KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 28, 2011

Azam: Yanga ivunje benki kumrejesha Ngasa



UONGOZI wa klabu ya Azam umesema, hakuna klabu ya ligi kuu yenye uwezo wa kumsajili mshambuliaji Mrisho Ngasa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Nassoro Idrisa alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, timu inayotaka kumsajili mshambuliaji huyo, inapaswa kuwa imejiandaa vilivyo.
Nassoro alisema Ngasa ana mkataba wa kuichezea Yanga kwa miaka miwili, hivyo iwapo kuna klabu inamuhitaji, inapaswa kulipa gharama za kuvunja mkataba huo.
Alisema hadi sasa hakuna kiongozi wa klabu yoyote, aliyewasiliana nao kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo zaidi ya kupata taarifa hizo kupitia kwenye vyombo vya habari.
“Tunasikia tu kwamba Yanga inataka kumrejesha Ngasa kwao, sisi hatuna pingamizi, lakini wanapaswa kuelewa kwamba gharama za kuvunja mkataba wake ni kubwa, ni mara mbili ya mkataba alionao na Azam,”alisema.
Ngasa alisajiliwa na Azam msimu uliopita akitokea Yanga. Usajili wa mshambuliaji huyo uliigharimu Azam sh. milioni 50.
Kumekuwepo na tetesi kwamba, uongozi wa Yanga unataka kumrejesha mchezaji huyo Jangwani baada ya yeye mwenyewe kuonyesha yupo tayari kufanya hivyo.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Seif Mohamed alikiri kuwa, bado hawajakutana na uongozi wa Azam kwa ajili ya usajili wa mchezaji huyo.
Hata hivyo, Seif alisema upo uwezekano wa klabu yake kumrejesha Ngasa, lakini itategemea uamuzi wa wanachama na benchi la ufundi.
“Azam wanasema wanahitaji pesa nyingi, mbona wao walipokuja kwetu, tulikaa na kuzungumza, hivyo hata nasi tunaweza kukutana nao na gharama za uhamisho wake zisiwe kubwa,”alisema.
Wakati huo huo, uongozi wa Azam umesema utatangaza kikosi chao kipya Juni 10 mwaka huu baada ya kukamilisha taratibu za usajili wa wachezaji wapya.
Katibu Mkuu wa Azam, Nassoro Idrisa alisema juzi kuwa, kikosi hicho kitaanza mazoezi siku hiyo hiyo kwenye uwanja wao uliopo Mbande, Temeke, Dar es Salaam.
Nassoro alisema hadi juzi walikuwa wameshafanikiwa kumsajili kipa wa zamani wa Yanga, Obren Curkovic na bado wanaendelea na kazi ya kuziba baadhi ya mapengo ya wachezaji watakaoachwa.

No comments:

Post a Comment