KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 23, 2017

BMT YATOA MAAGIZO YA KUMALIZA MZOZO WA TFF NA SIMBASIMBA KUVAANA NA AZAM; YANGA NA MBAO FC KOMBE LA SHIRIKISHO


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), leo limetangaza ratiba ya mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama Azam Sports Federation Cup.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, iliyopangwa na kutangazwa leo, mabingwa watetezi Yanga wamepangwa kumenyana na Mbao FC, katika mechi itakayopigwa Aprili 30, mwaka huu, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ratiba hiyo inayonyesha kuwa, mabingwa wa mwaka juzi, Azam watacheza mechi hiyo kwa kuumana na wakongwe Simba. Mechi hiyo itapigwa Aprili 29, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

SIMBA YAPOKWA POINTI TATU ZA KAGERA SUGAR


KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeamua kuipokonya Simba pointi tatu ilizopewa na Kamati ya Saa 72,  baada ya kubainika kuwa, Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.

Akisoma maamuzi ya kamati hiyo leo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, amesema Kamati ya Saa 72 ilikosa uhalali wa kusikiliza rufani ya Simba kutokana na kikao chake kuwashirikisha baadhi ya wajumbe wasiohusika.

Aidha, Mwesiga alisema Kamati ya Nidhamu imebaini kuwa, rufani ya Simba ilikosa uhalali wa kusikilizwa kutokana na walalamikaji kutokana rufani na pia kushindwa kulipia ada ya sh. 300,000.

Licha ya Simba kupokwa pointi hizo, bado inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 59, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56, lakini ikiwa na mechi mbili mkononi, hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa.

HAJI MANARA ATUPWA JELA YA SOKA MWAKA MMOJA, ATOZWA FAINI MILIONI MOJA


 
MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara, amefungiwa kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja, kutokana na kutoa lugha chafu kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Aidha,  Manara, ambaye alishindwa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Nidhamu ya TFF, kilichotoa adhabu hiyo leo, ametozwa faini ya sh. milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu.

Manara alishindwa kuhudhuria kikao hicho kwa madai ya kupata dharura, lakini anayo nafasi ya kukata rufani.

Saa kadhaa baada ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kutangaza kumfungia Manara, Ofisa Habari wa zamani wa Yanga, ambaye naye alifungiwa mwaka mmoja, Jerry Muro, ametumia ukurasa wake wa instagram kuandika alivyoupokea uamuzi huo.

“Mtuache sasa tupumzike, tuliyofanya kwa taifa hili haswa kwenye mpira nadhani yametosha, swahiba karibu kijiweni @hajismanara.“

DK MWAKYEMBA AKUTANA NA KUTETA NA VIONGOZI WA SIMBA

Picha na Kitengo cha Mawasiliano WHUSM Dodoma.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe amekutana na na uongozi wa klabu ya Simba ukiongozwa na Rais wake Bw. Evans Aveva kwenye Ofisi zake Mjini Dodoma.

Uongozi wa Simba umeitikia wito wa Mhe. Mwakyembe wa kukutana naye na kujadili masuala mbalimbali ya mpira wa Miguu zikiwemo fursa na changamoto katika mabadiliko na maedneleo ya uendeshaji wa timu.

Aidha  Mhe. Mwakyembe  amepokea maoni ya Uongozi wa samba na kusahauri kuendelea kutoa ushirikiano na wadau wa mpira wa miguu nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa  na Katibu Mkuu Wizara husika prof Elisante Ole Gabriel, Mkurugenzi wa Michezo Yusufu Omary, Katibu Mkuu wa BMT Mohamed Kiganja, na Msajili wa Vilabu na Vyama nchini.

YANGA YAZIFUATA SIMBA, AZAM NUSU FAINALI KOMBE LA FAMabingwa wa tetezi wa Kombe la Shirikisho, Yanga wametinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Mchezo huo wa robo fainali ulifanyika jana, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Yanga sasa inaungana na mahasimu wao Simba, Azam na Mbao FC katika hatua inayofuata ya nusu fainali.

Yanga ilipata magoli yake kupitia kwa Amissi Tambwe aliyefunga dakika ya 16 ya mchezo, Obrey Chirwa aliyefunga bao la pili dakika ya 41. Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Simon Msuva aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 46 na kuihakikishia ushindi. Mechi hiyo haikuwa na mvuto kutokana na kunyesha kwa mvua kubwa.

Prisons nusura wapate bao la kufutia machozi baada ya kupata penalti dakika ya 54, lakini mpigaji Victor Hangaya aligongesha mwamba.

Ratiba ya mechi za nusu fainali inatarajiwa kupangwa leo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Friday, April 21, 2017

TFF YAMPELEKA HAJJI MANARA KAMATI YA MAADILIKwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.

Wanafamilia wa mpira wa miguu ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi mbalimbali.

Ili kutunza heshima ya mpira wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu zote hizo ndani na nje ya uwanja.

Taswira njema ya shirikisho inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho.

Dhima ya uongozi wa TFF ni pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua zitachukulia.

Na kwa muktadha huu Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji wa Simba Bw. Hajji Manara kwenye Kamati ya Maadili. Leo hii Aprili 21, 2017 atapewa mashtaka yake na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.

TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.

YOUNG AFRICANS, TANZANIA PRISONS KUMALIZIA ROBO FAINALI ASFC


 Mchezo wa Robo Fainali ya Nne ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC utafanyika kesho Aprili 22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utatoa mshindi ambaye ataungana na timu nyingine tatu ambazo tayari zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali. Timu zilizotangulia Nusu Fainali ya ASFC ni za Mbao FC, Simba SC na Azam FC.

Jumapili Aprili 23, mwaka huu kutakuwa na droo ya wazi kwa timu nne zitakazokuwa zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali ya ASFC, itakayofanyika Kituo cha Televisheni cha Azam ambao ni wadhamini wakuu wa jina la michuano na haki ya kuonesha mubashara michuano hii ambayo inafanyika kwa msimu wa pili mfululizo.

Azam FC ilikata tiketi ya kucheza Nusu Fainali ya ASFC baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Aprili 5, 2017 ikitanguliwa na Mbao iliyoishinda Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 18, 2017 ilihali Machi 19, mwaka huu Simba iliwatoa Madini ya Arusha kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Nusu Fainali inatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, kabla ya fainali ambako Bingwa wa michuano hii ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 ikiwa ni pamoja na za Ligi Kuu ya Vodacom (timu 16); Ligi Daraja la Kwanza (timu 24); Ligi Daraja la Pili (timu 24) na mabingwa wa mikoa timu 22, atazawadiwa Sh. 50 milioni na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho - CAF.

WAINGIZAJI, WASAMBAZAJI FILAMU WATAKIWA KUZINGATIA SHERIANa: Abuu Kimario – BODI YA FILAMU

Waingizaji na Wasambazaji wa Filamu za nje watakiwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya filamu nchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda wakati akizungumza na wadau wa Sekta ya filamu nchini mara baada ya kupokea maandamano ya Amani ya waigizaji wa Filamu za Kitanzania (Bongo Movie) katika makutano ya mtaa wa Magira na Lukoma, Kariakoo Jijini Dar es Salaam leo.

Makonda amesema kuwa lengo la Serikali siyo kuwazuia wafanyabiashara hao, bali inawataka wafuate sheria na taratibu zinazosimamia sekta hiyo muhimu katika maendeleo ya taifa letu.

“Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam haitawaonea haya wafanyabiashara wote wanaouza kazi za wasanii wa muziki na filamu ambao hawazingatii sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hizo kwani kufanya hivyo kunalikosesha taifa mapato yatokanayo na Kodi na kusababisha kukosekana kwa uwiano kwenye ushindani wa kibishara kati ya filamu za ndani na filamu kutoka nje ya nchi,” alisema Makonda.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nuru Millao akiwasilisha salamu za Waziri wa Wizara hiyo alisema kuwa, Waziri Mwakyembe anasikitishwa na uharamia unaofanywa na wafanyabishara wasiokuwa waaminifu na kusababisha kudumaza kazi za wasanii wazawa.

Aliongeza kuwa Serikali haitaishia kufanya operesheni za kushtukiza pekee, badala yake Serikali imeendelea kufanya maboresho ya Sera na Sheria zinazosimamia kazi za wasanii nchini ili ziendane na wakati.

Awali akitoa ufafanuzi kuhusu sheria Na.4 ya mwaka 1976 ya Filamu na Michezo ya kuigiza nchini alisema kuwa waingizaji na wasambazaji wa filamu za kutoka nje nchi wanao wajibu kisheria kuwasilisha kazi zao katika ofisi zake kwa ajili ya ukaguzi ili kujiridhisha kama kazi hizo zinakidhi vigezo vya kisheria ikiwemo maudhui na maadili, kisha zinapangiwa madaraja kulingana na maudhui yake.

Fissoo alisema kuwa sheria pamoja na kanuni zake hazihishii tu kwa watengenezaji na wasambazaji wa filamu za ndani, hivyo ni vyema wafanyabiashara wanaofanya biashara hiyo wakazingatia sheria hiyo na kanuni zake, kinyume chake ni uvunjifu wa sheria kwa makusudi.

“Niseme tu kuwa lengo la Serikali sio kuwazuia kufanya biashara yenu ya uingizaji na usambazaji wa filamu za nje, kinachofanyika ni kuhakikisha mnafuata sheria na taratibu kama wafanyabiashara wengine ili kuleta usawa kwenye ushindani wa kibiashara”, alisema Fissoo.

Kwa muda sasa Serikali imekuwa ikihamasisha wafanyabiashara wa kazi za Muziki na Filamu kuzingatia sheria ili kulinda maslahi ya pande zote. Kikao cha leo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wa Wizara na taasisi zinazosimamia kazi za wasanii nchini ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuinua hadhi na maslahi ya wasanii.

Sunday, April 16, 2017

SAFARI YA YANGA KIMATAIFA YAFIKIA TAMATI


UNAWEZA kusema kuwa safari ya Yanga katika michuano ya Afrika mwaka huu imefikia ukingoni baada ya kupigwa mweleka wa mabao 4-0 na MC Alger ya Algeria.

Kipigo hicho kwa Yanga, ilichokipata katika mechi ya marudiano iliyochezwa jana mjini Algiers, kimeifanya itolewe kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya kushinda mechi ya awali mjini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Yanga iliangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa raundi ya pili na Zanaco ya Zambia kwa faida ya bao la ugenini, baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka  Guinea, Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa imeshakubali kipigo cha mabao 2-0.

Dalili za Yanga kupoteza mchezo huo zilionekana mapema kutokana na kuibuka migogoro baina ya wachezaji na viongozi kabla ya safari ya kuanza safari ya Algeria

Wachezaji Vincent Bossou kutoka Togo na Obrey Chirwa kutoka Zambia, waligoma kusafiri na timu kwa sababu ya madai ya mishahara yao ya miezi mitatu.

SIMBA YAKWAA KISIKI KWA TOTO AFRICAN


MATUMAINI ya Simba kutwaa taji la ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, jana yaliota mbawa baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Toto African katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Sare hiyo imeifanya Simba iendelee kuongoza ligi ikiwa na pointi 62 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56 huku ikiwa na mechi mbili za viporo mkononi.

Iwapo Yanga itashinda mechi hizo mbili, itafikisha pointi 62, sawa na Simba, hivyo kufanya ushindani wa kuwania ubingwa kuamuliwa kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu muda wote wa dakika 90, lakini hakuna iliyoweza kupata bao.

Saturday, April 15, 2017

MAJALIWA YA YANGA KOMBE LA SHIRIKISHO MIKONONI MWA MC ALGERINAWEZEKANA ukawa mwisho wa safari ya Yanga katika michuano ya Afrika mwaka huu, au ukawa ni mwendelezo wa kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Jibu hilo litapatikana leo wakati mabingwa hao wa Tanzania Bara, waliotolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, watakaporudiana na MC Alger ya Algeria mjini Algiers.

Mechi hiyo ni ya marudiano kati ya timu hizo. Katika mechi ya awali, iliyochezwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ili iweze kusonga mbele, Yanga inahitaji kushinda mechi hiyo au kupata sare ya aina yoyote wakati wapinzani wao watalazimika kushinda kwa mabao 2-0.

Kwa mujibu wa ratiba, mechi hiyo imepangwa kuanza saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, lakini bado haijafahamika iwapo utaonyeshwa moja kwa moja na televisheni za hapa nchini.

Katika mechi hiyo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake wa kulipwa, Obrey Chirwa kutoka Zambia, ambaye hakusafiri na timu hiyo kwenda Algeria, kwa kile kinachodaiwa kuwa ameweka mgomo baridi kutokana na kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu.

Pengine tegemeo kubwa kwa timu hiyo litakuwa kwa washambuliaji wake nyota, Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma, waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu.

KAGERA SUGAR YAPINGA USHINDI WA MEZANI WA SIMBA


SIMBA, TOTO HATUMWI MTOTO DUKANI LEO


VINARA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba leo wanateremka dimbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kumenyana na Toto Africans.

Simba inashuka dimbani kucheza mechi hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya kuichapa Mbao FC mabao 3-2 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo Jumatano iliyopita.

Kabla ya kucheza na Mbao, Simba ilikuwepo mjini Bukoba, ambako ilimenyana na Kagera Sugar na kuchapwa mabao 2-1, lakini ikaambulia ushindi wa mezani baada ya kubainika kuwa, wapinzani wao walimchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano.

Katika mechi ya leo, Simba imepania kuifunga Toto African ili kujiimarisha zaidi kileleni mwa ligi hiyo na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa, ambao imekuwa ikiukosa kwa miaka mitatu sasa.

Hata hivyo, mechi hiyo haitarajiwi kuwa nyepesi kwa Simba kwa vile Toto African nayo itacheza kufa na kupona ili kujinasua katika janga la kushuka daraja.

Katika mechi ya awali iliyochezwa Oktoba, mwaka jana, mjini Dar es Salaam, Simba iliinyuka Toto mabao 3-0.

Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 61, baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 baada ya kucheza mechi 25.

KAMATI YA SAA 72 YAIPA SIMBA USHINDI WA POINTI TATU DHIDI YA KAGERA SUGAR

HATIMAYE hayawi hayawi yamekuwa. Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, 'Kamati ya Saa 72', imefikia uamuzi wa kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu kutokana na rufaa waliyoikatia Kagera Sugar.

Simba iliikatia rufaa Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi huku akiwa na kadi tatu za njano, wakati timu hizo zilipomenyana katika mechi baina ya timu hizo iliyochezwa Aprili 2, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Kagera Sugar iliichapa Simba mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Ilidaiwa kuwa, Kagera Sugar ilikiuka kanuni za ligi kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba huku akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kamati yake ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake ni kupokonywa ushindi.

Kutokana na kupewa pointi hizo, Simba sasa inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 kutokana na mechi 25 walizocheza hadi sasa.

Tuesday, April 11, 2017

SARAH SOLO; MWANAMUZIKI NYOTA WA KIKE ANAYETIKISA DRC

WASWAHILI wana msemo unaosema, nyota njema huonekana asubuhi. Hivyo ndivyo ilivyojidhihirisha kwa mwanamuziki mpya wa kundi la Wenge Musica Maison Mere, Lisungi Kabedi Sarah Urielle, maarufu kwa jina la Sarah Solo.

Mwanadada huyo ametokea kuwa maarufu baada ya kufuzu majaribio aliyofanyiwa na kundi la Wenge Musica Maison Mere na kutambulishwa mbele ya mashabiki, katika onyesho lililofanyika hivi karibuni, kwenye ukumbi wa Zamba Playa.

Ukumbi huo ulioko mjini Kinshasa, ndio unaotumiwa na kundi hilo kufanya mazoezi na pia ndio uliotumika kumtambulisha Sarah Solo, ambaye aliwahi kufanya shughuli za muziki nchini Ivory Coast, kwa miaka kadhaa, akiwa mwanamuziki wa kujitegemea.

Katika onyesho hilo, Werrason alitumia dakika kama 10, kumtambulisha Sarah, akielezea uwezo na umahiri wake wa kupiga gita la solo na kuimba huku mashabiki wakimsikiliza kwa makini.

Baadaye Werrason alimpa nafasi mwanamama huyo ya kuwasalimia mashabiki. Akazungumza maneno machache kisha akalifuata gita la solo mahali lilipokuwa, akalivaa mwilini huku akilitazama kwa makini kama mtu anayeajabia kitu fulani.

Werrason akamtazama binti huyo kwa makini kisha akatabasamu na kutamka neno moja 'solo'. Sarah akaitikia kwa kupiga mdonoo mmoja wa gita. Werrason akaita tena kwa mara ya pili 'solo'. Sarah akajibu kwa kupiga mdonoo wa pili wa gita.

Ni kuanzia hapo mashabiki wakaanza kulipuka mayowe ya kumshangilia. Kuona hivyo, Werrason akawauliza wanataka mipigo gani ya solo kutoka kwa Sarah. Bila kumung'unya maneno wakamjibu kwa pamoja 'Sebene'.

Hapo ndipo Sarah alipoanza kuonyesha kuwa sio wa mchezo mchezo. Akaanza kufanya mavitu yake kwa kulipiga gita hilo kwa umahiri mkubwa na kuwafanya mashabiki wapagawe.

Katika onyesho hilo la utambulisho, mwanadada huyo alipiga gita hilo kwa
kunakili nyimbo zilizopigwa na wacharaza magita wa bendi hiyo, ambao aidha bado wanaitumikia ama walishaondoka, kama vile Flammi Kapaya, Kimbangu, Burkina Wasewa ‘Mbokalia’ na wengineo.

Ilikuwa raha iliyoje kumshuhudia mwanamama huyo akilidonoa gita hilo kwa staili za kuvutia huku baadhi ya mashabiki wakiufananisha umahiri wake huo na ule waliokuwa nao wakongwe Diblo Dibala, Dally Kimoko na Nene Tchakou.

Sarah, aliyekuwa amevalia blauzi iliyoungana na kaptula ya rangi ya kahawia, na ambaye hupenda kusuka nywele zake kwa staili ya mabutu, alikoleza starahamu ukumbini kwa kupiga gita hilo huku akiwa anayumba stejini, mithili ya mtu aliyetaka kuanguka.

Werrason akatoa ishara ya kusimamisha muziki kisha akaanza kuimba kibwagizo cha moja ya nyimbo zake maarufu. Baadaye akatoa ishara ya muziki kuendelea. Sarah akaendelea kufanya mavitu huku akitikisa kichwa chake na kurusha miguu yake huku na huko.

Baadhi ya mashabiki walishindwa kuvumilia, wakavamia stejini na kuanza kumtuza fedha lukuki huku wengine wakicheza kwa kufuatisha mapigo ya ala na kumshangilia kwa nguvu.

Wapiga picha nao wakawa wakipigana vikumbo stejini ili kupata picha nzuri za mwanamama huyo akiwa anacharaza gita la solo. Kwa hakika ilifurahisha kumkodolea macho.

Ili kudhihirisha kwamba Sarah hakuwa wa kawaida, Werrason akampa nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuimba na kupiga gita. Naye hakufanya ajizi. Akawaongoza wanamuziki wenzake kupiga kibao cha Nakei Nairobi cha kundi la Afrisa International, kilichoimbwa na mkongwe Mbilia Bel.

Mshangao waliokuwa nao mashabiki kwa Sarah, pia ndio waliokuwa nao wanamuziki wa Wenge Musica Maison Mere. Baadhi ya wakati wanamuziki hao walijikuta wakimkodolea macho mwanadada huyo mithili ya watu waliokuwa wakistaajabu kumuomba kiumbe mpya aliyeteremshwa na Mola moja kwa moja kutoka mbinguni.

Sarah alizaliwa katika Jiji la Kinshasa na kuanza shughuli za muziki akiwa na umri wa miaka 12. Bendi yake ya kwanza ilikuwa Lavoniora Esthetique, iliyokuwa ikiongozwa na Dakumuda New Man.

Baada ya kudumu kwenye bendi hiyo kwa miaka saba, alijiunga na bendi ya Bana Ok inayoongozwa na mkongwe, Lutumba Simaro hadi mwaka 2012, alipoamua kuhamia nchini Ivory Coast kwa lengo la kusaka mafanikio zaidi.

Akiwa nchini humo, Sarah aliamua kuwa mwanamuziki wa kujitegemea, akirekodi na wanamuziki mbalimbali wa DRC waliokwenda huko kufanya maonyesho ya muziki.

Akimuelezea mwanadada huyo, Lutumba alisema ni mwenye uwezo wa kuelewa mafundisho kwa haraka na pia msikivu na mwenye adabu na tabia njema.

Sunday, April 9, 2017

HATIMAYE ROMA MKATOLIKI APATIKANA AKIWA MZIMA WA AFYA


HATIMAYE kitendawili cha kutekwa kwa msanii nyota wa muziki za bongo fleva, Ibrahim Mussa, maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki kimeteguliwa baada ya jana kuonekana katika kituo cha polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam.

Roma na wenzake wawili, waliodaiwa kutekwa hivi katibuni, walionekana kituoni hapo wakihojiwa na polisi kuhusu kutoonekana kwao kwa zaidi ya siku tano.

Madai ya kutekwa kwa wasanii hao, ambayo yalitapakaa kila kona ya nchi na kuzua taharuki miongoni mwa mashabiki, yalisababisha baadhi ya wasanii kupatwa na wasiwasi kuhusu hatma ya maisha yao na kulitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta kwa udi na uvumba.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwenye kituo hicho cha polisi kilieleza kuwa, Roma na wenzake hao walifikishwa kituoni hapo asubuhi. Hata hivyo, hakikueleza walifikishwa kituoni hapo kwa tuhuma zipi.

" Ni kweli kuwa Roma na wenzake wapo hapa na wapo katika hali nzuri. Kinachofanyika sasa ni kuwahoji ili kujua walikuwa wapi na kama ni kweli walitekwa na hao waliowateka ni kina nani,"kilisema chanzo hicho.

Hadi ilipofika saa 11 jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda hakuweza kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.

Roma na wenzake wanadaiwa kutekwa nyara wakati walipokuwa kwenye studio za Tongwa Records, Dar es Salaa, Ilidaiwa kuwa, watu waliowateka pia waliondoka na kompyuta na seti ya televisheni ya studio hiyo.


YANGA YAPATA USHINDI MWEMBAMBA KWA WAALGERIA


BAO lililofungwa na kiungo Thabani Kamusoko jana liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya MC  Alger ya Algeria katika mechi ya awali ya hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kamusoko alifunga bao hilo dakika ya 61 kwa shuti kali baada ya gonga safi kati yake, Haruna Niyonzima na Simon Msuva.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inahitaji sare ya aina yoyote timu hizo zitakaporudiana wiki ijayo mjini Algiers.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa soka wameilaumu Yanga kwa kushindwa kuondoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao kwa vile wapinzani wao walicheza kwa kasi ndogo huku wakionekana dhahiri kutafuta sare.

Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wachache, Yanga ilipata nafasi nzuri kadhaa za kufunga mabao, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake, Obrey Chirwa, Deus Kaseka na Msuva kutokana na kukosa umakini kila walipolikaribia lango la wapinzani wao.

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWAALIKA SERENGETI BOYS NYUMBANI KWAKE KWA AJILI YA CHAKULA USIKU
Monday, April 3, 2017

SIMBA YAPIGWA MWELEKA 2-1 NA KAGERA SUGAR


MATUMAINI ya Simba kutwaa taji la ligi kuu ya Tanzania Bara yameanza kuota mbawa baada ya kupigwa mweleka wa mabao 2-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kipigo hicho kimeifanya Simba iendelee kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 55, nyuma ya mabingwa watetezi Yanga wanaoongoza kwa kuwa na pointi 56.

Washambuliaji wa zamani wa Simba, walioachwa kwa madai ya viwango vyao kushuka, Mbaraka Yussuf na Christopher Edward, ndio waliopeleka kilio Msimbazi baada ya kuifungia Kagera Sugar mabao hayo mawili.

Mbaraka, mchezaji kinda kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa  Stars, aliifungia Kagera Sugar bao la kwanza dakika ya 27 kwa shuti kali lililomshinda kipa Daniel Agyei wa Simba. Bao  hilo lilidumu hadi mapumziko.

Christopher, aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 50 baada ya gonga safi kati yake na washambuliaji wenzake wa Kagera.

Bao la kujifariji la Simba lilifungwa na Muzamil Yassin dakika ya 65 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Kagera.

Simba ilijitahidi kucheza kufa na kupona ili kusawazisha, lakini kikwazo kikubwa kilikuwa kipa wa zamani wa timu hiyo, Juma Kaseja, aliyekaa imara kwenye lango la Kagera.

Sunday, April 2, 2017

YANGA YAIENGUA SIMBA KILELENI MWA LIGI KUU


BAO lililofungwa na mashambuliaji Obrey Chirwa katika kipindi cha pili, jana liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuiengua Simba kileleni mwa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 56. Simba inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 55.

Hata hivyo, Simba inaweza kurejea kileleni mwa ligi hiyo leo, iwapo itaishinda Kagera Sugar, katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

SERENGETI BOYS YAITUNGUA TENA BURUNDITIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kirafiki baada ya  kuifunga Burundi mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Serengeti Boys baada ya juzi kuichapa Burundi mabao 3-0 katika mchezo mwingine wa kirafiki.
Katika mechi hiyo, Kocha Bakari Shime, anayefanya kazi chini ya Mshauri wa Ufundi, Kim Poulsen, alifanya mabadiliko makubwa kikosini mwake, akiwapa nafasi zaidi wachezaji ambao hawakucheza mechi ya kwanza.
Wafungaji wa mabao ya Serengeti Boys walikuwa Issa Abdi Makamba dakika ya 36 na Ibrahim Abdallah Ali dakika ya 89.
Serengeti Boys ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku wapinzani wao wakicheza rafu nyingi. 
Serengeti Boys imerejea Dar es Salaam, ambako kesho watakuwa na mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Ghana, kabla ya kwenda Morocco kwenye kambi ya mwezi mmoja, kujiandaa na fainali za U-17 Afrika, Mei mwaka huu nchini Gabon.

Thursday, March 30, 2017

MECHI YA AZAM, NDANDA FC KUPIGWA USIKU

Robo Fainali ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Azam FC na Ndanda FC itafanyika Aprili 5, 2017 saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, imefahamika.

Kadhalika, Robo Fainali ya nne ya mwisho ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC itafanyika Aprili 22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Washindi wa kila mchezo watasonga mbele kwenda Raundi ya Nane ambayo ni Nusu Fainali. Tayari klabu za Mbao na Simba zilitangulia hatua hiyo ya Nusu Fainali.

Mbao FC ya Mwanza nayo imetangulia hatua ya Nusu Fainali baada ya kuilaza Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo wa Robo Fainali ya kwanza uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 18, mwaka huu.

Kwa upande wake, Klabu ya Simba ya Dar es Salaam imepita baada ya kuishinda Madini FC ya Arusha kwa bao 1-0 katika mchezo wa Robo Fainali ya pili uliofanyika Machi 19, 2017 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

CAF YAIGOMEA YANGAUongozi wa klabu ya Yanga umethibitisha mchezo wao wa kimataifa wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya MC Algers sasa utachezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Awali kulikuwepo na taarifa kuwa mchezo huo ungechezwa jijini Mwanza lakini kufuatia klabu ya Yanga kuchelewesha kuwasilisha mabadiliko ya uwanja CAF,shirikisho hilo limeshindwa kutoa idhini kutumika kwa uwanja huo kwani uwanja unaotambulika ambao uliwasilishwa na klabu hiyo ni uwanja wa Taifa.

Yanga itashuka dimbani kumenyana na MC Algers siku ya tarehe 8 ya mwezi wa nne mwaka huu katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika ambapo mshindi wa jumla atafuzu kucheza hatua ya makundi.

TAIFA STARS YAIPIGA BURUNDI 2-0


MSHAMBULIAJI kinda wa Kagera Sugar, Mbaraka Yussuf jana aliibuka shujaa wa timu ya Taifa, Taifa Stars baada ya kuifungia bao la pili na la ushindi dhidi ya Burundi.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yussuf, ambaye apelekwa Kagera Sugar kwa mkopo akitokea Simba, alifunga bao hilo dakika ya 77.

Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Simon Msuva katikati ya uwanja, aliyemsogezea Yussuf, ambaye alikimbia nao hadi nje kidogo ya eneo la hatari la Burundi, akafumua shuti likagonga mwamba wa goli, mpira uliporudi akauwahi na kuutumbukiza kimiani.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yussuf tangu alipoitwa kwenye kikosi hicho kwa mara ya kwanza na Kocha Mkuu mpya, Salum Mayanga, ambaye sasa ameweka rekodi ya kushinda mechi mbili.

Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 22 lililofungwa na Msuva kwa shuti kali baada ya kuuwahi mpira uliopigwa kwa kichwa na Ibrahim Ajib, aliyepewa pasi ya juu na Mohamed Hussein. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Burundi ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 53 kwa bao lililofungwa na mshambuliaji wa Simba, Laudin Mavugo, kutokana na uzembe wa beki wa kati wa Taifa Stars, Abdi Banda.

Monday, March 27, 2017

TAIFA STARS, INTAMBA MURUGAMBA KESHO JUMANNE


Taifa Stars ya Tanzania kesho Machi 28, 2017 saa 10:00 jioni inaingia tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kucheza na Intamba Murugamba ya Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kwa mujibu wa kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa ya FIFA.

Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars kucheza ndani ya wiki moja baada ya ule wa awali dhidi ya The Zebras ‘Pundamilia’ wa Botswana uliofanyika Uwanja huo wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.

Katika mchezo huo wa Jumamosi, Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa na Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya wa kikosi hicho, walishinda kwa mabao 2-0.

Tayari Intamba Murugamba wametua nchini tangu jana Jumapili saa 4.30 asubuhi na kufikia Hoteli ya De Mag iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na jioni yake walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini. Leo Jumatatu, inafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ndani ya kikosi hicho wamo washambuliaji wawili wanaotamba katika klabu za Simba na Young African za Dar es Salaam. Nyota hao ni Amisi Tambwe wa Young Africans na Laudit Mavugo wa Simba.

Leo Jumatatu Machi 27, 2017 saa 8.30 alasiri nyota hao wakiongozana na kocha wao watazungumza na wanahabari namna walivyoajiandaa kucheza na Taifa Stars ambayo pia ina nyota wengi wanaocheza na wachezaji hao wa Burundi katika klabu za Simba na Young Africans.

Wakati Mavugo ni mshambuluaji, anatarajiwa kuwa na wakati mgumu mbele ya walinzi mahiri ambao pia wako Simba kama vile Abdi Banda na Mohammed Hussein wakati Andrew Vicent anayetoka Young African atakuwa kisiki kwa Tambwe wanayecheza naye timu moja kama makocha watawapanga.

Kwa upande wake, Mayanga alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi iliyopita dhidi ya The Zebras ya Botswana na hivyo amehimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho.

Katika kuunga mkono wito wa Kocha Mayanga, TFF imebakiza viingilio vya mchezo huo kuwa sawa na vile vya Jumamosi iliyopita kwani katika mzunguko ambao unachukua mashabiki wengi kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000.

Kwa upande wa VIP “A” Kiingilio kitakuwa ni Sh 15,000 wakati VIP “B” na VIP “C” kiingilio kitakuwa ni Sh 10,000. Viingilio hivyo vimelenga kuwaalika Watanzania wengine kwenda uwanjani.

DK. MWAKYEMBE HATAKI KUFUNGWAFUNGWA


Waziri wa Mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ameanza kazi katika Wizara mpya kwa pongezi kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kuasisi mageuzi ya Kandanda nchini.

 "Watanzania tumechoka na huu uteja, kusukumwa sukumwa tu kwenye soka. Ni hamu ya watanzania sasa tuonekane katika ulimwengu wa soka", amesema Waziri Dk. Mwakyembe aliyezungumza na Kamati ya Hamasa kwa Serengeti Boys alipokutana nayo kwa mara ya kwanza jana Machi 25, mwaka huu.

Waziri alikwenda mbali kwa kuiagiza Wizara yake yote ijikite kuhakikisha maandalizi ya Serengeti Boys yanakamilika kwa wakati.

"Nataka Wizara yangu yote sasa wimbo wetu uwe Serengeti Boys," amesema Dk. Mwakyembe.

Katika hafla hiyo, Dk Mwakyembe amempongeza mtangulizi wake, Mheshimiwa Nape Nnauye kwa kuunda Kamati ya Serengeti Boys ili kutoa hamasa ya Watanzania kwa timu yao.

Alisema Serengeti Boys ni nyota wanaoinukia (upcoming stars) na wanampa sababu ya kuanza kwenda mpirani tena.

Waziri Dk Mwakyembe aliendelea kusema kuwa michezo ya leo inahitaji uwekezaji hivyo Wizara yake itahakikisha kuwa jukumu hilo analibeba.

"Naona kama imechelewa, lakini bado muda upo, tukimbie, nataka Wizara nzima wimbo wetu uwe Serengeti Boys", alisema kwa hamasa kubwa.

Dk Mwakyembe amempongeza Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Serengeti Boys, Charles Hilary kwa mafanikio ya program ya mageuzi ya soka nchini.

Naye Mkurugenzi wa Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yussuf Singo alisema sasa imechoka kuwa kichwa cha mwenda wazimu na hivyo Taifa limeazimia kucheza Kombe la Dunia kupitia vijana wa Serengeti Boys.

Rais wa Shirikisho la Kandanda Tanzania, Jamal Malinzi alisema kufuzu kwa Serengeti Boys kucheza fainali za AFCON ni sifa pekee na mwanzo mpya wa mageuzi makubwa ya soka la Tanzania.

Amesema maandalizi ya ushiriki wa fainali za AFCON zitahitaji takriban Shilingi bilioni moja.

Amesema mikakati mbalimbali imeandaliwa kuchangisha kiasi hicho cha fedha, ikiwa ni pamoja na kuandaa chakula cha hisani.

Waziri Mwakyembe amesema atahakikisha fedha hiyo inapatikana ili vijana wa Serengeti Boys waweze kufuzu kucheza kombe la dunia huko India mwishoni mwa mwaka huu.

SERENGETI BOYS WAKO BUKOBA, IKIRUDI KUIVAA GHANA


Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya vijana wenye umri wa miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys imetumia ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam alfajiri ya leo Machi 26, mwaka huu na kutua Bukoba mkoani Kagera kwa kambi ya wiki moja.

Serengeti Boys itakuwa kambini Bukoba hadi Aprili 2, mwaka huu ambako inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu vijana ya Burundi kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera. Michezo hiyo itafanyika Machi 30, 2017 na kurudiana Aprili mosi, mwaka huu.

Serengeti Boys ambayo inajiandaa na michuano Afrika huko Gabon itarejea Dar es Salaam Aprili 2, mwaka huu ambako imepangwa kucheza na Ghana Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mchezo huo utatanguliwa na hafla ya kuagwa kwa kukabidhiwa bendera.


Timu itaelekea Morocco Mei 5, mwaka huu baadaye itapita Cameroon kwenye kambi ya zaidi ya mwezi mmoja baadaye itakwenda Gabon katika michuano itakayoanza Mei 14, 2017. Ikiwa Cameroon itacheza mechi mbili za kimataifa dhidi ya wenyeji kabla ya kwenda kwenye fainali.

Serengeti Boys ni timu ya vijana ambayo imefuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu. Timu hiyo imepangwa Kundi ‘B’ pamoja na mabingwa watetezi Mali, Niger na Angola. Ina lengo la kurejea na Kombe la Afrika kwa vijana.

La ikitokea imekosa nafasi hiyo angalau ikafika nusu fainali ambako kwa mafanikio hayo itakuwa tayari ina tiketi mkononi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia huko India, Novemba, mwaka huu.

Kikosi cha Serengeti Boys kinaundwa na Makipa:  Ramadhan Kabwili, Samwel Edward na Kelvin Kayego.

Walinzi:  Kibwana Ally Shomari, Nickson Kibabage, Israel Mwenda, Dickson Job, Ally Msengi, Issa Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.

Viungo: Kelvin Nashon Naftali, Ally Ng’anzi, Mohamed Rashid, Shaaban Ada, Mathias Juan, Marco Gerald, Abdulhamis Suleiman, Saidi Mussa na Cyprian Benedictor Mtesigwa.

Washambuliaji:  Muhsin Malima Makame, Yohana Mkomola, Ibrahim Abdallah, Assad Juma na Abdul Suleiman.

Benchi la Ufundi:
Bakari Shime (Kocha Mkuu)
Oscar Mirambo (Kocha Msaidizi)
Muharami Mohamed (Kocha wa makipa)
Kim Poulsen (Mshauri wa Ufundi)
Edward Evans (Mtunza Vifaa)
Shecky Mngazija (Daktari wa timu)
 

KAMATI YA UCHAGUZI TAFCA KUKUTANA JUMAMOSI

Kamati ya Utendaji ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu (TAFCA) Mkoa wa Kinondoni inakutana Jumamosi (Aprili 1, 2017) kupata tarehe ya uchaguzi mkuu wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mbwana Makata (0655520129), Mkutano huo wa Kamati ya Utendaji ya TAFCA Kinondoni utaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Eliutery Mholery (0715621667).

Alisema mbali ya ajenda hiyo, pia Kamati hiyo itaanda taarifa ya utendaji pamoja na taarifa ya fedha ambazo zitawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Kawaida wa chama hicho kabla ya ajenda ya uchaguzi.

Makata alisema pia Kamati yao itajadili uhai wa wanachama wao, hivyo kuwataka ambao hawajalipa ada za uanachama kufanya hivyo haraka ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Alisema makocha wote wa Kinondoni ambao ndiyo wanachama wa chama hicho wanatakiwa kulipia ada zao kupita TAFCA Taifa au kwa Mhazini wa TAFCA Kinondoni.

TFF YAWATIA HATIANI VIONGOZI WATATU RUREFAKamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewatia hatiani viongozi watatu akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA), James Thomas Makwinya.

Viongozi wa RUREFA waliotiwa hatiani ni pamoja na Blassy Kiondo na Kaimu Katibu Mkuu, Ayoub Nyauringo ambao Kamati ya Nidhamu chini ya Mwenyekiti Abbas Tarimba iliyosikiliza shauri hilo zaidi ya mara tatu kabla ya kufikia uamuzi.

Blassy Kiondo

Baada ya Blassy Kiondo kutiwa hatiani, Kamati imechukua uamuzi wa kumfungia kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje kwa mwaka mmoja kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za TFF, Kanuni ya 64 (4) na inamuamuru kulipa faini ya Sh. 1,000,0000 (Milioni moja) kwa mujibu wa Kanuni ya ya 64 (1) (a) ya Kanuni za nidhamu za TFF. Mlalamikiwa ana haki ya kukata rufaa kama kanuni zinavyoelekeza.

Awali, Kiondo alilalamikiwa na TFF kuwa alishindwa kuheshimu uamuzi halali wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF kinyume cha kanuni ya 64 ya kanuni za Nidhamu za mwaka 2012.

Kwamba akiwa Mwenyekiti wa RUREFA, anadaiwa kuwa kati ya Desemba 2016 na Januari 2017, alipuuza maelekezo ya kusimamisha uchaguzi wa RUREFA hadi hapo rufaa zilizokuwa zimekatwa kuamuliwa. Kadhalika, Kiondo alishiriki katika uchaguzi huo.

Ayoub Nyauringo

Kamati kwa kauli moja, imemtia hatiani Ayoub Nyauringo amefungiwa kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa muda wa mwaka mmoja chini ya Kanuni ya 64(4)  za nidhamu za TFF. Hiyo ni adhabu kama alivyoshitakiwa ili iwe fundisho kwa viongozi wengine katika kutii maagizo wanayopewa na ngazi za juu za uongozi.

Awali, Nyauringo alilalamikiwa na TFF kuwa alishindwa kuheshimu uamuzi halali wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF kinyume cha kanuni ya 64  ya kanuni za Nidhamu za mwaka 2012.

Kwamba akiwa Kaimu Katibu wa RUREFA, anadaiwa kuwa kati ya Desemba 2016 na Januari 2017, alipuuza maelekezo ya kusimamisha uchaguzi wa RUREFA hadi hapo rufaa zilizokuwa zimekatwa kuamuliwa.

Katika utetezi wake, Nyauringo mbele ya Kamati ya Nidhamu ya TFF alikiri kupokea barua ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi kama ilivyoagizwa, lakini ushauri wake haukufanyiwa kazi wala kusikilizwa bali aliambiwa kwamba Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA inafanyia kazi na uchaguzi upo pale pale.

Kamati baada ya kupitia ushahidi wote imejiridhisha bila shaka yoyote kuwa mlalamikiwa alitenda kosa analoshitakiwa nalo na kushindwa kuheshimu uamuzi wa TFF; sababu zikiwa ni nyingi ikiwamo kukiri kuwa mchakato wa uchaguzi ulisitishwa sambamba na kukosa Mwakilishi kutoka TFF. Mlalamikiwa ana haki ya kukata rufaa kama kanuni zinavyoelekeza.

James Makwinya

Kuhusu James Makwinya, Kamati inamtia hatiani mlalamikiwa kwa makosa mawili kama alivyoshitakiwa na TFF. Kwamba Mlalamikiwa alishindwa kuheshimu uamuzi halali  wa Kamati ya Uchaguzi  ya TFF na vilevile imethibitishwa kuwa alitoa lugha isiyo ya kiungwana na kiuanamichezo kama ushahidi unavyooneshwa hapo juu.

Katika shitaka la kwanza mlalamikiwa anafungiwa kutojihusisha kwa namna yoyote ile na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kipindi cha mwaka mmoja kwa mujibu wa Kanuni ya 64 (4) ya kanuni za nidhamu za TFF pamoja na kulipa faini ya Sh. Milioni moja kwa mujibu wa kanuni ya 64 (1) (a)ya kanuni za nidhamu.

Hii ni kwa sababu imethibitika kuwa mlalamikiwa alipokea barua ya Desemba 19, 2016 iliyomtaka kusitisha mchakato wa uchaguzi wa RUREFA. Alikaidi maagizo hayo na kuendeleana uchaguzi bila uhalali wowote na bila kuwepo mwakilishi yeyote kutoka TFF. Mlalamikaji ana haki ya kukata rufaa kama kanuni zinavyoelekeza.

Sunday, March 26, 2017

TAIFA STARS YAWAPA RAHA WATANZANIA, YAWATUNGUA BOTSWANA MABAO 2-0, SAMATTA ATUPIA ZOTE MBILI

MABAO mawili yaliyofungwa na nahodha Mbwana Samatta, jana yaliiwezesha timu ya Taifa, Taifa Stars kuibwaga Botswana mabao 2-0 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbwana alifunga bao la kwanza dakika ya pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shiza Kichuya na kumtoka beki Kaone Vanderwesthuizem kabla ya kupiga shuti lililompita kipa Kabelo Dambe wa Botswana.

Mshambuliaji huyo anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Genk ya Ubelgiji, aliongeza bao la pili dakika ya 87 kwa shuti la mpira wa adhabu lililotinga moja kwa moja wavuni.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Taifa Stars mwaka huu na pia ya kwanza kwa kocha mpya, Salum Mayanga, aliyerithi mikoba ya Charles Boniface, aliyejiuzulu mapema mwaka huu.

Katika mechi hiyo, Mayanga aliwachezesha wachezaji wengi chipukizi, wakiwemo aliowaita kwa mara ya kwanza, ambao walionyesha kiwango kizuri cha soka na kuwapa raha mashabiki.

Iwapo mshambuliaji Simon Msuva angekuwa makini, Taifa Stars ingeweza kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao, lakini alipoteza umakini kwa kupiga mashuti nje ya lango.

Saturday, March 25, 2017

TAIFA STARS KUJIPIMA NGUVU KWA BOTSWANA LEO


Na Alex Matias,Dar es salaam
Nahodha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta amedai mabadiliko ya kikosi cha timu hiyo yaliyofanywa na Kocha Mkuu, Salum Mayanga hayawezi kuathiri nguvu na mipango yao ya kupambana katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Botswana utakaopigwa jioni ya Leo uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Alisema Kocha Mayanga aliamua kufanya mabadiliko hayo kutokana na kutambua udhaifu uliopo kwenye kikosi hicho, hivyo kuamua kuwaita wachezaji wengine wapya ambao wataleta chachu ya ushindi kwa timu hiyo iliyo katika nafasi ya mbaya ya msimamo wa viwango vya Shirikisho la Soka Duniani(FIFA) vilivyotolewa hivi karibuni.
Samatta alisema ni kweli timu ya Taifa inahitaji wachezaji wazoefu watakaoendeleza mbinu zitakazotolewa na Kocha Mkuu lakini wengi wa wachezaji wakongwe waliopo kwenye timu hiyo walishindwa kuonesha uwezo wao na hatimaye kuipeleka timu mahali pasipo stahili kuelekea.
“Nasikia jinsi watu wanavyolaumu uamuzi uliofanywa na Kocha Mayanga, lakini mi nataka niwaambie ukweli Watanzania kwamba hawa wachezaji ambao wanawasema ni wakongwe ni lazima na wao wakae pembeni wawapishe wachezaji wapya waoneshe uwezo na kitu kipya walichokuwa nacho ambacho kitakuja kuliinua taifa katika anga la kimichezo,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Kocha Mayanga, alisema mchezo huo ni wa kwanza kwake utampatia nafasi ya kujua mapungufu na uhiamara wa kikosi chake kabla ya kuelekea kwenye michuano ya AFCON inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Juni mwaka huu.
Alisema kutokana na mazoezi mazuri waliyoyafanya kwa siku nne mfululizo yatawasaidia kuibuka na ushindi mkubwa pamoja picha ya ubora wa kikosi hicho chenye malengo ya kupanda maradufu kwenye viwango vya FIFA.
Alidai anaamini wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho watatumia akili na nguvu zao zote ili kuhakikisha Botswana haichomoki na ushindi wa aina yoyote ile huku akiwataka watanzania kujenga imani na kikosi hicho chenye wachezaji vijana zaidi.
“Kwenye kikosi chetu hiki safari hii kuna wachezaji wengi ambao ni vijana, niliwaamini na ndio maana nikaamua kuwaita kwenye kikosi change, kwahiyo Watanzania tarajieni makubwa zaidi katika mchezo wetu huu wa kesho(leo) utakaopigwajijini Dar es Salaam,” alisema Mayanga.
Alisema ni vigumu kutoa ahadi katika mchezo wa mpira wa miguu kutokana na kwamba hawajui timu wanayokwenda kushindana nayo imejiandaa vipi dhidi ya mchezo huo ambao unaumuhimu mkubwa kwa pande zote  mbili.
Wakati huohuo, Kocha wa Timu ya Botswana, Peter Buttler alisema wanauchukulia mchezo wao wa kirafiki na Taifa Stars kuwa ni zaidi ya wa kirafiki kutokana na kuona umuhimu uliopo kwenye mchezo huo ambao unatambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na (FIFA).
“Tumekuja Tanzania kupambana na naomba niwashukuru kwa ukarimu wao wote waliotuonesha ila kiukweli ni lazima tuibuke na ushindi kwa gharama yoyote ile kwa sababu tunataka tupande zaidi kwenye msimamo wa viwango vya soka katika mataifa ya Afrika tofauti na hivi ilivyo sasa,” alisema Buttler.
Mbali na hilo, Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Alfred Lucas alitoa taarifa za kubadilishwa kwa kiwango cha chini cha gharama za kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo ambapo hapo awali ilikuwa ni Tsh. 5,000 na sasa kuwa ni Tsh.3,000.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA FULL SHANGWE