KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 28, 2011

Rage awatangazia vita mafisadi Simba



MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amekuwa mbogo baada ya kudai kwamba, kamwe hawezi kuacha baadhi ya watu wakinufaika na klabu hiyo.
Rage amesema ni makosa makubwa kwa watu hao kuitumia Simba kwa manufaa yao huku wachezaji, ambao ndio wavuja jasho wakiishi maisha duni na kupata mapato madogo.
Mwenyekiti huyo wa Simba alielezea msimamo wake huo juzi mjini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na Burudani kuhusu mikakati yake ya kuiwezesha klabu hiyo ijitegemee.
Alisema katika kutekeleza azma yake hiyo, ameamua kuwashirikisha viongozi wenzake ili kupambana na watu hao na kuitokomeza kabisa tabia hiyo.
Rage alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha mapato yote ya klabu yanaingia sehemu husika na wachezaji wanapata malipo yao halali kulingana na mikataba yao.
"Simba ni klabu kubwa, inazo mali nyingi, yakiwemo majengo na viwanja, lakini nimebaini kwamba wapo baadhi ya watu wananufaika navyo huku klabu ikiendelea kukabiliwa na hali mbaya,"alisema kiongozi huyo ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini.
Alisema kwa sasa bado wanaendelea kupitia mikataba yote ya wapangaji katika majengo ya klabu hiyo ili kujua uhalali wa malipo yao na mengine.
Kiongozi huyo wa juu wa Simba alisema, wakati umefika kwa watu hao kuacha mara moja tabia ya kuitumia klabu hiyo kama mtaji na kusisitiza kuwa hayupo tayari kuwafumbia macho.
"Mimi nilikuwa mchezaji hapa Simba, naona jinsi wachezaji wanavyoumia kwa ajili ya kuitetea klabu wakati kuna baadhi ya watu wanakula fedha za klabu kiulaini, nitaanza na watu hao, "alisema.

No comments:

Post a Comment