'
Tuesday, October 24, 2017
KUZIONA SIMBA, YANGA BUKU KUMI, MECHI KUCHEZWA SHAMBA LA BIBI
KIINGILIO cha chini katika mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Oktoba 28, kitakuwa ni Sh 10,000.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam kwamba kiingilio hicho kitahusu majukwaa ya mzunguko ya Uwanja huo, wakati jukwaa kuu watu watalipa Sh. 20,000.
Kidau amesema kwamba utaratibu maalum umewekwa kuhakikisha idadi inayotakiwa ya watu 22,000 ndiyo wanaoingia uwanjani kwa kuhakikisha haziuzwi tiketi zaidi.
Aidha, kiungo huyo wa zamani wa Simba SC, amesema kwamba imelazimika mchezo huo kufanyika Uwanja wa Uhuru kwa sababu Uwanja mkubwa wa Taifa upo kwenye ukarabati.
Kidau pia amesema kwamba Alhamisi wiki hii Kamati mpya ya Uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) ya TFF itafanya kikao chake cha kwanza mjini Dar es Salaam, kubwa likiwa ni maandalizi ya mchezo huo.
Lakini pia, Kidau amesema kwamba ajenda nyingine katika kikao hicho ni kuteua Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, na Kamati nyingine mbalimbali.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amesema kiingilio cha chini Simba na Yanga ni Sh. 10,000
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment