziwazi dhidi yake, bila sababu yoyote, hali inayomweka kwenye wakati mgumu.
Khadija alisema mara kadhaa anapoalikwa kufanya maonyesho kwa kushirikiana na kundi hilo, viongozi na wasanii wake humfanyia vituko vya kila aina, ambavyo humfanya wakati mwingine ashindwe kuimba.
"Mara kwa mara ninapoalikwa kuimba pamoja na Jahazi, huwa sipewi ushirikiano. Hunifanyia vituko vingi sana,”alisema.
Mkongwe huyo wa taarab, aliyeanza kung’ara akiwa katika kundi la Culture la Zanzibar, alisema binafsi hana bifu na uongozi ama msanii yeyote wa kundi hilo na kwamba anawaheshimu.
Gwiji huyo wa kundi la taarab la Tanzania One Theatre (TOT Plus), anayetamba na wimbo wa Top in Town alisema, kutokana na vituko anavyofanyiwa na uongozi wa kundi hilo, analiona kama vile limeamua kumdhalilisha na kumvunjia heshima.
Akitoa mfano alisema, katika tamasha la Mitikisiko ya Pwani lililofanyika mwishoni mwa mwaka jana katika ukumbi wa Daimond Jubilee, Dar es Salaam, alilazimika kuimba kwa tabu baada ya Jahazi kuondoa stejini baadhi vyombo vyao.
Kwa mujibu wa Khadija, kuna siku alikodiwa na mfanyabiashara Abbas Shentemba kuimba akiwa na waimbaji wengine pamoja na kundi la Jahazi, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na kuwekewa ngumu na viongozi wa kundi hilo.
"Nakumbuka nilialikwa pamoja waimbji wengi, akiwemo Mohamed Iliyas na Afua Suleiman, lakini sikuweza kuimba kutokana na kubaniwa na uongozi wa Jahazi na kila nilipokuwa namkumbusha msimamizi wa onyesho hilo, alinijibu kwa kejeli,”alisema.
"Alianza kupanda jukwaani Afua, wakati anapanda Mohamed Iliyas, nilimtuma mpiga kinanda mmoja wa Jahazi akamwambie yule msimamizi kwamba akiteremka Iliyas nipande mimi, lakini wakampa majibu ya kebehi,”aliongeza.
Akisimulia zaidi mkasa huo, nguli huyo wa mipasho alisema, siku hiyo alipata taarifa mapema kwamba hawezi kuimba na alimfuata aliyemkodi na kumuuliza, lakini alimpa majibu kwamba lazima aimbe.
Alisema baada ya Iliyas kuteremka stejini, alipanda Mzee Yusuf na kuanza kuimba na hapo ndipo alipoamini maneno aliyoambiwa mapema kwamba hawezi kuimba siku hiyo.
“Baada ya Mzee Yusuf kupanda stejini, nilimfuata aliyenialika na kumuaga na yeye akakubali, kwa maana hiyo niliondoka bila kuimba,”alisema Khadija.
"Mimi binafsi ni mtu wa watu, kwa hiyo naomba kama Jahazi nimewakosea kitu, wanambie ili niwaombe radhi na mimi kama wamenikosea waniombe radhi,”aliongeza.
"Namheshimu kila mtu, sijawahi kugombana na yeyote, naona Jahazi wanajisumbua kwa sababu kwangu ni watoto wadogo sana," alisema.
Mkongwe huyo wa mipasho amewatahadharisha waimbaji chipukizi kwa kuwataka wasibweteke na kuvamia mambo yasiyowahusu badala yake waonyeshe vipaji vyao.Alisema waimbaji wengi chipukizi wanalewa sifa na kusahau wajibu wao.
Khadija, ambaye alizaliwa miaka 47 iliyopita katika mtaa wa Makadara, Zanzibar amewahi kuimba pia kwenye vikundi vya East African Melody na Muungano.

CHEZA SIKINDE UPATE KONYAGI


MWAKILISHI wa Mauzo wa Kampuni ya Konyagi, Sankey Mbuja (kulia) akimkabidhi zawadi ya kinywaji cha Konyagi mwanadada Tina Method (kushoto) baada ya kuibuka mshindi wa kujibu maswali yanayohusu bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra. Shindano hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. Wengine pichani ni wanamuziki wa bendi hiyo, Hassan Kunyata, Hamisi Milambo na Habibu Jeff.
BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’, imeanzisha utaratibu wa kuwazawadiwa mashabiki wake vinywaji katika maonyesho yake inayoyafanya kila siku za Jumamosi kwenye ukumbi wa DDC, Kariakoo, Dar es Salaam.
Kiongozi wa bendi hiyo, Habibu Abbas ‘Jeff’ alisema mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, zawadi hizo zinatokana na udhamini walioupata kutoka Kampuni ya Konyagi.
Jeff, ambaye ni mmoja wa wanamuziki wakongwe wa Sikinde alisema, kampuni hiyo imeamua kuidhamini Sikinde kila Jumamosi kwa lengo la kutangaza kinywaji hicho.
Kwa mujibu wa Jeff, wakati wa maonyesho hayo, uongozi wa bendi huwazawadia mashabiki wanaojibu vizuri maswali kuhusiana na Sikinde na wanamuziki wake.
“Maswali yetu hulenga historia ya bendi, wanamuziki na majina ya nyimbo zetu mbalimbali za tangu mwaka 1978 na mashabiki wanaoyajibu vizuri tunawapa zawadi ya konyagi,”alisema.
Katika onyesho la mwishoni mwa wiki iliyopita, mwanadada Tina Method aliibuka mshindi wa kwanza wa zawadi ya Konyagi baada ya kumudu vyema kutaja majina ya wanamuziki wawili pekee waliopo kwenye bendi hiyo tangu ilipoanzishwa hadi sasa. Wanamuziki hao ni mpuliza tarumbeta Joseph Benard na mpiga drums, Jeff.
Naye Mwakilishi wa Mauzo wa Konyagi katika maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam, Sankey Mbuja alisema wamefurahishwa na promosheni inayofanywa na Sikinde kwa kinywaji hicho.
Alisema kutokana na ukongwe wa bendi hiyo katika masuala ya muziki wa dansi, maonyesho yake yamekuwa yakihudhuriwa na mashabiki wengi hivyo kupata nafasi ya kukitangaza vyema kinywaji hicho.

Namshukuru Tenga kwa kunihudumia matibabuSWALI: Pole kwa kuumwa. Hali yako inaendeleaje hivi sasa? Unapata matibabu?
JIBU: Namshukuru Mungu kwamba ninaendelea vizuri na matibabu, ambayo kwa asilimia kubwa yanasimamiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na watu wengine, ambao wamejitokeza kunisaidia. Kwa kweli nawashukuru kwa msaada wanaonipatia.
Pia nawashukuru sana viongozi wa serikali na watu binafsi, ambao wamekuwa wakinisaidia kwa muda mrefu sasa. Pia nawashukuru ndugu zangu, familia yangu, watoto wangu na mama yao kwa misaada, ambayo wamekuwa wakinipatia.
SWALI: Unazo taarifa zozote kuhusu kinachoendelea hivi sasa ndani ya klabu ya Yanga? Na je, zinakukumbusha kitu gani?
JIBU: Nimesikia kwamba kumezuka mgogoro mkubwa baina ya viongozi waliopo madarakani na wanachama. Kwa kweli ni aibu kubwa kwa klabu kama Yanga kukumbwa na migogoro ya mara kwa mara wakati timu yao ikiwa inawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Nawashauri viongozi wa Yanga wakae chini na kumaliza tofauti zao kwa sababu haziwezi kusaidia kuijenga timu hiyo zaidi ya kuibomoa. Ikumbukwe kuwa mgogoro huu hauleti sura mbaya kwa Yanga pekee bali nchi nzima. Mgogoro huu unaipaka matope nchi yetu kwa sababu taarifa zake zinatapakaa sehemu mbalimbali duniani. Unajua siku hizi dunia imekuwa kama kijiji, habari zinatapakaa kwa muda mfupi. Ni vyema Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga na viongozi wenzake wachukue tahadhari kubwa katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Wamalize tofauti zao na kuwa kitu kimoja.
Binafsi mgogoro huu unanikumbusha mambo mengi, hasa wakati nilipokuwa nikichezea Yanga. Nakumbuka kuna wakati mgogoro wa aina hii ndio uliosababisha kugawanyika kwa viongozi na wanachama na kuzaliwa kwa klabu ya Pan African. Tahadhari isipochukuliwa mapema, inawezekana jambo hilo likatokea tena.
SWALI: Unawashauri nini viongozi wa Yanga kuhusu ushiriki wao katika michuano ya Kombe la Shirikisho?
JIBU: Wasikate tamaa baada ya kutoka sare ya mabao 4-4 na Dedebit ya Ethiopia. Uwezo wa kushinda mchezo wa marudiano kule Ethiopia upo. Wanachopaswa kufanya ni kuacha malumbano na kumtafuta mchawi. Wajiandae vyema kwa mchezo wa marudiano. Wahakikishe dosari zote zilizojitokeza katika mechi ya awali hazirudiwi tena.
Namshauri mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji ahakikishe wachezaji wote wanaodai pesa zao za usajili wanalipwa mara moja. Hii itasaidia sana kuwaongezea nguvu na ari ya kushinda mchezo huo. Vinginevyo Yanga itavuna ilichopanda kwa kuyaaga mashindano hayo mapema.
SWALI: Unadhani nini kilisababisha Yanga ishindwe kufanya vizuri katika mchezo huo?
JIBU: Kutokana na taarifa nilizozisoma kwenye magazeti na kuzisikia kwenye redio na televisheni, mgogoro uliopo sasa Yanga umeingia hadi kwa wachezaji. Hili ni jambo la hatari na linaweza kusababisha hali ikawa mbaya zaidi.
Wajifunze kwa wenzao Simba, ambao hivi sasa wametulia na ndio sababu timu yao imekuwa ikifanya vizuri katika michuano mbalimbali. Timu yao inakaa kambini wakati Yanga wachezaji wanafanya mazoezi na kurejea nyumbani.
SWALI: Unawashauri nini wachezaji wa Yanga kuhusu mgogoro huu, ambao unaonekana kuwachanganya?
JIBU: Wasijiingize upande wowote kwenye mgogoro huu. Wakumbuke kuwa ajira yao ni kucheza soka. Wasikubali kushirikishwa katika mgogoro huu kwa sababu wakifanya hivyo, watakaoathirika zaidi ni wao.
Wakumbuke kuwa, mashindano hayo yana umuhimu mkubwa kwao, hivyo wakifanya vizuri watanufaika na wakiboronga, watakosa mambo mengi. Hii ni nafasi nzuri kwao kuonekana kimataifa na kupata nafasi ya kucheza soka ya kulipwa. Kama wana madai yoyote kwa uongozi, wafuate taratibu kuyadai kuliko kufanya huduma.
SWALI: Unazungumziaje maandalizi na ushiriki wa timu ya Taifa, Taifa Stars katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2012?
JIBU: Sidhani kama maandalizi yanayofanywa na Taifa Stars katika mashindano hayo ni mabaya. Na kinachofurahisha zaidi ni kwamba huduma zinazotolewa kwa wachezaji wa timu hiyo hivi sasa ni nzuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Binafsi napenda kuona timu hiyo ikivunja rekodi tuliyoweka mwaka 1980 kwa kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za michuano hiyo zilizofanyika Nigeria. Nitafurahi nikiona rekodi hiyo inavunjwa na kuandikwa nyingine na ikiwezekana warudi na ubingwa. Nadhani hiyo itakuwa ni furaha kubwa katika maisha yangu.
Nawashauri wadau wa soka nchini wampe ushirikiano mkubwa Kocha Jan Poulsen ili malengo yake yaweze kutimia. Pia timu icheze mechi nyingi za kimataifa kwa lengo la kuwajenga zaidi wachezaji na kuwapa uzoefu.