KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 4, 2017

AVEVA, KABURU WAZIDI KUSOTA RUMANDE




Na Furaha Omary

UPELELEZI wa kesi inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu' bado haujakamilika.

Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter akishirikiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, walidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo walidai mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa kutajwa, ambapo waliomba kuahirishwa hadi tarehe nyingine.

Hakimu Mwambapa aliahirisha shauri hilo hadi  Oktoba 11, mwaka huu, kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa mahabusu.

Mara ya mwisho, upande wa jamhuri uliieleza mahakama kuwa jalada la shauri hilo liko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), hivyo wanasubiri lirejeshwe ili kujua kinachoendelea na usikilizwaji wa shauri kama DPP atakuwa amejiridhisha na uchunguzi kuwa umekamilika.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano, yakiwemo ya kutakatisha fedha, hivyo kuwafanya wakae mahabusu kwa kuwa shitaka hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mashitaka mengine yanayowakabili ni  kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za Marekani  300,000.

Washitakiwa hao wanadaiwa Machi Machi 15, mwaka jana,  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 5, mwaka jana,  wakionyesha klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati siyo kweli.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa  Machi 15, mwaka jana, katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe, Ilala, Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo, ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016, wakati akijua ni kosa.

Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29, mwaka jana, Dar es Salaam, kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15, mwaka jana, katika benki ya Barclays, Mikocheni, alijipatia USD 300,000, wakati akijua zimetokana na kughushi.

Nyange anadaiwa kuwa Machi 15, mwaka jana, katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni, alimsaidia Aveva kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.




No comments:

Post a Comment