KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 10, 2011

MWANAHAWA: Mimi ni mzee, lakini bado nipo juu


"Sifurahishwi na mwenendo wa baadhi ya viongozi na waimbaji wa kikundi cha taarab cha Jahazi," ndivyo anavyosema mwimbaji mkongwe wa muziki huo, Mwanahawa Ally alipozungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Dar es Salaam juzi.
Mwanahawa, ambaye katika siku za hivi karibuni imekuwa ikivumishiwa kwamba amelihama kundi hilo na kujiunga na East African Melody, alisema taarifa hizo si za kweli.
Alisema kilichomfanya ajitenge kwa muda na kundi hilo lenye mashabiki wengi hivi sasa nchini ni ubinfasi uliokithiri kwa baadhi ya viongozi na waimbaji wenzake.
Mkongwe huyo alisema, kutokana na kukithiri kwa tabia hiyo, ameamua kujiengua kwa muda hadi pale hali itakapokuwa shwari.
"Mimi ni mtu mzima, roho yangu inaniuma sana ninapotolewa maneno na mtu, ambaye naweza kumzaa kwa jambo, ambalo halina maana," alisema.
Mwanahawa alisema ndani ya kundi la Jahazi, hakuna upendo na umoja miongoni mwa wasanii wake na baadhi ya waimbaji hujiona bora kuliko wenzao licha ya ukweli kuwa bado ni wachanga katika fani.
Alisema kundi hilo kwa sasa linaendeshwa katika misingi ya chuki, uhasama na majungu, hali inayosababisha baadhi ya wasanii wake kujifanya 'Miungumtu'.
Mwimbaji huyo mwenye sauti mithili ya 'tirihanga' aliwataja baadhi ya viongozi waliojenga chuki dhidi yake kuwa ni pamoja na Hamisi Boa, ambaye ni miongoni mwa wakurugenzi wa bendi na mtunza fedha, aliyemtaja kwa jina moja la Seif.
Mkongwe huyo wa mipasho hakusita kumtaja mwimbaji machachari, Isha Mashauzi, kuwa ni mmoja wa waimbaji wanaoongoza kwa kumchukia na kujenga chuki dhidi yake na wasanii wengine ndani ya kundi hilo.
“Kwa kweli, kuwa muwazi ni kwamba hawa ndio waliosababisha mimi nijitoe kwa muda ndani ya kundi hili kutokana na kuniandama kwa chuki,”alisema.
Mwanahawa alisema, ulifika wakati Isha alikuwa akijifanya mtu wa kuabudiwa ndani ya kikundi na hata alipofanya ‘madudu’ na kuonyesha utovu wa nidhamu, hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake.
"Namshangaa sana Isha kujifanye yeye ndiye kila kitu katika lile kundi na hajawahi kufanywa chochote," alisema.
Kinachomshangaza zaidi Mwanahawa ni kwamba, kila alipokuwa akimsalimia mwimbaji huyo, haitikii, hali inayojenga taswira kwamba kuna uhasama na chuki kati yao.
Mwimbaji huyo anayetamba kwa kibao chake cha 'Wema hazina kwa Mungu' alisema, Isha ni mwimbaji anayechipukia na hawezi kujilinganisha na yeye kwa namna yoyote.
"Nipo kwenye fani hii takribani miaka 44 iliyopita, nimejifunza mengi na sijawahi kugombana na mtu yeyote, kwa hiyo namshangaa sana anajilinganisha na mimi," alisema.
Mwanahawa alisema licha ya umri wake mkubwa, bado anajiona yupo juu katika fani hiyo na hamuoni msanii anayeweza kumfikia ama kumzidi.
Akiwazungumzia Boa na Seifu, alisema binafsi anashangazwa na tabia zao, ambazo alizielezea kuwa ni nadra kwa watoto wa kiume.
“Sijawahi kuona mtoto wa kiume akimchukia mtu, ambaye anaweza kuwa sawa na mama yake bila sababu yoyote. Kama kuna tatizo ni bora wanieleze,”alisema.
Mwanahawa alibainisha kuwa, tayari hivi sasa amesharekodi kibao kipya ndani ya kundi la East African Melody, kinachokwenda kwa jina la ‘Rabi niepushe na wenye roho mbaya kwangu’, ambacho kimeshaanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya radio nchini.
Mwimbaji huyo aliyewahi kutamba kwa vibao kadhaa kama vile, ‘Kinyago cha mpapure’, ‘Mwanamke hulka’ na ‘Roho mbaya sio mtaji’, alisema kwa sasa anafanyakazi na Melody kama mwimbaji mwalikwa.
Amewashauri waimbaji wenzake wa muziki huo kuachana na tabia ya majungu, badala yake waendeleze vibaji vyao. Alisema majungu hayawezi kuwafikisha mbali kiusanii zaidi ya kushusha vipaji vyao na kuwafanya wazidi kujengeana chuki.
"Binafsi sina bifu na mtu yeyote, nawaona waimbaji wa sasa kama wanangu na wengine ni wajukuu zangu, kwa hiyo nitaendelea kushirikiana nao hata wakinisusia, mimi bado nipo juu," alisema.

No comments:

Post a Comment