KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

Simba, Casablanca kukipiga Cairo



PAMBANO la kutafuta timu itakayocheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa wa Afrika kati ya Simba na Wydad Casablanca ya Morocco litachezwa Mei 28 mwaka huu kwenye uwanja wa Petrosport mjini Cairo, Misri.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, iwapo timu hizo zitamaliza dakika 90 zikiwa sare, mshindi itabidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano.
Wambura alisema uamuzi huo umefikiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kuamuru timu hizo zicheze mechi ya mkondo mmoja kwenye uwanja huru.
Kwa mujibu wa ofisa huyo wa TFF, Chama cha Soka cha Misri (EFA) ndicho kilichopewa jukumu la kuzipokea timu za Simba na Wydad Casablanca zitakapowasili mjini Cairo.
Aliongeza kuwa, kila timu imetakiwa kujigharamia usafiri wa kwenda Cairo na kurudi pamoja na gharama za malazi. Alisema gharama zingine zozote zitakazojitokeza, zitabebwa na timu hizo kupitia vyama vyao vya soka.
Wambura alisema pia kuwa gharama za waamuzi wa mchezo huo pamoja na kamishna, zikiwemo usafiri wa ndani na malazi, nazo zitabebwa na timu hizo kupitia vyama vyao vya soka.
“Mapato yatakayopatikana kutokana na viingilio vya mechi hiyo, yatagawiwa nusu kwa nusu kwa timu zote mbili kupitia vyama vyao vya soka,”alisema Wambura.
Simba imerejeshwa katika michuano hiyo, baada ya kushinda rufani yao waliyokata kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Timu hiyo ya Tanzania ilikata rufani CAF ikipinga TP Mazembe kumchezesha mchezaji Janvier Besala Bokungu katika mechi ya awali ya raundi ya pili kati yao kinyume cha kanuni za usajili.
Simba ilidai kuwa, Bokungu hakuwa mchezaji halali wa TP Mazembe kwa vile bado alikuwa na mkataba na klabu yake ya zamani ya Esperance ya Tunisia. Simba ilitolewa katika michuano hiyo na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 6-3.
Kwa mujibu wa ratiba, mshindi wa mechi hiyo atacheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa wa Afrika katika kundi B. Timu zingine zilizopangwa kundi hilo ni Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia na Moloudia Club ya Algeria.
Iwapo Simba itapoteza mechi hiyo, itaangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho na kucheza hatua ya mtoano dhidi ya DC Motema Pembe ya Congo.

No comments:

Post a Comment