KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 3, 2011

Namshukuru Tenga kwa kunihudumia matibabu



SWALI: Pole kwa kuumwa. Hali yako inaendeleaje hivi sasa? Unapata matibabu?
JIBU: Namshukuru Mungu kwamba ninaendelea vizuri na matibabu, ambayo kwa asilimia kubwa yanasimamiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na watu wengine, ambao wamejitokeza kunisaidia. Kwa kweli nawashukuru kwa msaada wanaonipatia.
Pia nawashukuru sana viongozi wa serikali na watu binafsi, ambao wamekuwa wakinisaidia kwa muda mrefu sasa. Pia nawashukuru ndugu zangu, familia yangu, watoto wangu na mama yao kwa misaada, ambayo wamekuwa wakinipatia.
SWALI: Unazo taarifa zozote kuhusu kinachoendelea hivi sasa ndani ya klabu ya Yanga? Na je, zinakukumbusha kitu gani?
JIBU: Nimesikia kwamba kumezuka mgogoro mkubwa baina ya viongozi waliopo madarakani na wanachama. Kwa kweli ni aibu kubwa kwa klabu kama Yanga kukumbwa na migogoro ya mara kwa mara wakati timu yao ikiwa inawakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Nawashauri viongozi wa Yanga wakae chini na kumaliza tofauti zao kwa sababu haziwezi kusaidia kuijenga timu hiyo zaidi ya kuibomoa. Ikumbukwe kuwa mgogoro huu hauleti sura mbaya kwa Yanga pekee bali nchi nzima. Mgogoro huu unaipaka matope nchi yetu kwa sababu taarifa zake zinatapakaa sehemu mbalimbali duniani. Unajua siku hizi dunia imekuwa kama kijiji, habari zinatapakaa kwa muda mfupi. Ni vyema Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga na viongozi wenzake wachukue tahadhari kubwa katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Wamalize tofauti zao na kuwa kitu kimoja.
Binafsi mgogoro huu unanikumbusha mambo mengi, hasa wakati nilipokuwa nikichezea Yanga. Nakumbuka kuna wakati mgogoro wa aina hii ndio uliosababisha kugawanyika kwa viongozi na wanachama na kuzaliwa kwa klabu ya Pan African. Tahadhari isipochukuliwa mapema, inawezekana jambo hilo likatokea tena.
SWALI: Unawashauri nini viongozi wa Yanga kuhusu ushiriki wao katika michuano ya Kombe la Shirikisho?
JIBU: Wasikate tamaa baada ya kutoka sare ya mabao 4-4 na Dedebit ya Ethiopia. Uwezo wa kushinda mchezo wa marudiano kule Ethiopia upo. Wanachopaswa kufanya ni kuacha malumbano na kumtafuta mchawi. Wajiandae vyema kwa mchezo wa marudiano. Wahakikishe dosari zote zilizojitokeza katika mechi ya awali hazirudiwi tena.
Namshauri mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji ahakikishe wachezaji wote wanaodai pesa zao za usajili wanalipwa mara moja. Hii itasaidia sana kuwaongezea nguvu na ari ya kushinda mchezo huo. Vinginevyo Yanga itavuna ilichopanda kwa kuyaaga mashindano hayo mapema.
SWALI: Unadhani nini kilisababisha Yanga ishindwe kufanya vizuri katika mchezo huo?
JIBU: Kutokana na taarifa nilizozisoma kwenye magazeti na kuzisikia kwenye redio na televisheni, mgogoro uliopo sasa Yanga umeingia hadi kwa wachezaji. Hili ni jambo la hatari na linaweza kusababisha hali ikawa mbaya zaidi.
Wajifunze kwa wenzao Simba, ambao hivi sasa wametulia na ndio sababu timu yao imekuwa ikifanya vizuri katika michuano mbalimbali. Timu yao inakaa kambini wakati Yanga wachezaji wanafanya mazoezi na kurejea nyumbani.
SWALI: Unawashauri nini wachezaji wa Yanga kuhusu mgogoro huu, ambao unaonekana kuwachanganya?
JIBU: Wasijiingize upande wowote kwenye mgogoro huu. Wakumbuke kuwa ajira yao ni kucheza soka. Wasikubali kushirikishwa katika mgogoro huu kwa sababu wakifanya hivyo, watakaoathirika zaidi ni wao.
Wakumbuke kuwa, mashindano hayo yana umuhimu mkubwa kwao, hivyo wakifanya vizuri watanufaika na wakiboronga, watakosa mambo mengi. Hii ni nafasi nzuri kwao kuonekana kimataifa na kupata nafasi ya kucheza soka ya kulipwa. Kama wana madai yoyote kwa uongozi, wafuate taratibu kuyadai kuliko kufanya huduma.
SWALI: Unazungumziaje maandalizi na ushiriki wa timu ya Taifa, Taifa Stars katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 2012?
JIBU: Sidhani kama maandalizi yanayofanywa na Taifa Stars katika mashindano hayo ni mabaya. Na kinachofurahisha zaidi ni kwamba huduma zinazotolewa kwa wachezaji wa timu hiyo hivi sasa ni nzuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Binafsi napenda kuona timu hiyo ikivunja rekodi tuliyoweka mwaka 1980 kwa kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali za michuano hiyo zilizofanyika Nigeria. Nitafurahi nikiona rekodi hiyo inavunjwa na kuandikwa nyingine na ikiwezekana warudi na ubingwa. Nadhani hiyo itakuwa ni furaha kubwa katika maisha yangu.
Nawashauri wadau wa soka nchini wampe ushirikiano mkubwa Kocha Jan Poulsen ili malengo yake yaweze kutimia. Pia timu icheze mechi nyingi za kimataifa kwa lengo la kuwajenga zaidi wachezaji na kuwapa uzoefu.

No comments:

Post a Comment