KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 26, 2011

Yanga kuilipa CECAFA mil. 52/-?


KLABU ya Yanga imesema ipo tayari kulipa faini ya dola 35,000 za Marekani (sh. milioni 52) ilizotozwa mwaka 2008 na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wapo tayari kulipa faini hiyo ili waweze kushiriki michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu.
CECAFA imeamua kuhamishia michuano hiyo nchini Tanzania kutoka Sudan, kufuatia mapigano yaliyozuka nchini humo kati ya majeshi ya Sudan na Sudan Kusini.
Kwa mujibu wa kanuni za baraza hilo, nchi mwenyeji huwakilishwa na timu mbili, bingwa wa ligi na mshindi wa pili. Simba itashiriki michuano hiyo ikiwa bingwa wa ligi ya mwaka jana wakati Yanga ilishika nafasi ya pili.
Yanga ilitozwa faini hiyo na CECAFA baada ya kugoma kucheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo kati yake na Simba mwaka 2008 mjini Dar es Salaam, ikitaka ilipwe dola 50,000.
Mbali na kutozwa faini, Yanga pia ilifungiwa kushiriki katika michuano hiyo kwa miaka mitatu. Adhabu hiyo inatarajiwa kumalizika mwaka huu.
“Tunataka kushiriki katika michuano ijayo ya Kombe la Kagame, ambayo pia tutaitumia kukipima kikosi chetu kabla ya mashindano ya klabu bingwa Afrika,”alisema Mwesigwa.
“Tunataka kulimaliza sakata hili. Kwa sasa, tunajadiliana na viongozi wa CECAFA kwa lengo la kulipa faini hiyo. Tunaguswa sana kwa sababu ni pesa nyingi, lakini hatuna jinsi,”aliongeza.

'Barcelona isipotwaa ubingwa, naacha Pombe'

BAADHI ya mashabiki wa soka nchini wameweka nadhiri, viapo na wengine kucheza kamari ya fedha kuhusu mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Mchezo huo utakaopigwa keshokutwa kwenye uwanja wa Wimbley mjini London, England umewagawa mashabiki wa soka nchini, kila upande ukiitabiria mema timu unayoipenda.
Kwa kipindi cha takriban wiki mbili sasa, waandishi wa habari wa gazeti hili, wameshuhudia tambo na mabishano kutoka kwa mashabiki wa klabu hizo mbili kwenye kumbi mbalimbali za buudani za mjini Dar es Salaam.
Kwenye hoteli ya New Happy iliyopo eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, shabiki Hamad Jella, ameitabiria Barcelona ushindi huku akisema, iwapo timu hiyo itashindwa kuchukua ubingwa, ataacha kunywa pombe maisha yake yote na itakuwa mara ya mwisho kwenda hapo.
“Barcelona ikishindwa kutwaa ubungwa, naacha kunywa pombe na itakuwa mara yangu ya mwisho kuja kwenye baa hii,” alisikika shabiki huyo akiweka nadhiri.
Kwa upande wake, Frank Kamugisha maarufu kwa jina la Frank Manchester alisema, ameanza kushangilia ubingwa kwa kuwa dalili zote zinaonyesha Man U itashinda.
“Hii siyo mara ya kwanza kukutana na Barcelona kwenye fainali, mara ya mwisho walitufunga na baada ya hapo tumewafuatilia na kujua udhaifu wao, lazima tutashinda,” alisema Frank.
Katika klabu ya Italian House eneo la Tabata Mawenzi, mashabiki wa timu zote wameanza kutambiana huku kila upande ukipanga kufunga bendera kubwa za timu zao nje ya klabu hiyo.
“Nipo tayari kuweka shilingi laki moja kama Manchester itafungwa,” alisikika akisema Joseph Michael, ambaye alipingwa na shabiki wa Barcelona, anayefanya kazi ya uwakili, lakini hakutaka jina lake litajwe.
Mashabiki hao kila mmoja ameweka shilingi laki moja, akifagilia timu yake kuibuka na ushindi. Hata hivyo, dakika tisini ndizo zitakazomua fedha hizo zitakwenda kwa nani.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa baadhi ya maeneo nchini, mfalme wa soka duniani Pele na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa England, Garry Lineker wameitabiria ushindi Manchester United.
Kwa upande wake, Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amekiri kuwa Barcelona ya mwaka huu ni nzuri kuliko ilivyokuwa mwaka 2009.

KABURU: Hatuna mchezaji mwenye virusi vya Yanga

MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' amesema, ndani ya kikosi chao, hakuna wachezaji wenye 'virusi' vya Yanga.
Kaburu alisema hayo jana alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha michezo cha Radio One.
Alisema kikosi chao kinaundwa na wachezaji wengi waadilifu na kwamba, kamwe hawajawahi kugundua kuwepo kwa baadhi yaowenye mapenzi na mahasimu wao, Yanga.
"Mimi nasema wachezaji wote waliopo Simba wanaipenda timu yao kwa dhati na wapo kwa ajili ya kuitetea klabu yao na nchi kwa jumla,"alisema Kaburu.
Aliongeza kuwa, wapo baadhi ya watu, ambao pengine kwa kutofahamu, wanapoona mchezaji anacheza chini ya kiwango, wanahisi anatumiwa na wapinzani wao kuhujumu timu.
" Wachezaji ni binadamu, kuna siku wanaweza kuamka na kujisikia vibaya na wakipangwa, wanacheza chini ya kiwango na kushindwa kuonyesha uwezo wao,”alisema.
Amewataka wanachama na mashabiki wa Simba, kuwaamini wachezaji wanaosajiliwa na klabu hiyo kwa vile kamati ya usajili ipo makini katika kazi hiyo na haifanyikazi zake kwa kukurupuka.
Aliongeza kuwa, yeye na viongozi wenzake wa Simba wana imani kubwa na wachezaji wao na wanakwenda Misri wakiwa na uhakika mkubwa wa ushindi dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Akizungumzia usajili wa wachezaji msimu ujao, kiongozi huyo alisema wapo katika mchakato wa kumpata beki namba tano, ambaye ataziba pengo la Joseph Owino.
Owino amefanyiwa upasuaji wa goti na kutakiwa kukaa nje ya dimba kwa miezi kadhaa na kusababisha timu hiyo kuwa na pengo kubwa la mlinzi wa kati katika mechi zake za mwisho za ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita.
Mbali na kusajili beki, Kaburu alisema pia kuwa, wamepanga kumnasa mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa kutoka nje ili kuziba mapengo ya Mbwana Samatta na Emmanuel Okwi.

Simba yakata rufani nyingine


UONGOZI wa klabu ya Simba umesema utakata rufani nyingine kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kupinga kupambanishwa na Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya klabu bingwa Afrika.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha michezo cha Radio One.
Rage alisema, wameamua kuwasilisha rufani hiyo CAF kwa vile baadhi ya vifungu vya kanuni za mashindano hayo, vinaonyesha kuwa walipaswa kuingizwa moja kwa moja kwenye hatua ya nane bora.
Kikosi cha Simba kikiwa na wachezaji 18 na viongozi kadhaa, kilitarajiwa kuondoka mjini Dar es Salaam jana usiku kwa ndege kwenda Misri kwa ajili ya mechi hiyo.
Simba na Wydad Casablanca zinatarajiwa kuteremka dimbani keshokutwa mjini Cairo katika mechi itakayoamua timu itakayofuzu kucheza hatua hiyo katika kundi B.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, kikanuni hawakupaswa kucheza na Wydad Casablanca katika mechi hiyo kwa vile Wamorocco hao walishatolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
"Hawa Wydad walishatolewa na TP Mazembe, na sisi tuliwakatia rufani TP Mazembe na kushinda, kwa hiyo tulitakiwa kucheza hatua hiyo. Nikifika tu Cairo, nitakwenda makao makuu ya CAF, tutacheza 'under protest' ili lengo letu lifanikiwe,"alisema kiongozi huyo.
Rage alisema safari yake ya kwenda makao makuu ya CAF itakuwa na lengo la kutaka kupata ufafanuazi ili kujua wanachopaswa kufanya iwapo kanuni zitakuwa zimekiukwa.
Akizungumzia mchezo wa keshokutwa, Rage alisema kikosi chao kipo fiti na kusisitiza kuwa, wamejipanga vyema kukabiliana na mbinu zote wanazoweza kufanyiwa na wapinzani wao ndani na nje ya uwanja.
Rage alisema wamewapa wachezaji wao mafunzo maalumu ya kisaikolojia ili kuhakikisha wanacheza mpira wa kiwango cha juu na kukwepa jazba.
Iwapo Simba itafanikiwa kuitoa Wydad Casablanca, itapangwa kundi B pamoja na timu za Al Ahly ya Misri, MC Algers ya Algeria na Esperance ya Tunisia.

Ni vita ya Rooney na Messi J'Mosi

Rooney

Messi


MIAMBA ya soka barani Ulaya, Manchester United ya England na Barcelona ya Hispania, inashuka dimbani keshokutwa katika mechi ya fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Mechi hiyo, itakayopigwa kwenye uwanja wa Wembley mjini London nchini Uingereza, inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kwa vile kila timu imepania kushinda ili kutwaa ubingwa.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu kwa Manchester na Barcelona kukutana katika fainali ya michuano hiyo. Zilikutana kwa mara ya mwisho mwaka 2009 mjini Rome, Italia ambapo Barcelona iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Barcelona na Manchester United zimewahi kukutana katika michuano hiyo mara 11, ambapo kila moja imeshinda mechi tatu. Timu hizo pia zimetwaa ubingwa wa Ulaya mara tatu kila moja.
Timu zote mbili zinashuka dimbani huku kila moja ikiwa imetwaa ubingwa wa ligi ya nchi yake. Manchester United imetwaa ubingwa wa ligi hiyo mara nne katika kipindi cha miaka mitano wakati Barcelona imetwaa ubingwa mara tano katika kipindi cha miaka saba.
Pamoja na timu zote kuundwa na wachezaji wengi nyota, macho ya mashabiki wengi wa soka duniani yanatarajiwa kuwa kwa wachezaji wawili, Wayne Rooney wa Manchester United na Lionel Messi wa Barcelona.
MESSI
Akizungumzia mechi hiyo hivi karibuni, Messi alisema ushindi wa taji hilo dhidi ya Manchester United ni muhimu kwake kuliko kufunga bao ndani ya ardhi ya Uingereza.
Messi alisema hawapaswi kuidharau Manchester United kwa kigezo cha kuifunga katika mechi yao ya mwisho mwaka juzi na kwamba ushindi keshokutwa ni muhimu kwake kuliko kuibuka mfungaji bora.
Katika msimu huu, Messi ameifungia Barcelona mabao 52, mabao 11 akiyafunga katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya. Anaweza kuweka rekodi ya kufunga mabao 12, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Ruud van Nistelrooy.
Messi alisema kwake, anaweka mbele zaidi ushindi wa Barcelona katika michuano hiyo kuliko rekodi yake binafsi. “Mabao yanakuwa muhimu pale tu mnaposhinda mechi,” alisema.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina anaamini kuwa, kikosi cha Manchester United, kinachofundishwa na Kocha Sir Alex Ferguson, kitakuwa tishio na amewaonya wachezaji wenzake wasiwadharau wapinzani wao.
“Nawaheshimu sana, ni timu nzuri na wanaye kocha mwenye rekodi nzuri na wachezaji wake ni tishio. Kukaa kwenye klabu miaka mingi na kushinda mataji mengi ni heshima kubwa,”alisema.
Messi alizaliwa Juni 24, 1987 katika mji wa Rosario nchini Argentina. Ni mchezaji anayevaa jezi namba 10 katika klabu yake ya Barcelona, aliyojiunga nayo mwaka 2005, akitokea kikosi cha pili cha klabu hiyo.
Aliitwa kwenye timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 20 ya Argentina mwaka 2005 na baadaye timu ya vijana wa chini ya miaka 23. Aliichezea timu ya taifa ya wakubwa kwa mara ya kwanza mwaka 2005. Ameichezea timu hiyo mechi 55.
ROONEY
Rooney alitoa mpya mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kushangilia ushindi wa Manchester United katika ligi kuu ya England kwa kuchora namba 19 kifuani kwake.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Everton, alionyesha mchoro huo mara baada ya Manchester United kutoka sare ya bao 1-1 na Blackburn Rovers na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya 19.
Rooney ndiye aliyeifungia Manchester United bao hilo la pekee. Mara baada ya mchezo huo, aliituma picha aliyopiga kwenye vyumba vya wachezaji, ikionyesha mchoro huo, kwenye mtandao wa Twitter. Hiyo ilikuwa zawadi aliyowapa mashabiki wa klabu hiyo.
Ushindi wa Manchester United uliiwezesha kuipiku rekodi ya Liverpool, iliyotwaa ubingwa wa England mara 18.
“Hakuna aliyetarajia Rooney angeituma picha hiyo kwenye mtandao wa Twitter. Alikuwa kama kichaa kuliko tulivyofikiri,”alisema mshambuliaji mwenzake, Michael Owen.
Rooney anaamini kuwa, zawadi pekee iliyobaki kwa mashabiki wa Manchester United ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya nne.
Mshambuliaji huyo ghali nchini England kwa sasa, alizaliwa Oktoba 24, 1985. Alicheza michuano ya fainali za Ulaya kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na kufunga mabao manne.
Aliitwa kwenye kikosi cha England kwa mara ya kwanza mwaka 2003. Aliichezea timu hiyo katika fainali mbili za Kombe la Dunia mwaka 2006 na 2010.
Alishinda tuzo ya mwanasoka bora wa England mara mbili mwaka 2008 na 2009. Hadi ilipofika Machi mwaka huu, aliweka rekodi ya kucheza mechi 79 za kimataifa na kufunga mabao 26.
Rooney alijiunga na Manchester United msimu wa 2004-05, akiwa na umri wa miaka 18, akitokea Everton. Usajili wake uliigharimu Manchester United kitita cha pauni milioni 25.6 za Uingereza.
Mara baada ya kujiunga na Manchester United, alikabidhiwa jezi namba nane, lakini baadaye alipewa jezi namba 10, iliyokuwa ikitumiwa na Ruud van Nistelrooy.

WACHEZA FILAMU WA KIKE WANAONG'ARA BONGO

KWA kipindi kirefu sasa, fani ya filamu imekuwa ikijipatia umaarufu mkubwa hapa nchini, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wasanii wake kujizolea sifa lukuki na pesa nyingi kutokana na umahiri wao katika uigizaji. Wafuatao ni waigizaji 10 wa kike wa filamu, ambao wamejizolea sifa na umaarufu mkubwa hapa nchini.

ZAMDA SALIM
Ni mshiriki mpya katika fani ya uigizaji filamu, lakini umakini na mvuto wake ni miongoni mwa mambo yaliyomwezesha kupata sifa na umaarufu mkubwa. Ameshiriki kucheza filamu nyingi na ambazo zilitingisha anga la Bongo kama vile Unfortunate Love, Born Again, Hot Friday na Pigo, ambayo aliicheza vizuri zaidi.

WEMA SEPETU

Alikuwa mrembo wa Tanzania mwaka 2006. Aliingizwa kwenye fani ya uigizaji filamu na mpenzi wake wa zamani, Steven Kanumba. Licha ya kukumbwa na kashfa nyingi, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani mara kwa mara, Wema ni mmoja wa waigizaji nyota na wenye mvuto nchini. Baadhi ya filamu alizoshiriki kuzicheza na kujipatia sifa ni pamoja na A Point of no Return, Fake Pastor, White Maria na My Diary, ambayo ameicheza kwa kushirikiana na Jackline Wolper na Rose Ndauka kupitia kampuni yao ya Jerowe.
WASTARA JUMA

Mwanadada huyu ni mmoja wa wacheza filamu wanaochupikia hapa Bongo, akiwa maarufu zaidi kwa jina la Stara. Mbali na kucheza filamu, fani nyingine ya Stara ni uandishi wa habari. Alianza kujijengea jina alipocheza filamu ya 2 Brothers na baadaye Mboni Yangu. Filamu zingine, ambazo hata yeye mwenyewe anazikubali ni Vita Mkomanae na Vivian.RIYAMA ALLY

Jina lake si geni katika fani ya filamu hapa nchini. Alianza kuonyesha makali yake katika tamthilia ya Fungu la Kukosa, iliyokuwa ikirushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV. Ameshiriki kucheza filamu nyingi, lakini zilizompatia sifa na umaarufu ni kama vile Mwasu, Alfa na Omega na Second Wife. Ni mwanadada mwenye sura na umbo lenye mvuto.NDUMBAGWE MISAYO

Anajulikana zaidi kwa jina la Thea. Ni msanii, ambaye kwa sasa huwezi kuacha kumzungumzia ama kumkosa katika fani ya filamu. Alianza kujulikana akiwa katika kundi la Sanaa la Kaole. Ameshiriki kucheza filamu nyingi kama vile Segito na Suspense. Moja ya sifa zake ni mvuto na kuuvaa uhusika wa nafasi anazocheza kiusahihi.YVONNE CHERRLY

Ni maarufu zaidi kwa jina la Monalisa. Ni mmoja wa wacheza filamu wakongwe hapa nchini, akiwa ameanzia katika kundi la Mambo Hayo, lililokuwa likionyesha tamthili zake kupitia kituo cha televisheni cha ITV. Amewahi kushiriki kwenye filamu nyingi kama vile behind the Scene, Binti Nusa. Filamu yake ya kwanza ni Girlfriend. Kwa sasa ni mtunzi na mtayarishaji wa filamu.
JACKLINE WOLPER

Ni mwanadada mwenye sura yenye mvuto. Ni msanii wa kike aliyeshiriki kucheza filamu nyingi, lakini zilizomwezesha kumjengea sifa na umaarufu ni Surprise na Secretary. Pia ameshiriki kuandaa filamu mpya ya My Diary akishirikiana na Rose Ndauka na Wema Sepetu.


IRENE UWOYA

Kama ni sura tu na umbo, mwanadada huyu, ambaye ni mke wa mwanasoka mmoja maarufu wa Burundi anatisha. Ni mwigizaji aliyedhihirisha kwa vitendo kwamba hapendi mchezo. Baadhi ya filamu alizoshiriki kucheza na kujipatia umaarufu ni pamoja na Mid Night na My Dreams. Irene, ambaye naye hana jina la utani, pia amewahi kutayarisha filamu ya Oprah on Sunday, ambayo imezidi kumng’arisha.
ELIZABETH MICHAEL

Ni maarufu zaidi kwa jina la Lulu. Ni binti anayejaribu kwa kasi kubwa kutishia nafasi za wakongwe katika fani hiyo. Alianza kujihusisha na uigizaji katika kundi la sanaa la Kaole kabla ya kujitosa rasmi kwenye fani ya filamu. Ameweza kufanya vizuri katika filamu nyingi kama vile Family Tears na Reason to die. Ni binti mwenye sura na umbo lenye mvuto.
AUNTY EZEKIEL

Ni mmoja wa wacheza filamu nyota wa kike hapa nchini, akiwa ameshiriki kucheza filamu nyingi na zilizotingisha anga la Bongo kama vile Young Billionaire, Mask na Hard Love Moro, ambayo aliitayarisha. Pia ni mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Filamu ya Jawero, akishirikiana na Rose Ndauka na Jackline Wolper. Kwa pamoja wametoa filamu mpya inayoitwa My Diary.
ROSE NDAUKA

Msanii huyu ameshiriki kucheza filamu nyingi. Filamu ya kwanza kumtambulisha katika ulimwengu huo hapa nchini ni Swahiba. Mbali ya kucheza filamu, Rose ambaye hana jina la utani, kwa sasa ni mtunzi na mtayarishaji wa fani hiyo. Pia ni mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Filamu ya Jawero, akishirikiana na Jackline Wolper na Wema Sepetu. Hivi karibuni walishirikiana kuandaa filamu ya My Diary.

Simba ni kufa au kupona


Inapambana na Wydad Casablanca keshokutwa
Rage atamba jeshi lake limekamilika kila idara


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Simba keshokutwa wanatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya raundi ya tatu itakayochezwa mjini Cairo, Misri.
Simba imerejeshwa katika michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kushinda rufani yake dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara, waliilalamikia TP Mazembe kwa kumchezesha mchezaji Janvier Besala Bokungu katika mechi ya awali kati yao kinyume cha kanuni za usajili.
Simba ilidai kuwa, Bokungu hakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa vile bado alikuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia. Simba ilitolewa katika michuano hiyo na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3.
Mshindi wa pambano hilo, atacheza hatua ya makundi ya ligi hiyo katika kundi B. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Al Ahly ya Misri, EST ya Tunisia na Moloudia Club ya Algeria.
Iwapo Simba itatolewa na Wydad Casablanca, italazimika kucheza hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kupambana na DC Motema Pembe ya Congo. Mechi kati ya timu hizo zimepangwa kuchezwa mwezi ujao.
Akihojiwa katika kipindi cha michezo cha Radio One jana, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema Simba ilitarajiwa kuondoka jana usiku kwa ndege kwenda Misri kwa ajili ya mechi hiyo, ikiwa na kikosi cha wachezaji 18 na viongozi kadhaa.
Kwa mujibu wa Rage, wameshafanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mechi hiyo, ikiwa ni pamoja na kupata ushirikiano kutoka ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Misri, ambayo imeiandalia hoteli ya kukaa pamoja na usafiri wa ndani.
Rage alisema Simba itakwenda Misri ikiwa na mashabiki wapatao 1,000 kutoka Tanzania. Alisema wanatarajia kupata mashabiki wengine huko huko Misri, ambako baadhi ya watanzania wanasoma katika vyuo mbalimbali.
Pamoja na kutambia maandalizi waliyoyafanya, Simba itawakosa wachezaji wake Mbwana Samatta na Patrick Ochan, ambao wameuzwa kwa klabu ya TP Mazembe kwa jumla ya kitita cha sh. milioni 300.
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilieleza juzi kuwa, CAF imewazuia wachezaji hao kucheza mechi hiyo kwa vile wameshauzwa hivyo kukosa uhalali wa kuichezea Simba.
Simba kupitia TFF ilitaka kufahamu kutoka CAF iwapo inaweza kuwatumia wachezaji hao kwa vile hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ya kuichezea TP Mazembe bado haijatolewa.
Kwa mujibu wa CAF, wachezaji hao wawili hawawezi kuichezea Simba kwa vile tayari wameshauzwa, hivyo hawana sifa ya kuwa wachezaji wa timu hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 26 (1) ya kanuni za ligi ya mabingwa Afrika.
Pamoja na kanuni kuwazuia wachezaji hao kuichezea Simba, Rage amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wao na wanakwenda Misri wakiwa na tahadhari kubwa.
Rage alisema pia kuwa, hawana wasiwasi wa mechi hiyo kuchezeshwa na waamuzi kutoka Misri kwa sababu kama timu inao uwezo wa kucheza soka, hawawezi kufanya lolote kuihujumu.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema wanafahamu vyema mbinu, ambazo hufanywa na timu za nchi za ukanda wa kaskazini wakati wa michuano hiyo, hivyo wamejiandaa vyema kukabiliana nazo.
“Hata hao Wamirsi wanafahamu vyema kwamba timu inayokwenda kwao ni tishio barani Afrika, hivyo tunakwenda huko tukiwa tumejiandaa kwa vita,”alisema.
Kocha mpya wa Simba, Moses Basena kutoka Uganda, aliyechukua nafasi ya Patrick Phiri wa Zambia, alisema juzi kuwa, amewaandaa vyema wachezaji wake kisaikolojia na pia kwa mbinu za kukabiliana na wapinzani wao.
Alizitaja baadhi ya mbinu, ambazo amewaelekeza wachezaji wake kuzitumia kuwa ni kuepuka jazba iwapo watabaini mwamuzi anawabeba wapinzani wao ili kukwepa kuonyeshwa kadi nyingi za njano na nyekundu.
“Tunafahamu wazi kwamba Wydad Casablanca ni timu nzuri, lakini hata Simba nayo ni timu nzuri, hivyo mwamuzi wa mwisho ni dakika 90 za uwanjani,”alisema kocha huyo na kusisitiza kuwa, jeshi lake limekamilika katika kila idara.
Alipoulizwa kwa nini kikosi chake hakijacheza mechi za kirafiki kwa ajili ya kujipima nguvu, Basena alisema hofu yake kubwa ilikuwa wachezaji kuumia, hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa timu imebakiwa na wachezaji wachache.
Iwapo timu hizo zitamaliza dakika 90 zikiwa sare, mshindi itabidi apatikane kwa njia ya kupigiana penalti tano tano.
Baadhi ya wachezaji wa Simba wanaotarajiwa kuwemo kwenye safari hiyo ni Emmanuel Okwi, Uhuru Selemani, Rashid Gumbo, Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Juma Nyoso, Shija Mkina, Juma Jabu, Nico Nyagawa, Jerry Santo, Abdulrahim Humud, Salum Gila, Mohamed Banka, Salum Aziz na Juma Kaseja.
Swali kubwa wanalojiuliza mashabiki wa soka nchini ni iwapo Simba itaweza kuimudu Wydad Casablanca bila kuwa na mazoezi ya muda mrefu wakati wapinzani wao hao bado wanashiriki katika michuano ya ligi ya Morocco.
Wydad ni timu yenye mafanikio makubwa nchini Morocco, ikiwa imetwaa ubingwa wa nchi hiyo mara 12, sawa na FAR Rabat. Wydad pia imeshika nafasi ya pili mara tisa wakati FAR wameshika nafasi hiyo mara sita.Raja Casablanca, ambayo ni maarufu zaidi nchini kutokana na kupambana na Yanga mwaka 1998, ni ya tatu kwa kuchukua ubingwa wa Morocco mara sita.
Wydad pia imeweka rekodi ya kushinda Kombe la Morocco mara tisa wakati FAR Rabat imelinyakua mara 11. Raja Casablanca ni ya tatu kwa kulitwaa mara sita.
Katika historia yake, Wydad imetwaa ubingwa wa Afrika mara moja mwaka 1992. Mwaka 2002 walitwaa Kombe la Washindi la Afrika na mwaka 1994 walitwaa ubingwa wa nchi za Afrika zenye asili ya kiarabu.
Kikosi cha Wydad kimesheheni nyota wengi wanaocheza katika ligi hiyo na kutoka nje ya nchi. Mmoja wa washambuliaji hao nyota kutoka nje ni Luiz Jeferson Escher kutoka Brazil, ambaye alinunuliwa msimu huu kutoka Kawkab Marrakech ya huko huko Morocco.
Nyota wengine, ambao timu hiyo inajivunia ni pamoja na Jean Louis Paschal Angan na Fabrice N’Guessi, ambaye ni raia kutoka Congo. Angan ni mchezaji wa kimataifa wa Benin. Kwa wachezaji wa nyumbani, Wydad inajivunia nyota wake, Youness Mankari. Kocha Mkuu wa timu hiyo ni Fakhreddine Rahji.

AT awapiga madongo Offside TrickBAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii Ally Ramadhani, maarufu kwa jina la AT ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Vifuu Tundu’.
AT amerekodi kibao hicho kwa kutumia swaga za mduara na inasemekana ameamua kuwapiga dongo wasanii wenzake wa kundi la Offside Trick lenye maskani yake Zanzibar.
Akizungumza mjini hapa mwanzoni mwa wiki hii, AT alisema ameamua kuwapiga madongo wasanii wa kundi hilo kwa lengo la kulipiza kisasi.
Alidai kuwa, kundi hilo hivi karibuni lilirekodi kibao cha ‘Kidudu mtu’ kwa lengo la kumkashifu yeye hivyo naye ameamua kulipiza kisasi.
“Nimeamua kuwaonyesha kuwa mimi ni mkali wa kutunga mashairi ya kupiga madongo kuliko wao, nadhani hili litakuwa fundisho kwa ‘wajinga’ wengine wanaopenda kutumia majina ya watu kutafuta umaarufu,” alisema AT.
Msanii huyo mwenye maskani yake Zenj alianza kupata umaarufu kimuziki alipoibuka na kibao chake cha ‘Nipigie’, alichomshirikisha mkongwe Stara Thomas.
AT pia aling’ara katika kibao cha ‘Mama ntilie’ kilichotungwa na Gelly, aliyemshirikisha pia mwanadada Rehema Chalamika ‘Ray C’.

Mzee Yusuph acha maringo-Mashabiki

BAADHI ya mashabiki wa muziki wa taarab wa Jiji la Dar es Salaam, wamemlalamikia kiongozi wa kundi la Jahazi, Mzee Yusuph kwa madai kuwa amezidisha maringo wakati wa maonyesho ya kundi lake.
Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti kwenye kumbi mbalimbali za starehe, mashabiki hao wamedai kuwa, Mzee amekuwa na tabia ya kuchelewa kufika ukumbini.
Mbali na kuchelewa kufika ukumbini, mashabiki hao wamedai kuwa, kiongozi huyo wa kundi la Jahazi amekuwa na kawaida ya kuimba nyimbo chache anapofika ukumbini na kisha kutoweka.
Katika onyesho moja la kundi hilo, lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam, mwandishi wa habari hizi alimshuhudia kiongozi huyo wa Jahazi akifika ukumbini saa saba usiku wakati wenzake wakiwa wameshaanza onyesho.
Licha ya kufika ukumbini akiwa amechelewa, Mzee aliimba nyimbo tatu na baadaye kutoweka, hali iliyolalamikiwa na mashabiki wengi waliodai kuwa, kiongozi huyo wa Jahazi ameanza kuwa na maringo.
“Hii haikuwa tabia ya kawaida kwa Mzee Yusuph. Siku hizi amebadili mno, sijui anachoringia ni kitu gani,” alilalamika shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Rehema Hassan, mkazi wa Magomeni.
Shabiki mwingine anayefahamika kwa jina la Hussein Makoroboi alisema, kwa staili hiyo, kundi la Jahazi litaanza kupoteza mashabiki kutokana na wasanii wake kuzidisha maringo.
Hivi karibuni, kundi hilo liliwasimamisha waimbaji wake wawili nyota, Leila Rashid na Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ kwa tuhuma za makosa ya utovu wa nidhamu.
Waimbaji hao walisimamishwa kwa madai ya kuchelewa kufika kwenye maonyesho, kujiona wao bora kuliko wenzao na pia kutohudhuria mazoezini mara kwa mara.
Juhudi za kumpata Mzee ili ajibu malalamiko ya mashabiki hao hazikuweza kufanikiwa kwa vile simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

Muumini bado aikumbuka Bwagamoyo Sound


MTUNZI na mwimbaji nyota wa muziki wa dansi nchini, Mwinjuma Muumini amesema yupo katika hatua za mwisho za maandalizi ya albamu ya bendi yake ya zamani ya Bwagamoyo Sound.
Muumin aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa juzi kuwa, amebakiza nyimbo mbili kabla ya kukamilisha albamu hiyo, itakayokuwa na nyimbo sita.
Mwimbaji huyo wa zamani wa bendi za Mchinga Sound na African Revolution alisema, albamu yake hiyo itajulikana kwa jina la ‘Nafsi haina urithi’.
Alivitaja vibao vingine vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Mwanamtiti Malunde’, ‘Cute Baby’, ‘Natafuta mume’, ‘Ufukara Jeraha’, ‘Udugu wa mashaka’.
Mwinjuma alisema amerekodi albamu hiyo kwa kuwashirikisha wanamuziki wa zamani wa bendi hiyo na kwamba hatarajii kufanya uzinduzi.
“Nitaiingiza albamu hii moja kwa moja sokoni, sitafanya uzinduzi kama ilivyo kwa bendi zingine,”alisema mwimbaji huyo, ambaye kwa sasa yupo bendi ya Twanga Pepeta International.
Aliwataja baadhi ya wanamuziki alioshirikiana nao kurekodi albamu hiyo kuwa ni Geoge Gama, Yahya Mkango, Venas Joseph, Wera Baba, Karama Legesu na marehemu Mwamvita Ramadhani.
Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kuivunja Bwagamoyo Sound na kujiunga na Twanga Pepeta, mwanamuziki huyo alisema, umetokana na kutafuta maslahi zaidi.
Alikiri kuwa, bendi yake hiyo ilishindwa kukamata soko la muziki nchini kutokana na kuwepo kwa bendi nyingi na kusisitiza kuwa, kwa sasa ameamua kuweka maskani ya kudumu Twanga Pepeta.
Kwa mujibu wa Mwinjuma, tayari ameshatunga kibao kimoja kinachokwenda kwa jina la ‘Penzi la shemeji’, ambacho kitakuwa cha kumi na moja kwenye albamu mpya ya bendi hiyo.
Alisema anachokifanya kwa sasa ni kusoma muziki wa bendi hiyo na kujipanga upya kwa sababu imepita miaka mingi tangu alipokuwa akipigia bendi ya African Revolution.
“Nimepania kurudisha heshima yangu kimuziki, iliyopotea baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu bila kusikika kwa mashabiki,”alisema.
Ameushukuru uongozi wa bendi hiyo pamoja na wanamuziki wenzake kwa kumpa mapokezi mazuri na kuongeza kuwa, atahakikisha anatimiza malengo waliyojiwekea.

Wednesday, May 25, 2011

K-One atambulisha moja mpya

MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Karim Othman amedhihirisha kuwa ni moto wa kuotea mbali baada ya kuanza kung’ara katika kibao chake kipya cha Yule.
Karim, maarufu zaidi kwa jina la K-One, amerekodi kibao hicho kwa kushirikiana na msanii nyota wa kike wa muziki huo, Maunda Zorro.
Kibao cha Yule, ambacho kimepigwa katika miondoko ya zouk, kimeshaanza kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni pamoja na kupigwa kwenye vituo vya radio nchini.
K-One amerekodi kibao hicho katika studio za Baucha zilizopo Magomeni, Dar es Salaam wakati picha za video zimepigwa na kampuni ya 01 Video chini ya Dk. Tonee.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, K-One alisema ameamua kutoa kibao hicho kwa ajili ya maandalizi ya ujio wa albamu yake ya kwanza.
“Huu ni utambulisho wangu tu kwa mashabiki kabla ya kuzindua albamu yangu ya kwanza,”alisema msanii huyo, ambaye pia hushiriki kuonyesha mavazi.
K-One alisema baada ya kibao cha ‘Yule’, anatarajia kukitambulisha kibao chake cha pili kinachojulikana kwa jina la ‘Ngoja niseme’, alichokirekodi kwa kushirikiana na msanii mkongwe, Chege Chigunda.
Msanii huyo machachari alisema, anatarajia kuzindua albamu yake ya kwanza mwezi ujao, ikiwa na vibao vinane, alivyovirekodi kwa kushirikiana na wasanii mbalimbali wakongwe.
Mbali na ‘Yule’ na ‘Ngoja niseme’, alivitaja vibao vyake vingine, vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Dhahabu’ alichomshirikisha Ali Kiba na ‘Niwaambie’ alichorekodi na Madee.
Vibao vingine ni ‘Muelewe’ alichomshirikisha Tundaman, ‘Bora’ alichorekodi na Top C, ‘Weekend Special’ alichomshirikisha Baker na ‘Sina hakika’ alichorekodi peke yake.
“Namshukuru Mungu kwamba kibao changu cha kwanza hadi sasa kimepokewa vizuri, nasubiri kuona mambo yatakuwaje katika kibao changu cha pili na baada ya hapo ndipo nitafanya uzinduzi wa albamu yangu,”alisema.
Kwa mujibu wa K-One, iwapo mashabiki watampokea vizuri kwenye gamu, uzinduzi wa albamu hiyo utafanyika mapema mwezi ujao.
Amemshukuru Mkurugenzi wa Studio za Baucha Records, Ally Baucha kwa kukubali atumie nembo yake.

Monday, May 23, 2011

Utata wagubika kifo cha Wanjiru

Mama yake Wanjiru na mkewe

Maiti ya Wanjiru ikiingizwa kwenye gari la wagonjwa


Wanjiru, sehemu ya nyumba yake na mkewe


Samuel Wanjiru enzi zake


Ni milionea aliyejua viatu akiwa na miaka 14
Wanawake wamfanya afe na umri wa miaka 24
Ni bingwa wa dunia wa mbio ndefu za Beijing
Alivunja rekodi ya dunia ya miaka 44
Utata wa kifo chake wazidi kutanda


SAMUEL Kamau Wanjiru, milionea wa Kenya aliyeupata utajiri akiwa na umri wa miaka 20, ambapo utajiri wake umeelezwa kuchangia kifo chake akiwa na umri mdogo wa miaka 24.

Wanjiru aliyezaliwa Jumatatu, akaoa Jumatano na akafariki dunia Jumapili, historia ya mafanikio yake inatokana na kocha wa riadha wa Japan, Sunish Kubayash aliyemuona kwenye mashindano ya riadha ya shule za msingi yaliyofanyika Kisumu, Kenya, mwaka 1999.

Mauti yalimkuta akiwa nyumbani kwake na hawara, muhudumu wa baa ya jirani na nyumbani kwake iliyo umbali wa karibu kilometa moja.

Hata hivyo mazingira ya kifo chake bado ni utata, lakini hawara aliyekuwa naye hadi mwisho wa maisha yake, Jane Nduta katika maelezo yake anaamini Wanjiru hakujiua kwa kujirusha toka ghorofani.

Mama mzazi wa Wanjiru, Hanna Wanjiru kwa upande wake anaamini mwanawe ameuawa kwa makusudi, na anamtuhumu mke wa marehemu Teresia Njeri, kwamba anahusika na mauaji hayo.

Hanna anadai kulikuwa na alama za damu kwenye chumba cha mapumziko na pia damu zingine zilionekana kwenye chumba cha kulala kilichopo ghorofani.

Wanjiru amekufa akiwa na mgogoro na mkewe Teresia na aliwahi kumtumia ujumbe wa kwenye simu kumtishia kumuua, kiasi cha Teresia kuamua kufungua kesi mahakamani kulalamikia vitisho vya mumewe vya kutaka kumuua. Pia mlinzi wake wa nyumbani aliwahi kufungua kesi kumlalamikia bosi wake aliyetishia kumuua, lakini wote Teresia na mlinzi waliondoa kesi zao mahakamani.

Mwanamke mwingine anayedai ni mke wa pili wa Wanjiru ni Judy Wambui (25), aliyezaa naye mtoto wa kike, pia alisema ana ujauzito wa miezi mitano wa Wanjiru na kwamba taratibu zote za kufunga ndoa zilikuwa kwenye hatua za mwisho, na ndoa hiyo ilikuwa ifungwe kiserikali, baada ya ndoa ya kwanza na Teresia iliyofungwa kanisani.

Siku ya kifo chake, Wanjiru aliyekuwa kwenye kambi ya mazoezi katika mkoa wa Eldoret, aliondoka huko Jumapili saa tatu asubuhi akieleza anakwenda Nyahururu kutatua matatizo ya kifamilia.

Kocha wake alisema Wanjiru aliomba ruhusa kwenda Nyahururu kwa ajili ya kuonana na wakili wake kuhusiana na kesi inayomkabili ya kumiliki bunduki ya AK47 bila kibali, kesi hiyo ilipangiwa kuendelea mahakamani Jumatatu ya Mei 23.

Saa saba nchana ya siku hiyo ya Jumapili, Wanjiru aliwasili Nyahururu ambapo alikwenda kwenye mgahawa wa Jimrock ambako alikutana na mtu aliyefahamika kwa jina la George wa benki ya Barclays, aliyekuwa na ahadi naye.

Taarifa zilisema saa 4 usiku Wanjiru aliwasili kwenye mgahawa wa Water Falls ambako alikula na kupata kinywaji, kilichoelezwa kilikuwa ni kilevi hadi saa 5 usiku alipoondoka na kwenda kwenye baa ya Kawa Falls alipokutana na muhudumu Jane Nduta aliyelezwa kuwa hawara yake.

Jane akielezea mkasa mzima wa hadi kifo cha Wanjiru, alisema mwanariadha huyo alikwenda kwenye baa anayofanyakazi saa tano usiku akiwa tayari amelewa pombe, na kwamba yeye na Wanjiru ni marafiki wa siku nyingine, ambapo mwanaridha huyo mara kadhaa amekuwa akienda nyumbani kwa Jane.

Alisema ilikuwa mara yake kwanza kwenda nyumani kwa Wanjiru na alikubali baada ya kuthibitishiwa kwamba mkewe hayupo, ambapo kabla ya kwenda nyumbani, walienda kwenye mgahawa wa Jimrock ambako Wanjiru aliongeza kunywa pombe.

Jane alisema walipofika nyumbani, Wanjiru alitoka ndani ya gari na kuzungumza na mlinzi na baadaye alirejea kwenya gari, na waliingia ndani ya eno la nyumba ambapo walishuka kwenya gari na kwenda kukaa kwenye chumba cha mapumziko wakiangalia televisheni, wakati huo ilikuwa mida ya saa sita usiku.

Alisema baada ya dakika zipatazo tano ghafla aliingia mke wa Wanjiru, na alianza kumtolea maneno makali mumewe akimuhoji kuhusu yeye (Jane) akitaka kujua ni nani.

“Aliniuliza uhusiano wangu na mumewe, nikamjibu ni rafiki yangu wa karibu na tumekuwa marafiki kwa muda mrefu, nilimwambia kama si urafiki wetu nisingekuja nyumbani kwake,” alisema Jane.

Alisema Teresia aliondoka kwenye eneo hilo ambapo baada ya muda mfupi alirejea tena na kuendeleza mzozo, ambapo aliondoka tena kwa mara ya pili, ambapo aliporudi tena kwa mara ya tatu wao walikuwa wamekwisha ingia chumbani wakiwa wamekaa kitandani.

Jane alisema Teresia aliendeleza mzozo na kuchukua jagi la maji na kutishia kumpiga nalo (Jane), ambapo alijitetea kwa kumdaka mkono, wakati huo Wanjiru alikuwa kitandani kazidiwa na ulevi kiasi cha kushindwa hata kujitetea.

Kwa mujibu wa Jane, Teresia alianza kuruhsiana maneno na Wanjiru, ambapo aliamua kuchukua funguo za mlango unaoelekea kwenye ngazi za kushuka chini na kuwafungia chumbani.

Jane alisema alifungua mlango wa kwenye veranda ya chumbani iliyopo ghorofani na kuanza kumbembeleza mkewe aliyekuwa tayari chini, arudi kuwafungulia mlango. Wakati huo yeye (Jane) alikuwa bado amekaa kitandani.

Alisema ghafla alimsikia mlinzi akipiga kelele na alikwenda kwenye veranda kuangalia kulikoni, na alipomuuliza mlinzi kilichotokea, mlinzi huyo alimuonyesha kwenye sakafu ambapo alimuona Wanjiru kalala sakafuni huku akivuja damu kichwani.

Jane kwa maelezo yake haamini kama Wanjiru alijiua, anamini ni ajali iliyomkuta kwakuwa muda wote alikuwa mwenye furaha, na hakuonekana kusongwa na mawazo.

Bingwa huyo wa mbio ndefu duniani (ambaye sasa ni marehemu) alianza kuwa maarufu alipokuwa na umri wa miaka 18, ambapo katika umri huo alimuoa Teresia Njeri, aliyefanikiwa kuzaa naye watoto wawili Anne Wanjiru mwenye umri wa miaka mine na Simon Njoroge mwenye umri wa miaka miwili.

Wanjiru alimvutia Kubayash baada ya kushinda mashindano ya riadha ya shule za msingi, akikimbia akiwa hana viatu, pekupeku, ambapo alimdhamini kwenda kusoma shule ya riadha nchini Japan kwa kipindi cha miaka miwili.

Mwanariadha huyo aliyezaliwa Novemba 10, 1986 katika mji wa Nyahururu, hakuona aibu kuelezea maisha yake duni ya utotoni, ambapo aliwahi kuhojiwa na gazeti moja na kueleza kuwa katika maisha yake alianza kuvaa viatu akiwa na umri wa miaka14, na viatu vyenyewe vilikuwa ni makobazi ya plastiki.

Alisema wazazi wake walitengana akiwa na umri wa miaka mitano, na tangu wakati huo amekuwa akilelewa na mama yake akiwa mtoto kutoka kwenye familia duni iliyoshindwa hata kumnunulia viatu.

Wanjiru anasema alipomaliza shule ya msingi mwaka 2000, wakati huo akisoma shule ya msingi ya Githunguri, Olkalau, mwaka 2002 alikwenda Japan na kujiunga na shule ya riadha ya Sendai Ikuei Gakuen iliyopo Sendai.

Alimaliza shule hiyo mwaka 2005 ambapo alijiunga na timu ya riadha ya Toyota Kyushu, ambapo aliazna kuvuna mamilioni ya fedha baada ya kushinda mara tano. Ushindi uliomfanya kuwa milionea ni baada ya kuvunja rekodi katika mashindano ya Olimpiki ya Beijing, China, iliyowekwa na mwanaridha wa Ureno, miaka 44 iliyopita.

Hadi kifo chake ana hisa katika baadhi ya kampuni nchini Japan na anamiliki magari ya kifahari, Range Rover na Toyota VX na ana mali zisizo hamishika katika miji ya Nairobi na Nakuru.

Baadhi ya marafiki zake walimuelezea Wanjiru kwamba ni mtu aliyekuwa haoni shida kugawa fedha kwa marafiki zake. Ambapo alisema alilazimika kuoa akiwa na umri wa miaka 18 ili awe na mtu wa kuangalia mali zake wakati yeye anapokuwa akiendelea na masuala ya riadha.

Thursday, May 19, 2011

Nembo ya Blog ya Tanzanianblogspotawards

Kutokana na maombi ya wengi ambayo tumeyapokea. Tumeongeza muda wa kupendekeza majina yatakaoshiriki katika mashindano yetu. Hivyo tarehe ya kutuma majina ya blog hizo umebadilishwa kutoka tarehe 31 May 2011 kwenda tarehe 10 June 2011.Pia sasa hivi tumeamua logo ya shindano hili ni hii hapa...Kuna nyingine tulitengeneza mwanzoni lakini hii ndio tumeichagua kwa sasa. Sasa kama ukipost habari za shindano hili tafadhali tumia picha hii.Pia kutokana na blog mbalimbali zimepost hili shindano letu na tumeona kuna maswali ambayo hayana majibu kwenye comments zao. Na sisi kwa vile hatutaweza kupitia kila blog iliyopost maelezo na kuwaelewesha watu. Hapa nitaweka majibu ya maswali baadhi nimeona yameandika najua kuna mengi lakini hatujaweza kuyaona. Ila kama una swali usisite kututumia.1. Kuna mtu amesema kuwa shindano letu haliwashirikishi watanzania wanaoishi nje ya nchi. Hiyo siyo kweli kabisa. 2. Shindano letu ni kwa blog zilizoandikwa kwa kiswahili tu. Hilo sio kweli pia3. Tunapendekeza wenyewe majina ya watu watakao shiriki katika shindano letu. Hio sio kweli kabisa. 4. Sio kila blog itakayowekwa kwenye Directory list yetu. Hilo sio kweli...Ukituletea blog yeyote iliyoandikwa na mtanzania mahali popote pale alipo ulimwenguni tutaiweka. Ili mradi hiyo blog inaweza kusomwa na mtu yeyote. Blogs ambazo hatuziweki huku ni zile ambazo waanzilishi wa blog hizo wamezifunga na wanahitaji msomaji wa blog hiyo awe mwanachama wa blog hiyo kabla hujaweza kusoma "members only blogs".


Wednesday, May 18, 2011

Simba, Casablanca kukipiga CairoPAMBANO la kutafuta timu itakayocheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa wa Afrika kati ya Simba na Wydad Casablanca ya Morocco litachezwa Mei 28 mwaka huu kwenye uwanja wa Petrosport mjini Cairo, Misri.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, iwapo timu hizo zitamaliza dakika 90 zikiwa sare, mshindi itabidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano.
Wambura alisema uamuzi huo umefikiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kuamuru timu hizo zicheze mechi ya mkondo mmoja kwenye uwanja huru.
Kwa mujibu wa ofisa huyo wa TFF, Chama cha Soka cha Misri (EFA) ndicho kilichopewa jukumu la kuzipokea timu za Simba na Wydad Casablanca zitakapowasili mjini Cairo.
Aliongeza kuwa, kila timu imetakiwa kujigharamia usafiri wa kwenda Cairo na kurudi pamoja na gharama za malazi. Alisema gharama zingine zozote zitakazojitokeza, zitabebwa na timu hizo kupitia vyama vyao vya soka.
Wambura alisema pia kuwa gharama za waamuzi wa mchezo huo pamoja na kamishna, zikiwemo usafiri wa ndani na malazi, nazo zitabebwa na timu hizo kupitia vyama vyao vya soka.
“Mapato yatakayopatikana kutokana na viingilio vya mechi hiyo, yatagawiwa nusu kwa nusu kwa timu zote mbili kupitia vyama vyao vya soka,”alisema Wambura.
Simba imerejeshwa katika michuano hiyo, baada ya kushinda rufani yao waliyokata kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Timu hiyo ya Tanzania ilikata rufani CAF ikipinga TP Mazembe kumchezesha mchezaji Janvier Besala Bokungu katika mechi ya awali ya raundi ya pili kati yao kinyume cha kanuni za usajili.
Simba ilidai kuwa, Bokungu hakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa vile bado alikuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia. Simba ilitolewa katika michuano hiyo na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3.
Kwa mujibu wa ratiba, mshindi wa mechi hiyo atacheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa wa Afrika katika kundi B. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia na Moloudia Club ya Algeria.
Iwapo Simba itapoteza mechi hiyo, itaangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho na kucheza hatua ya mtoano dhidi ya DC Motema Pembe ya Congo.

Asamoah aitesa YangaAtaka alipwe mil 19.5/-

Niyonzima amwaga wino

Yamtosa ‘pro’ kutoka Uganda


KAMATI ya Usajili ya klabu ya Yanga, inahaha kusaka dola 13,000 za Marekani (sh. milioni 19.5) kwa ajili ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Kenneth Asamoah.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seif Ahmed alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Asamoah anataka alipwe kiasi hicho cha fedha ili akaziwasilishe kwa klabu yake ya zamani ya FK Jagodina ya Serbia.
Kwa mujibu wa Seif, FK Jagodina inataka ilipwe fedha hizo ili iweze kutoa uhamisho wa kimataifa wa mshambuliaji huyo, aliyejiunga na Yanga tangu mwaka jana.
Asamoah alisajiliwa na Yanga msimu uliopita, lakini alishindwa kuichezea katika michuano ya ligi na ya kimataifa, kufuatia timu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na FK Jagodina kuhusu malipo ya uhamisho wake.
Mshambuliaji huyo aliwasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na uongozi wa Yanga kuhusu usajili, lakini aliondoka patupu kutokana na kukosekana kwa kiasi hicho cha pesa.
Hata hivyo, Seif alisema wapo mbioni kutafuta kiasi hicho cha pesa ili waweze kukamilisha usajili wa mchezaji huyo haraka iwezekanavyo. Asamoah aliondoka nchini juzi kurejea Ghana. Katika hatua nyingine, kamati ya usajili ya Yanga jana ilitarajiwa kumsainisha mkataba mchezaji Haruna Niyonzima wa APR ya Rwanda mjini Kigali.
Seif alisema jana kuwa, usajili wa mchezaji huyo umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na kutoa masharti mazito kwa uongozi wa Yanga.
“Kwa sasa mambo yote yanakwenda vizuri, tumemtuma mjumbe wetu kule Rwanga na tunatarajia Niyonzima atatia saini mkataba wa kuichezea Yanga leo akiwa kwao Kigali,”alisema.
Hata hivyo, Seif hakuwa tayari kutaja kiwango cha pesa walichotumia kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Rwanda kwa madai kuwa, hiyo ni siri ya kamati yake.
Wakati Niyonzima alitarajiwa kumwaga wino jana, klabu hiyo imetangaza kufuta mpango wake wa kumsajili beki wa kimataifa wa Uganda, Godfrey Walusimbi.
Seif amesema wamefikia uamuzi huo kufuatia klabu hiyo kutimiza idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa mujibu wa kanuni za usajili za ligi kuu ya Tanzania Bara.
“Tulikutana na kushauriana na viongozi wa benchi la ufundi na pia kutazama mambo mbalimbali na hatimaye kukubaliana tumuache Walusimbi kwenye usajili wetu,”alisema.
Mbali na Niyonzima na Asamoah, wachezaji wengine wanaotarajiwa kusajiliwa na Yanga msimu ujao ni kipa Yaw Berko wa Ghana, Davies Mwape wa Zambia na Tony Ndolo wa Uganda.
Wachezaji walioachwa na Yanga katika msimu ujao ni pamoja na kiungo, Athumani Idi ‘Chuji’ aliyesajiliwa na Simba, Nelson Kimathi, Nsa Job, Job Ibrahim na Yahya Tumbo.

Mwaikimba apigwa 'stop'


UONGOZI wa timu ya soka ya Kagera Sugar umesema hauna taarifa yoyote kuhusu mshambuliaji wao, Gaudence Mwaikimba kutakiwa na timu ya Moro United.
Mbali na kutokuwa na taarifa hiyo, uongozi wa Kagera Sugar umesema haupo tayari kumuuza mshambuliaji huyo kwa vile bado wanamuhitaji katika msimu ujao wa ligi.
Kauli na msimamo huo ulitolewa juzi na mratibu wa timu hiyo, Mohamed Hussein alipozungumza na gazeti la Burudani kutoka mjini Bukoba.
Hussein alisema wamekuwa wakisikia taarifa za mchezaji huyo kusajiliwa na Moro United kupitia kwenye vyombo vya habari, lakini hawajawahi kufanya mazungumzo yoyote na uongozi wa timu hiyo.
"Mimi ninachojua ni kwamba, Mwaikimba ni mchezaji wa Kagera Sugar na bado tuna mkataba naye, hao Moro United hawajawahi kufika kwetu kwa ajili ya mazungumzo ya kumtaka mchezaji huyo,"alisisitiza mratibu huyo.
Akizungumzia maendeleo ya usajili wa timu yake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, Hussein alisema bado wanaendelea kuziba mapengo ya wachezaji walioachwa na waliouzwa.
Alisema lengo la timu yake ni kusajili wachezaji wengi wazalendo na kuongeza kuwa, wamepanga kufanya hivyo kupitia michuano ya Kombe la Taifa.
Mbali na kusajili wazalendo, Hussein alisema pia kuwa, wamefanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji kutoka nchi za Kenya, Uganda na Burundi kwa ajili ya usajili huo.

Kado atuliza mzuka Mtibwa


KIPA namba moja wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Shaaban Kado amesema, kwa sasa hana mpango wowote wa kuondoka katika timu hiyo.
Kado alisema kwa njia ya simu jana kutoka Morogoro kuwa, iwapo ataondoka Mtibwa Sugar, lengo lake litakuwa ni kwenda nje kucheza soka ya kulipwa.
Kipa huyo, ambaye pia yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 23, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kupewa ushauri na watu mbalimbali.
Kabla ya kufikia uamuzi, Kado alisema alikuwa amepata ofa za kujiunga na klabu za Simba na Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa.
"Nilipata ofa kibao, lakini nimepata ushauri wa kina kutoka kwa watu mbalimbali wanaonitakia mema, hivyo nimeamua kuendelea kuwepo ndani ya kikosi cha Mtibwa, ambako nina hakika ya ajira,"alisema mlinda mlango huyo.
Hata hivyo, Kado alisema bado anaendelea kufanya mawasiliano na baadhi ya mawakala wa wachezaji ili aweze kwenda kufanya majaribio nje ya nchi.
Aliongeza kuwa, lengo lake kubwa ni kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya Tanzania kwa lengo la kuinua zaidi kipaji chake na pia kuongeza mapato.

JABIR AZIZ: Mawazo yangu ni Ughaibuni tuMMOJA wa wanasoka waliojipatia umaarufu mkubwa nchini kutokana na umahiri wake wa kusakata kabumbu ni mshambuliaji Jabir Aziz wa Azam FC. Kabla ya kujiunga na Azam, Jabir alikuwa akichezea Simba, lakini hakuweza kupata mafanikio makubwa. Makala hii ya Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE inaelezea safari ya Jabir kisoka na matarajio yake ya baadaye.SWALI: Ulipokuwa ukichezea Simba, haukupata mafanikio makubwa kisoka kama ilivyo hivi sasa kwa Azam FC. Unaweza kueleza nini siri kubwa ya mafanikio yako?
JIBU: Kwa kweli sina jipya zaidi ya kujituma na kuhakikisha ninakuwa fiti ili niweze kumshawishi kocha kunipanga katika michezo zijazo.
Pamoja na hayo, huwa najisikia furaha kuona mchezaji mwenzangu wa Tanzania anapata maendeleo na hiyo inakuwa changamoto kwangu kuhakikisha najifua ili nami niweze kumfikia ama kumzidi.
SWALI: Nimesikia kupitia viongozi wako wa Azam kwamba umepata ofa ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa nchini Norway je, taarifa hizo ni za kweli?
JIBU: Ni kweli nimepata ofa hiyo, lakini viongozi wangu ndio wanaofahamu zaidi kwani kila kitu nimewaachia wao washughulikie.
Licha ya ofa hiyo, binafsi nimekuwa nawasiliana na baadhi ya mawakala wa soka ili waweze kunitafutia timu nje ya nchi. Lengo langu ni kuongeza kipato changu na pia kutumia ujuzi, ambao nitapata huko nje ya nchi kutoka kwa makocha ili niweze kuja kuinufaisha nchi yangu ya Tanzania.
Vilevile napenda nikiwa nje ya nchi, niitumie nafasi hiyo kuitangaza nchi yangu kwa kuvaa vitu mbalimbali, vikiwemo vinavyotangaza utalii wa Tanzania.
SWALI: Tukirudi nyuma, unazungumziaje kuhusu ushiriki wa Azam FC katika michuano ya ligi kuu msimu uliopita?
JIBU: Kufanya vibaya kwa Azam katika michuano ya ligi kuu ya msimu uliopita kumetupotezea malengo yetu mengi. Moja ya malengo hayo, tuliyokuwa tumejiwekea ni kutwaa ubingwa.
Zipo sababu nyingi zilizotufanya tushindwe kutwaa ubingwa. Miongoni mwa sababu hizo ni kikosi chetu kuwa na wachezaji wengi wapya, hivyo hakikuwa kimejiandaa vyema. Hali hiyo ilichangia kutufanya tupoteze mechi nyingi.
Nina hakika kasoro hiyo na nyinginezo hazitajitokeza tena msimu ujao. Nina hakika kikosi chetu kitakuwa moto wa kuotea mbali.
Nasema hivyo kwa sababu nimegundua kuwa, wachezaji wengi wanaosajiliwa na Azam wana vipaji vya hali ya juu vya kusakata kabumbu na kuipa matokeo mazuri. Kinachohitajika ni sisi wachezaji kuonyesha moyo wa kizalendo na kulipa fadhila kwa wamiliki wa klabu.
SWALI: Nini ushauri wako kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili michuano ya ligi kuu iwe ya kiwango cha hali ya juu?
JIBU: Binafsi nina mambo mawili makubwa ya msingi. La kwanza ni kuwaomba waamuzi wanaopangwa kuchezesha mechi za michuano hiyo, kuzingatia sheria zote 17 za soka badala ya kuchezesha kwa upendeleo.
Nimefanya uchunguzi wangu kwa muda mrefu na kugundua kwamba, baadhi ya waamuzi wanashindwa kuzitafsiri vyema sheria za soka na kutoa maamuzi, ambayo kidogo yanatatanisha.
Jambo la pili, nawaomba viongozi wa TFF na wale wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, ambao ndio wadhamini wakuu wa ligi hiyo, kuangalia suala la bima ya wachezaji.
Hili ni jambo la muhimu sana kutokana na wachezaji wengi kuumia na kukosa haki zao za msingi na wengine kupata ulemavu, hasa wale ambao wanachezea timu, ambazo hazina wadhamini.
Ni vyema TFF na Vodacom walitazame jambo hilo kwa umakini na ikiwezekana, iwapo wataongeza mkataba wa udhamini wa ligi hiyo miaka ijayo, suala hilo lipewe kipaumbele.
Napenda suala la bima lipewe nafasi katika mkataba mpya kati ya Vodacom na TFF ili wachezaji, ambao wanachezea timu zisizokuwa na wadhamini, waweze kupata malipo yao kila wanapoumia katika mechi za ligi badala ya kutelekezwa.

HUSSEIN MACHOZI: Mambo yangu sasa safi
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Rashid, maarufu kwa jina la Hussein Machozi, ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Mizimu.
Kibao hicho ni sehemu ya maandalizi ya ujio wa albamu ya tatu ya msanii huyo, baada ya kutesa katika albamu zake mbili za mwanzo za ‘Promise’ na ‘Kwa ajili yako’.
Akihojiwa katika kipindi cha Native Agenda cha televisheni ya TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Machozi alisema ameamua kuachia kibao hicho kwa lengo la kuwadhihirishia mashabiki kwamba bado yupo.
Machozi alisema ukimya wake wa muda mrefu uliwafanya mashabiki wengi wahoji mahali alipo na wengine kujenga hisia kamba ameishiwa kiusanii.
“Mimi bado nipo na nitaendelea kuwepo. Kuwa kimya kwa muda mrefu hakuna maana kwamba nimeishiwa. Yalikuwa maandalizi ya kuibuka na vitu vipya na mambo mapya,”alisema.
Katika kibao hicho, Machozi anasimulia kisa cha kijana msomi aliyeitwa kijijini na babu yake kwa lengo la kurithishwa mikoba ya uchawi, lakini akagoma kwa kile alichoeleza kuwa atapoteza hadhi na miaka mingi aliyosomea udaktari.
Hatimaye, baada ya kukataa kurithi mikoba hiyo, kijana huyo akaanza kutokewa na mauzauza mbalimbali, yaliyomfanya achanganyikiwe na kurukwa na akili.
Machozi, ambaye anafanyakazi zake chini ya lebo ya Respect ya Chifu Kiumbe, amewataka mashabiki wake wamvumilie kwa vile ukimya wake ulilenga kuwatayarishia vitu vya uhakika.
Msanii huyo, ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Singida alisema, anamshukuru Mungu kwamba hivi sasa maisha yanamuendea vizuri baada ya kuishi kwa dhiki kwa miaka kadhaa.
“Kwa kweli namshukuru sana Mungu kwani baada ya kuishi maisha ya dhiki, sasa naweza kuishi vizuri mimi na mama yangu, pesa ya kula na kununua hiki na kile hainipigi chenga,”alisema.
Machozi alikanusha madai kuwa, ametengana na promota wake wa zamani, Kid Boy, ambaye ndiye aliyemtoa kimuziki. Alisema hana tatizo lolote na Kid na kwamba bado wanaendelea kufanyakazi pamoja.
Alisema aliamua kuachana na Kid na kufanyakazi peke yake baada ya kujiona amekua na anastahili kujitegemea kwa kila kitu yeye mwenyewe.
“Nilitengana naye kwa sababu mtoto anapokua, anataka ajitegemee. Lakini hadi sasa bado namtegemea sana, anaendelea kunipa ushauri juu ya mambo mbalimbali. Naweza kusema hakuna mtu anayenifahamu vizuri zaidi ya Kid Boy,” alisema.
Machozi alisema kabla ya kujitosa katika fani ya muziki, alikuwa akicheza mpira na kiwango chake kilikuwa cha juu, lakini alilazimika kuachana na mchezo huo baada ya kuona hakuna maendeleo.
Alisema kutokuwepo kwa ufuatiliaji wa vipaji vya vijana na kuwaendeleza ni miongoni mwa sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kufifia kwa vipaji vya vijana wengi chipukizi, hasa waliopo vijijini.
Msanii huyo alianza kujihusisha na muziki tangu akiwa mdogo kwa kutunga na kuimba nyimbo za kaswida alipokuwa madrasa.
Alianza kung’ara kimuziki mwaka 2008 baada ya kurekodi wimbo wake wa kwanza, unaokwenda kwa jina la ‘Kafia ghatto’. Baadaye aliibuka na kibao cha ‘Full Shangwe’, alichomshirikisha Ambwene Yesaya ‘AY’.
Nyimbo hizo pamoja na ‘Maji yakimwagika’, ‘Niambie’ na zinginezo, zinapatikana katika albamu yake ya kwanza, aliyoitoa mwaka huo, inayojulikana kwa jina la ‘Promise’.
Baadaye, Machozi aliibuka na albamu yake ya pili, inayokwenda kwa jina la ‘Kwa ajili yako’, aliyoirekodi kwenye studio za Tetemesha zilizopo mjini Mwanza.
Machozi pia amewahi kushirikishwa katika kibao cha ‘Nimekosa nini’ cha msanii mwingine nyota wa muziki huo, H. Baba. Msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1986 wilaya ya Manyoni mkoani Singida, bado hajaoa.

Hii ndiyo Wydad Casablanca, itakayocheza na Simba


WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Simba mwishoni mwa wiki iliyopita walishinda rufani yao dhidi ya mabingwa watetezi, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Katika rufani hiyo, iliyowasilishwa mwezi uliopita kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Simba iliilalamikia TP Mazembe kwa kumchezesha mchezaji Janvier Besala Bokungu katika mechi ya awali kati yao kinyume cha kanuni za usajili.
Simba ilidai kuwa, Bokungu hakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa vile bado alikuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia. Simba ilitolewa katika michuano hiyo na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3.
Kufuatia rufani hiyo, CAF imeiondoa TP Mazembe katika michuano hiyo na kuipatia nafasi hiyo Simba, ambayo sasa imepangwa kucheza mechi moja na Wydad Casablanca ya Morocco kati ya Mei 27 hadi 29 katika uwanja huru utakaotangazwa baadaye.
Mshindi wa mechi hiyo, atacheza hatua ya makundi ya ligi hiyo katika kundi B. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Al Ahly ya Misri, EST ya Tunisia na Moloudia Club ya Algeria.
Iwapo Simba itapoteza mechi hiyo, itaangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho na kucheza hatua ya mtoano dhidi ya DC Motema Pembe ya Congo.
Kurejeshwa kwa Simba katika michuano hiyo kumezua maswali mengi. Wapo wanaoipongeza Simba kwa kuweza kutetea haki yake na wengine wanaionea huruma kwa vile kwa sasa haina kikosi kinachoweza kuhimili mikikimikiki ya Wamorocco hao.
Tangu kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, wachezaji wengi wa Simba walitawanyika. Wapo waliouzwa kwa klabu zingine za nje kama vile Mbwana Samatta na Patrick Ochan na wapo waliouzwa kwa mkopo kwa klabu zingine.
Tayari pia Simba ilishatangaza kuwatema wachezaji wengine kadhaa kwa madai ya viwango vyao kushuka na wengine walishutumiwa kwa kuwashawishi wenzao wacheze chini ya kiwango ili timu hiyo ishindwe kutetea ubingwa wake. Simba ilimaliza ligi hiyo ikiwa ya pili.
Hata hivyo, inatia moyo kuona kwamba Simba imeshaanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya pambano hilo na wachezaji wake kadhaa wa zamani wameshaanza kuripoti kambini isipokuwa Emmanuel Okwi aliyeko Afrika Kusini, Hillary Echessa aliyemaliza mkataba wake na Joseph Owino aliyejiunga na Azam. Timu hiyo ipo chini ya Kocha Moses Basena kutoka Uganda.
Wachezaji wa Simba walioripoti kwenye mazoezi ya timu hiyo hadi juzi ni Uhuru Selemani, Rashid Gumbo, Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Juma Nyoso, Shija Mkina, Juma Jabu, Patrick Ochan, Nico Nyagawa, Jerry Santo, Abdulrahim Humud, Salum Gila, Mohamed Banka, Salum Aziz na Juma Kaseja.
Swali kubwa wanalojiuliza mashabiki wa soka nchini ni iwapo Simba itaweza kuimudu Wydad Casablanca bila kuwa na mazoezi ya muda mrefu. Wapinzani wao hao bado wanashiriki katika michuano ya ligi ya Morocco.
Wydad ni timu yenye mafanikio makubwa nchini Morocco, ikiwa imetwaa ubingwa wa nchi hiyo mara 12, sawa na FAR Rabat. Wydad pia imeshika nafasi ya pili mara tisa wakati FAR wameshika nafasi hiyo mara sita.
Raja Casablanca, ambayo ni maarufu zaidi nchini kutokana na kupambana na Yanga mwaka 1998, ni ya tatu kwa kuchukua ubingwa wa Morocco mara sita.
Wydad pia imeweka rekodi ya kushinda Kombe la Morocco mara tisa wakati FAR Rabat imelinyakua mara 11. Raja Casablanca ni ya tatu kwa kulitwaa mara sita.
Katika historia yake, Wydad imetwaa ubingwa wa Afrika mara moja mwaka 1992. Mwaka 2002 walitwaa Kombe la Washindi la Afrika na mwaka 1994 walitwaa ubingwa wa nchi za Afrika zenye asili ya kiarabu.
Kikosi cha Wydad kimesheheni nyota wengi wanaocheza katika ligi hiyo na kutoka nje ya nchi. Mmoja wa washambuliaji hao nyota kutoka nje ni Luiz Jeferson Escher kutoka Brazil, ambaye alinunuliwa msimu huu kutoka Kawkab Marrakech ya huko huko Morocco.
Nyota wengine, ambao timu hiyo inajivunia ni pamoja na jean Louis Paschal Angan na Fabrice N’Guessi, ambaye ni raia kutoka Congo. Angan ni mchezaji wa kimataifa wa Benin.
Katika wachezaji wa nyumbani, Wydad inajivunia nyota wake, Youness Mankari. Kocha Mkuu wa timu hiyo ni Fakhreddine Rahji.

Aki na Ukwa wawekwa kikaangoni


LAGOS, Nigeria
BAADHI ya wazazi nchini Nigeria wametishia kuzipiga marufuku filamu zilizochezwa na waigizaji machachari, Aki na Ukwa kwa madai kuwa, zinatoa mafundisho mabaya kwa watoto wao.
Wazazi hao wamesema, filamu nyingi zinazochezwa na vijana hao wenye vimo vifupi, zinaonyesha dharau kwa watu wazima na kuwafundisha wizi vijana. “Vijana wengi wamekuwa wakiiga matukio yanayofanywa na Aki na Ukwa kwenye filamu wanazocheza, hivyo kuathirika,” amesema mmoja wa wazazi hao, aliyehojiwa na mtandao wa Nigeriafilms.
Mzazi mwingine alisema, matukio ya wizi yamekuwa yakiongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma, wahusika wakuu wakiwa vijana wa umri mdogo kutokana na kuiga tabia za wacheza filamu hao.
Wazazi hao wamedai kuwa, vijana wengi wa umri mdogo nchini Nigeria wanapenda kuishi maisha yanayofanana na yale ya Aki na Ukwa bila kujua kuwa ni ya uigizaji.
Baadhi ya wazazi wamehoji ni kwa nini filamu zote wanazoshiriki kucheza vijana hao, zinaonyesha vitendo vya uovu katika jamii badala ya mafundisho mema.
“Kama huonyeshi matendo mazuri kwa vijana wako nyumbani, lazima watakuiga,”alisema mmoja wa wazazi hao.
Mzazi huyo alisema wanawapa changamoto waandaaji wa filamu wa Nollywood, kubadili mwelekeo kwa kuandaa sinema, ambazo haziwezi kuathiri maisha ya vijana wao.
“Wanapaswa kutengeneza filamu zenye mwelekeo chanya. Vijana ni wepesi wa kuiga na wakifanya hivyo, wanaonyesha picha mbaya ya Wanigeria,”aliongeza.
Aki na Ukwa ni miongoni mwa wacheza filamu waliojipatia sifa na umaarufu nchini Nigeria kutokana na kucheza filamu nyingi na zinazopendwa na vijana wengi.

CHIOMA: Fani ya filamu inalipa Nigeria


LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI nyota wa kike wa filamu nchini Nigeria, Chioma Akpotha amekiri kuwa, kazi hiyo inalipa na imemwezesha kupata vitu vingi, ambavyo hakuvitarajia katika maisha yake.
Chioma aliueleza mtandao wa Nigeriafilms wiki hii kuwa, kwa sasa anaweza kuishi maisha ya kutanua, ambayo huko nyuma hakuweza kuyamudu na pia amepata tuzo na zawadi nyingi.
“Nimepata tuzo nyingi kiasi kwamba ziwezi kuzitaja moja moja. Licha ya kuwa mwigizaji, ninafanya mambo mengi, ambayo sipendi kuyataja,”alisema.
Mwanadada huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, pamoja na Nigeria kupiga hatua kubwa kimaendeleo katika fani hiyo, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ili kuiboresha zaidi.
Alisema licha ya nchi hiyo kushika nafasi ya tatu duniani kwa utengenezaji wa filamu nyingi, wanahitajika kuwa makini zaidi hasa katika masuala ya kiufundi.
Alilitaja tatizo lingine kubwa linaloikumba fani hiyo kuwa ni wizi wa kazi za sanaa. Alisema licha ya kuwepo kwa sheria ya hakimiliki, bado haijaweza kufanyakazi yake sawa sawa katika kupambana na wahalifu hao.
Chioma alisema hadi sasa hajaweza kutengeneza filamu yake mwenyewe, lakini yupo katika mchakato huo na kwamba hivi karibuni huenda mambo yakawa safi.
Alipoulizwa ni kwa nini amekuwa akipewa nafasi nzuri pekee katika uigizaji wa filamu za Nollywood, Chioma alisema huo ni uamuzi wa watayarishaji wa filamu.
“Sielewi kwa nini napewa nafasi nyingi za aina hiyo, lakini nafikiri ni kwa sababu ndizo ninazozimudu zaidi. Katika fani hii, waongozaji filamu wanapogundua wewe ni mzuri katika nafasi fulani, wanakupatia hiyo hiyo,”alisema.
“Nitakupa mfano. Mkongwe Patience Ozorkwor, ambaye alianza kucheza filamu kwa kupewa nafasi za kawaida na kufanya vizuri, lakini alipojaribiwa katika nafasi ya mama mkwe mwenye roho mbaya, ameendelea nayo kwa sababu alifanya vizuri zaidi,”aliongeza.
Chioma alisema tangu alipojitosa kwenye fani hiyo mwaka 1998, amekuwa akivutiwa na Kate Henshaw-Nuttall, aliyempa moyo wa kujiunga nayo pamoja na wacheza filamu, Joke Silva na Ramsey Nouah.
Mwigizaji huyo, ambaye ameolewa na kuzaa mtoto mmoja alisema, fani hiyo haijaathiri maisha ya familia yake kwa vile anao muda wa kutosha kuihudumua.
“Huwa ninahakikisha kuwa, naihudumia familia yangu kwanza kabla ya kwenda kazini, hasa kama ni nje ya mji. Kama ambavyo siku zote nimekuwa nikisema, mimi natoka familia ya kikristo,”alisema.
Vilevile alisema fani hiyo imemwezesha kuteuliwa kuwa balozi wa Afrika katika kampuni ya mawasiliano ya Globacom na pia kutwaa tuzo mbalimbali. Miongoni mwa tuzo hizo ni ule ya mwigizaji bora wa kike wa mwaka 2007.
Jambo pekee, ambalo Chioma halipendi katika maisha yake ni wizi. Alisema anachukia wizi na kamwe hawezi kukutwa akiiba kitu chochote.

Monday, May 16, 2011

Simba ikifungwa na Wydad, kuangukia Kombe la Shirikisho

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 16, 2011
SIMBA v WYDAD CASABLANCA
Mechi ya kutafuta nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuondolewa kwa kuchezesha mchezaji asiyestahili imepangwa kufanyika kati ya Mei 27, 28 na 29 mwaka huu kwenye uwanja huru (neutral ground).
Simba ya Tanzania na Wydad de Casablanca ya Morocco ndizo zitakazopambana katika mechi hiyo ya mkondo mmoja. Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linatarajia kutaja katika muda mfupi ujao nchi ambapo mechi hiyo itachezwa.
Timu itakayoshinda itaingia katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, ikiwa kundi B pamoja na Al Ahly ya Misri, Esperence (Tunisia) na Moloudia Club d’Alger ya Algeria.
Timu itakayoshindwa itaingia katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo itacheza mechi ya kwanza nyumbani na Daring Club Motema Pembe ya DRC kati ya Juni 10, 11 na 12 mwaka huu.

MAPATO STARS v BAFANA BAFANA

Pambano la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana) lililochezwa Mei 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 75,888,000 kutokana na watazamaji 10,554 walionunua tiketi.
Watazamaji 240 walilipa sh. 30,000, 585 (sh. 20,000) na 1,423 (sh. 10,000), 614 (sh. 7,000) na 7,692 (sh. 5,000).
Baada ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 11,576,135.59 na gharama za awali za mchezo ambazo ni sh. 21,843,600.00 mgawo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 10 kwa uwanja sh. 4,246,826.44, asilimia 10 kwa gharama za mchezo sh. 4,246,826.44, asilimia 5 kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 2,123,413.22 na asilimia 75 kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 31,851,198.31.

Nacho Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata asilimia tano kutoka kwa mgawo wa TFF ambayo ni sh. 1,592,559.92.

SEMINA YA WAAMUZI WA FIFA

Semina kwa waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) itafanyika Dar es Salaam kuanzia Mei 17 hadi 19 mwaka huu. Wakufunzi wa semina hiyo ni Riziki Majalla, Leslie Liunda na Omari Kasinde.

Waamuzi hao ni Ramadhan Ibada, Waziri Sheha, Oden Mbaga, Judith Gamba na Israel Mujuni. Waamuzi wasaidizi ni Hamis Chang’walu, Ally Kombo, Saada Tibabimale, Josephat Bulali, Samuel Mpenzu, Erasmo Jesse, Mwanahija Makame, John Kanyenye na Khamis Maswa.

Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF

Sunday, May 15, 2011

RATIBA KOMBE LA TAIFA


Mei 15, 2011
ROBO FAINALI KILI TAIFA CUP
Hatua ya robo fainali ya Kili Taifa Cup inaanza Mei 22 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Robo fainali zitachezwa mechi mbili kwa siku. Ya kwanza saa 8.00 mchana na ya pili saa 10.00 jioni.
Mei 22 mechi ya kwanza ni Singida (Kindai Shooting Stars) na Ilala. Mechi ya pili ni Mwanza (Mwanza Heroes) na Arusha (Mount Meru Warriors). Mei 23 mechi ya kwanza ni Mbeya na Ruvuma (Ruvuma Warriors) wakati ya pili ni timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 23 (U23) na Kagera (Lweru Eagles).
Nusu fainali ya kwanza itakayohusisha washindi wa robo fainali za Mei 22 itachezwa Mei 24. Ya pili itachezwa Mei 25 wakati Mei 26 itakuwa mapumziko. Mechi ya mshindi wa tatu itakuwa Mei 27 na fainali itachezwa Mei 28.Waamuzi watakaochezesha hatua hiyo ambao wote wana beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ni Israel Mujuni, Judith Gamba na Oden Mbaga. Waamuzi wasaidizi ni Samwel Mpenzu, Hamis Chan’gwalu, Saada Tibabimale, Zahra Hussein, John Kanyenye na Erasmus Jesse.
Makamishna wa mechi ni Hakim Byemba na Mrisho Bukuku wakati mtathmini wa marefa (referee assessor) ni Charles Mchau. Msimamizi wa fainali hizo ni Khalifa Mgonja ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
MALALAMIKO KILI ATAIFA CUP
Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana leo (Mei 15 mwaka huu) ilipitia taarifa za michuano hiyo hatua ya makundi ikiwemo malalamiko ya timu za Mara na Dodoma ambazo zililalamikia usajili wa mchezaji mmoja katika timu za Kigoma na Kagera. Kamati haikusikiliza malalamiko hayo kwa vile yaliwasilishwa nje ya muda wa pingamizi.


Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF

RATIBA LIGI YA TAIFA

Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa itaanza Juni 11 mwaka huu katika vituo vya Sumbawanga, Kigoma, Singida na Kibaha.
Washindi watatu wa kwanza wa kila kituo watashiriki hatua ya fainali itakayofanyika katika kituo kitakachotangazwa baadaye.Kituo hicho cha fainali kitakuwa na makundi matatu ya timu nne nne.
Mshindi wa kila kundi na washindwa bora (best losers) wawili, hivyo kufanya jumla ya timu tano ndizo zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Kituo cha Sumbawanga kitakuwa na timu za Small Kids (Rukwa), Ilonga FC (Mbeya), Mlale JKT (Ruvuma), Central Police (Dar 3), Tumbaku SC (Morogoro) na mabingwa wa Iringa.
Kituo cha Kigoma kitakuwa na timu za Shinyanga United (Shinyanga), Geita Veterans (Mwanza), Polisi SC (Mara), Kasulu United (Kigoma), Rumanyika FC (Kagera) na mabingwa wa Tabora.
Singida itakuwa na timu za Polisi SC (Arusha), Babati Mashujaa SC (Manyara), Lang’ata Bora FC (Kilimanjaro), Samaria FC (Singida) na Majengo FC (Dodoma).
Kituo cha Kibaha ni Cosmopolitan (Dar 1), Mgambo Shooting (Tanga), Mailimoja United (Pwani), Sifapolitan (Dar 2), Liwale Stars (Lindi) na mabingwa wa Mtwara.
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Mei 15 mwaka huu) imesisita kuwa iwapo mikoa ya Tabora, Iringa na Mtwara itakuwa haijawasilisha majina ya mabingwa wao katika muda uliopangwa ligi hiyo itaendelea bila timu zao kuwemo.
Mwisho wa timu kuthibitisha kushiriki na kulipa ada ya ushiriki ya sh. 70,000 ni Mei 20 mwaka huu. Mei 28 mwaka huu ndiyo siku ya mwisho ya kurudisha fomu za usajili.Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF

Nchimbi kukutana na wadau wa sanaa

National Arts Council BASATA 12/05/2011
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dr. Emmanuel Nchimbi (Mb), atakutana na wasanii katika ukumbi wa BASATA kuanzia tarehe 17 Mei na tarehe 18 Mei, 2011.Waziri ataongea na wasanii kwa utaratibu ufuatao:-17/05/2011 (Jumanne) Saa 4:00 asubuhi Wasanii Wote wa Sanaa za Muziki 18/05/2011 (Jumatano) Saa 4:00 asubuhi Wasanii Wote wa Sanaa za Ufundi,Filamu na MaonyeshoIzingatiwe kwamba Waziri ataongea na wasanii wa muziki wa aina zote wakiwemo wa Kizazi kipya,Bendi,Disco, Asili,Taarab na kadhalika katika siku ya kwanza.Katika siku ya pili yaani Tarehe 18/05/2011 ataongea na wasanii wa Sanaa za Filamu,Maonyesho na Ufundi pekee.Wasanii Wote mnaombwa kujitokeza kwa wingi.Lengo kuu la mikutano hii kati ya Waziri na Wasanii ni kuongelea maendeleo ya fani za sanaa.Ghonche Materego
KATIBU MTENDAJI
Mei 15, 2011

Thursday, May 12, 2011

MWANAHAWA ALLY: Siwezi kuacha kuimba taarabAsema muziki huo umemnufaisha na kumfikisha alipo sasa

Adai kamwe hatoisahau ajali iliyoua wasanii 13 wa Five Stars

Aamua kujiunga na East African Melody kama 'deiwaka'

MWIMBAJI mkongwe wa muziki wa taarab nchini, Mwanahawa Ally amesema kwa sasa hategemei kurudi katika kundi lake la Jahazi kutokana na mambo waliyomfanyia.
Amesema hivi sasa anaendelea na kazi yake ya uimbaji katika kundi la East African Melody la jijini Dar es Salaam na tayari amesharekodi kibao kinachoitwa 'Rabi nilinde na wenye nia mbaya'.
Mwanahawa aliyasema hayo juzi alipozungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa makala hii na kuongeza kuwa, hataki kuendelea kufanyakazi zake kwa kutegemea Jahazi.
Alisema yeye ni mwimbaji mzoefu na anayesifika ndani na nje ya nchi na kwamba kipaji chake ni cha kuzaliwa na si cha kutegemea kundi au mtu. Alisema uwezo alionao ndio uliomfikisha hapo alipo.
"Kwangu mimi Jahazi ni kama kundi la kawaida, siwezi kulipapatikia wala sina haja nalo, kipaji na uwezo nilionao unanitosha na unanifanya nitambe,"alisema mwanamama huyo mwenye umri unaokadiwa kuwa zaidi ya miaka 60.
"Nimeanza kazi hii ya uimbaji wakati hao waimbaji wa Jahazi hawajazaliwa na hadi sasa nipo kwenye fani na ninawika, siwezi kubembeleza mtu na wala sijaona cha kubembeleza," alisema gwiji huyo wa mipasho mwenye sauti ya kuvutia.
Alisema baada ya kujiondoa Jahazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kutoelewana na baadhi ya waimbaji pamoja na uongozi wa kundi hilo, amerudi katika kundi la East African Melody, ambako anaimba kama kibarua.
Muimbaji huyo aliyewahi kutamba na wimbo wa 'Kinyago cha Mpapure' na kujipatia umaarufu mkubwa alisema, akiwa katika kundi hilo, anafanya shughuli zake bila kuingiliwa na mtu.
Alisema kutokana na uwezo mkubwa wa uimbaji alionao, hawezi kubabaishwa na kundi lolote na anajiamini kwamba anaweza kufanyakazi sehemu yoyote.
Mwimbaji huyo, mwenye umbo kubwa na sauti ya kuvutia alisema, hajafikiria kuachana na kazi ya uimbaji kwani ni sehemu ya maisha yake na anaipenda kuliko kazi nyingine yoyote.
"Bado sijafikiria siku ya kuacha kuimba, kazi hii ndio iliyoniweka mjini hadi sasa, ninaendesha familia yangu kwa kazi hii, kwa hiyo bado ninaiheshimu sana," alisema mwimbaji huyo, anayetamba na kibao cha 'Roho mbaya siyo mtaji' alichokiimba akiwa Jahazi.
Mkongwe huyo wa mipasho pia alisema hana mpango wa kuhamia katika kundi la Fiver Stars 'Watoto wa Bongo' hata kama ataombwa kujiunga na kundi hilo.
Alisema mawazo yake ameyaelekeza kwenye makundi makongwe, likiwemo Melody kutokana na kusheheni waimbaji wenye umri unaoendana naye.
"Hata nikiombwa niende Fiver Stars, siwezi kwenda kwa sasa, watanisumbua tu, kiwango changu hakiendani nao," alisema mwimbaji huyo aliyenusurika kufa katika ajali ya gari akiwa na kundi hilo hivi karibuni.
Ajali hiyo ilitokea Machi 21 mwaka huu baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam, kulivaa lori lililokuwa limeegeshwa kando mwa barabara na baadae kupinduka na kusababisha vifo vya wasanii 13 wa kundi la Fiver Stars, akiwemo mwimbaji nyota wa kundi hilo Issa Kijoti.
Ajali hiyo ilitokea saa 2.30 usiku, ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, umbali wa kilomita sita kutoka lango kuu la kuingia hifadhini, ambapo wasanii wengine sita waliokuwa kwenye gari hilo walijeruhiwa.
Mwanahawa aliambatana na kundi hilo kama mwimbaji mwalikwa na katika ajali hiyo, aliumia mkono na kupelekwa Kenya kwa matibabu.
Akizungumzia afya yake baada ya ajali hiyo, Mwanahawa alisema anaendelea vizuri na anafanya shughuli zake kama kawaida.
Alisema katika maisha yake hawezi kuisahau ajali hiyo, na ndio kubwa aliyowahi kukumbana nayo tangu kuzaliwa.
"Itachukua muda mrefu kuisahau ajali kama ile ambayo ilipoteza roho za wasanii wezewtu 13 kwa mpigo, ninamuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu pahala pema peponi Amina," alisema.

Birmingham yaafiki kukipiga na Simba, Yanga

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage (kulia) akimkabidhi vipeperushi mbalimbali vinavyoonyesha Utalii wa Tanzania, Kocha Msaidizi wa timu ya Barningham City ya Uingereza, Andy Watson wakati walipokutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO Jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kuzungumzia ujio wa timu hiyo nchini. ( Picha na Mwanakombo Jumaa wa MAELEZO)UONGOZI wa klabu ya Birmingham City ya England, umekubali kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu za Simba na Yanga.
Uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kukubali kucheza mechi hizo, umekuja baada ya kuridhishwa na ubora wa Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam na hospitali ya Agakhan.
Mabingwa hao wa Kombe la Carling wamesema, kikosi chao kitatua nchini mwanzoni mwa mwezi Julai kwa ajili ya mechi hizo, ambazo watazitumia kujiandaa kwa michuano ya Ligi ya Ulaya na Ligi Kuu ya England.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mjini Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Andly Watson alisema wameridhishwa na mazingira ya Tanzania pamoja na masharti waliyotoa kwa uongozi wa Simba.
Alisema kikosi chake kinatarajiwa kuja nchini na nyota wake wote na kwamba kitaanza kucheza mechi yake ya kwanza Julai 12 dhidi ya Simba kabla ya kuvaana na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Yanga, Julai 14, mwaka huu.
Andly alisema katika msafara huo, timu yake inatarajiwa kuongozana na mashabiki wapatao 1,000 na baada ya kucheza michezo hizo, watatembelea mbuga mbalimbali za wanyama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage alisema, maandalizi kwa ajili ya mechi hizo za kirafiki yamekamilika na kwamba wao kama Simba, wamejiandaa kikamilifu.
Rage alisema baada ya Birmingham kucheza michezo hiyo, wachezaji na viongozi wake watapata fursa ya kutembelea vivutio vya kitalii kama vile mbuga za wanyama za Serengeti na Mikumi.
Alisema ujio wa timu hiyo nchini, utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa sababu utasaidia kutangaza vivutio vya kitalii katika nchi za Ulaya na kwingineko duniani.

Ngasa hauzwi ng'o-Azam


UONGOZI wa klabu ya soka ya Azam FC umeweka wazi kuwa, hauna mpango wowote wa kumuuza mshambuliaji Mrisho Ngasa kwa klabu ya Yanga.
Msimamo huo ulielezwa jana na Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrisa alipokuwa akizungumza na Burudani kuhusu maombi ya Yanga kutaka kumsajili mchezaji huyo.
Nassor alisema kwa sasa, hawatarajii kuuza mchezaji yeyote kwa sababu wamepania kutengeneza kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
“Tumeamua kwamba, hatutaki kuuza mchezaji yoyote katika kipindi hiki na Ngasa ni miongoni mwa wachezaji waliomo kwenye mipango yetu ya baadaye na tunaamini mchango wake bado unahitajika,”alisema Nassor.
Katibu Mkuu huyo wa Azam alisema, wameshaiandikia barua Yanga kuijulisha kuhusu uamuzi wao huo na kusisitiza kuwa, sera ya klabu yake ni kuuza wachezaji wao nje ya nchi.
“Tunaposema sera yetu ni kuuza wachezaji wetu nje, maana yake ni kwamba tunataka kupata pesa za kununua wachezaji chipukizi, ambao wataweza kuisaidia timu yetu na nchi kwa jumla,”alisema.
Nassor alisema wameshangazwa na hatua ya viongozi wa Yanga kukutana kwanza na mchezaji huyo na kuzungumza naye kabla ya kufanya hivyo kwa viongozi wa Azam kama kanuni za usajili zinavyosema.
"Ngasa ana mkataba na Azam FC wa miaka mitatu, kamwe hatupo tayari kuona taratibu zinavunjwa kwa mchezaji wetu kukutana au kuzungumza na timu yoyote bila ridhaa yetu,"alisema kiongozi huyo.
Msimamo huo wa Azam umekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kuripoti kuwa, mchezaji huyo amekubali kurejea Yanga.
Hata hivyo, Ngasa aliwataka viongozi wa Yanga kufanya mazungumzo kwanza na uongozi wa Azam ili waweze kufikia makubaliano.
Ngasa alisajiliwa na Azam msimu uliopita kwa dau la sh milioni 58 na ameisaidia timu hiyo kumaliza michuano ya ligi kuu msimu huu ikiwa nafasi ya tatu na pia kuibuka mfungaji bora.

Rage aionya Yanga kuhusu Asamoah

Ochan auzwa TP Mazembe kwa mil 150/-

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ameionya Yanga kuwa, inafanya makosa makubwa kutaka kumsajili tena mshambuliaji Kenneth Asamoah bila kufanya mazungumzo na klabu yake ya FK Jagodina ya Serbia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Rage alisema kwa mujibu wa kanuni za usajili, viongozi wa klabu hawapaswi kuzungumza na mchezaji kabla ya kupata ruhusa ya viongozi wake.
Rage alikiri kuwa, ni kweli kwamba Yanga imeshafanya mazungumzo na mchezaji huyo kwa ajili ya kumsajili tena msimu ujao na anatarajiwa kutua nchi leo, lakini wanaweza kukwama kwa vile hawajapata ridhaa ya klabu yake.
“Kanuni zinasema wazi kwamba, klabu ndizo zinazopaswa kufanya mazungumzo kwanza kuhusu usajili wa mchezaji ndipo baadaye yanafuata mazungumzo ya mchezaji na klabu inayotaka kumsajili,”alisema Rage.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, wao bado wanaendelea kufanya mipango ya kumsajili mshambuliaji huyo, lakini wameamua kwanza kuzungumza na klabu yake.
“Kama tutakubaliana na viongozi wa klabu yake, nina hakika tunaweza kumsajili mshambuliaji huyo,”alisema.
Hivi karibuni, Rage alikaririwa akisema kuwa, wamemtuma Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kwenda Serbia kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa klabu hiyo baada ya Asamoah kuwasilisha maombi ya kutaka asajiliwe na klabu hiyo.
Asamoah, ambaye alikuwa akicheza soka ya kulipwa nchini Serbia, alisajiliwa na Yanga msimu uliopita, lakini alishindwa kuichezea baada ya klabu hiyo kushindwa kumlipia ada ya uhamisho.
Usajili wa Asamoah uligubikwa na utata mkubwa msimu uliopita baada ya klabu yake ya FK Jagodina ya Serbia kugoma kumpatia uhamisho wa kimataifa (ITC) baada ya Yanga kushindwa kumlipia ada ya uhamisho.
Katika hatua nyingine, klabu ya Simba imesema imemuuza kiungo wake, Patrick Ochan kutoka Uganda kwa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa gharama ya sh. milioni 150.
Rage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi wa TP Mazembe umekubali kutoa kiasi hicho cha fedha baada ya kuridhishwa na kiwango cha Ochan.
Ochan anakuwa mchezaji wa pili wa Simba kuuzwa kwa TP Mazembe katika kipindi cha mwezi mmoja. Hivi karibuni, Simba pia ilimuuza mshambuliaji wake, Mbwana Samatta kwa kiasi hicho cha pesa kwa TP Mazembe.
Mabingwa hao wa Afrika walivutiwa na Samatta na Ochan wakati timu hiyo ilipokutana na Simba katika mechi za raundi ya pili ya michuano ya klabu bingwa Afrika zilizochezwa Machi mwaka huu.

Azam yaanika bunduki zake

UONGOZI wa Azam umetangaza kikosi cha wachezaji 21, ambacho hadi sasa wamesajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Taarifa iliyotolewa na tovuti ya klabu hiyo jana imeeleza kuwa, kwa sasa klabu hiyo imebakisha nafasi tatu za kusajili, ambazo ni beki wa kati na mshambuliaji kutoka nje na beki mwingine wa kati wa hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, beki wa kati na mshambuliaji kutoka nje, watasajiliwa kutoka nchini Ghana. Hata hivyo, tovuti hiyo haikutaja majina ya wachezaji hao.
Hivi karibuni, Azam ilifanikiwa kumsajili mshambuliaji Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast, ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Tusker Chalenji iliyofanyika mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Kusajiliwa kwa mchezaji huyo kumeifanya Azam iwe imesajili wachezaji wa kigeni watatu hadi sasa. Wengine ni nahodha Ibrahim Shikanda, aliyebakishwa kwenye usajili na kipa wa zamani wa Yanga, Obren Circovic kutoka Serbia.
Azam imesema katika usajili wake wa msimu ujao, imeamua kusajili wachezaji wapya saba na kuwaongezea mikataba wachezaji wa zamani 14.
Wachezaji wengine wapya ni kipa Mwadini Ali Mwadini na waziri Salum Omar kutoka Mafunzo ya Zanzibar, Ghulam Abdallah kutoka Chuoni Zanzibar, kiungo Abdulhalim Humud kutoka Simba,Zahor Pazi kutoka African Lyon, Said Murad kutoka Kagera Sugar na Khamis Mcha Vuai kutoka Ocean View ya Zanzibar.
Katika usajili wake huo, Azam pia imempandisha daraja kipa Daudi Mwasongwe na kuendelea kuwapa nafasi wachezaji chipukizi,Himid Mao, Salum Abubakar na Jamal Mnyate.
Wachezaji wengine walioendelea kufunga pingu na Azam kwa ajili ya msimu ujao ni mabeki Aggrey Moris, Malika Ndeule, Lackson Kakolaki na Erasto Nyoni. Viungo ni Ramadhani Chombo, Ibrahim Mwaipopo, Seleman Selembe, Kalimangonga Ongala, Jabir Azizi na Mrisho Ngassa wakati mshambuliaji pekee aliyebakishwa ni John Bocco.

Noorah, Tundaman watoka na vitu vipya

Noorah

Tundaman


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, wasanii wawili nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Tundaman na Noorah wameibuka na vibao viwili vipya.
Wakati Tundaman ameibuka na kibao kinachokwenda kwa jina la ‘Lugha gongana’, Noorah ameshusha kibao kinachoitwa ‘Starehe gharama’.
Tundaman alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amerekodi kibao chake hicho chini ya mtayarishaji maarufu wa muziki, anayejulikana kwa jina la Maneck.
Aliongeza kuwa, picha za video ya wimbo huo zimepigwa na Kampuni ya Visual Lab Next Lever.
Kwa mujibu wa Tundaman, tayari kibao hicho kimeshaanza kusikika na redioni na kuonyeshwa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni nchini.
Naye Noorah, ambaye ni msanii wa kundi la East Zoo alisema, kibao chake hicho kipya kimetengenezwa kwenye studio za B Hits chini ya mtayarishaji mahiri wa muziki, Hermy B.
Noorah amerekodi kibao chake hicho baada ya kuwa kimya kwa zaidi ya miaka mitatu. Alisema ukimya wake huo ulitokana na uamuzi wake wa kwenda kupiga kitabu.
Kibao hicho kinasimulia maisha ya msichana mmoja, aliyejitosa kimapenzi kwa kijana wa kiume, ambaye lugha ya Kiingereza inampiga chenga.
Licha ya kibao hicho kusimulia maisha ya msichana, kimeimbwa na Noorah mwenyewe na kuwekwa vikorombwezo na Hermy B kutokana na teknolojia inayopatikana kwenye studio yake.