KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 3, 2011

PAPIC AITOROKA YANGA



LICHA ya kuwekewa vikwazo vya kumfanya ashindwe kusafiri, Kocha Mkuu wa zamani wa Yanga, Kostadin Papic amefanikiwa kuondoka nchini kwa kutoroka.
Papic aliondoka nchini juzi saa moja usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Swiss Air baada ya kiongozi mmoja wa klabu hiyo kufanikisha safari yake.
Awali, mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji alikuwa amemzuia kocha huyo kuondoka ili ajibu tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili kuhusu ulaji wa fedha za usajili.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Llyod Nchunga alikiri jana kuwa, kocha huyo aliondoka kwa kutoroka na kurejea kwao Serbia.
Nchunga alisema Papic aliondoka baada ya kumuaga Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo,Davis Mosha na kusindikizwa uwanja wa ndege na mdau mmoja wa klabu hiyo.
Aliongeza kuwa, yeye alikuwa safarini kikazi nje ya mkoa wa Dar es Salaam na baada ya kurudi usiku wa Jumanne, alipata taarifa za kutoroka kwa kichwa huyo.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, Papic alifanikiwa kuondoka baada ya kutegua vikwazo alivyokuwa amewekewa na uongozi ili asiondoke.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baadhi ya wanachama wenye uadui na Nchunga walitengua vikwazo hivyo na kumwezesha kocha huyo kuondoka bila Manji na viongozi kuwa na taarifa.
Mbali na kufanikisha safari ya Papic, wanachama hao pia wamepanga kuihujumu Yanga katika mechi zake zijazo za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwa lengo la kumshinikiza Nchunga ajiuzulu.
Hata hivyo, tayari Nchunga ameshapata taarifa hizo na jana alikuwa akihaha kuhakikisha timu hiyo inashinda mechi yake dhidi ya Mtibwa Sugar. Wakati hayo yakiendelea, Nchunga amekiri kuwa wanaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu mkataba wa kipa Ivan Knezevic, aliyesajiliwa na Yanga kutoka Serbia.
Nchunga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepitia mkataba huo na kubaini kasoro kadhaa zikiwemo tofauti za malipo ya fedha.
Kwa mujibu wa Nchunga, mkataba wa kipa huyo unaonyesha kuwa alilipwa dola 3,000 za Marekani na Manji, lakini pesa alizopewa na viongozi ni pungufu.
Mwenyekiti huyo aliutaja mkataba mwingine wenye utata kuwa ni wa kiungo Omega Seme, ambao unaonyesha kuwa alilipwa sh. milioni 15 kutoka kwa Manji wakati fedha halisi alizopata ni sh. milioni 10.
Nchunga alisema uongozi umeamua kuingia mkataba na kampuni moja kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mapato na matumizi ya klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

No comments:

Post a Comment