KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 8, 2011

Mkapa ang'ara tuzo za TASWA

RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa juzi alikuwa kivutio kikubwa kwa waandishi wa habari za michezo na wageni waalikwa wakati wa sherehe za utoaji tuzo za wanamichezo bora wa mwaka 2010.
Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye hoteli ya Movenpick mjini Dar es Salaam, Rais mstaafu Mkapa alitunukiwa tuzo ya heshima na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA).
Mkapa alitunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa wakati wa utawala wake, ambapo alijenga uwanja mpya wa michezo wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 uliopo jirani na Uwanja wa Uhuru, Temeke mjini Dar es Salaam.
Mara baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Masoud Saanani kutangaza jina la Mkapa kuwa ndiye aliyetunukiwa tuzo hiyo ya heshima, ukumbi mzima ulilipuka mayowe ya kumshangilia. Mkapa alikabidhiwa tuzo hiyo na Makamu wa Pili wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkapa alisema siku alipopewa barua ya mwaliko wa sherehe hiyo na pia maelezo kwamba atatunukiwa tuzo ya heshima, alipatwa na mshtuko.
Mkapa alisema mshtuko huo ulitokana na ukweli kwamba, wakati wa utawala wake, hakuwa kuhudhuria mechi yoyote ama kufanya harakati za kusukumuma shughuli za michezo.
“Lakini maelezo yake yalikuwa hivi, nyote mnakumbuka zama zile za ukapa. Waswahili wanasema, kupanga ni kuchagua. Wakati ule wa ukapa niliamua kuweka mkazo katika kukusanya kodi ili serikali iweze kutumia kile ilichonacho kujiendesha na baadaye kupigania kupata misamaha ya madeni,” alisema Mkapa huku akishangiliwa kwa mayowe mengi.
Mkapa alisema katika awamu ya pili ya uongozi wake, ndipo alipoamua kuwaachia kumbukumbu watanzania kwa kujenga uwanja mpya wa michezo kwa kutumia fedha za serikali na msaada kutoka serikali ya China.
“Ipo dhana kwamba uwanja huu ulijengwa na serikali ya China, hii si kweli hata kidogo. Ukweli ni kwamba uwanja huu ulijengwa kwa ubia kutokana na fedha zenu na za wananchi wa China,”alisema.
Rais mstaafu alisema miongoni mwa watu wanaopaswa kushukuriwa kutokana na kusaidia ujenzi wa uwanja huo ni aliyekuwa Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo, Profesa Juma Kapuya na Rais Jakaya Kikwete, ambaye wakati huo alikuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
“Kapuya ndiye aliyenihamasisha na kunipa moyo wa kujenga uwanja huo na Rais Kikwete ndiye aliyejenga hoja kwa serikali ya China ili itusaidie kujenga uwanja huo,”alisema Mkapa na kuamsha shangwe kutoka kwa wanamichezo na wageni waalikwa.
Mkapa aliipongeza TASWA kwa kutambua mchango wake huo na pia kuwaenzi wanamichezo mbalimbali kwa kuwapa tuzo kutokana na mafanikio waliyoyapata kwa mwaka 2010.

Mwanaidi mwanamichezo bora 2010

Nsajigwa ashinda tuzo ya mwanasoka bora, Okwi, Hasheem Thabeet nao wang’ara

MCHEZA netiboli Mwanaidi Hassan wa timu ya JKT Mbweni ameibuka kuwa mshindi wa tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka 2010 wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA).
Mwanaidi, ambaye pia aliibuka mwanamichezo bora wa netiboli kwa mwaka huo, alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal katika sherehe zilizofanyika juzi usiku kwenye hoteli ya Movenpick mjini Dar es Salaam.
Ushindi huo ulimwezesha Mwanaidi kuzawadiwa gari aina ya Toyota Cresta GX 100 lenye thamani ya sh. milioni 13 lililotolewa na wadhamini wa tuzo hizo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
Mbali na zawadi ya gari, Mwanaidi alizawadiwa fedha taslim sh. milioni moja kwa kushinda tuzo ya mwanamichezo bora wa netiboli pamoja na cheti.
Mwanaidi aliibuka mshindi wa jumla kufuatia kuiwezesha JKT Mbweni kuibuka bingwa wa ligi daraja la kwanza mwaka 2010, mfungaji bora wa ligi hiyo, aliuwezesha mkoa wa Temeke kutwaa ubingwa wa Kombe la Taifa na pia kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.
Sifa zingine zilizomwezesha Mwanaidi kushinda tuzo hiyo ni kung’ara katika mashindano ya kimataifa yaliyofanyika Singapore, akiwa mmoja kati ya wafungaji bora na pia kuisaidia timu ya taifa kufuzu kucheza fainali za dunia za mwaka 2010 na kuibuka mfungaji bora wa mashindano ya Afrika yaliyofanyika Afrika Kusini.
Tuzo ya mwanasoka bora, iliyoonekana kuwa na ushindani mkali na kuwagawa mashabiki wa mchezo huo, ilinyakuliwa na beki Shadrack Nsajigwa wa Yanga, aliyewabwaga kipa Juma Kaseja wa Simba, mshambuliaji Mrisho Ngasa wa Azam na Khamis Mcha wa Ocean View ya Zanzibar.
Nsajigwa alishinda tuzo hiyo kutokana na kuisaidia Yanga kushika nafasi ya pili ya ligi kuu msimu wa 2009/2010, kuisaidia timu ya Tanzania Bara kutwaa kombe la chalenji baada ya kulikosa kwa miaka 16 kwa kuifungia bao pekee na la ushindi kwa njia ya penalti dhidi ya Ivory Coast na kuibuka mchezaji bora wa michuano hiyo.
Mchezaji nyota wa mpira wa kikapu, Hasheem Thabeet aliibuka mshindi wa tuzo ya mwanamichezo bora wa Tanzania anayecheza nje wakati mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba alishinda tuzo ya mwanamichezo bora wa nje anayecheza nchini.
Hasheem na Okwi hawakuhudhuria sherehe hizo. Tuzo ya Hasheem ilipokelewa na mama yake mzazi wakati ile ya Okwi ilipokelewa na mdau wa Simba, Evans Aveva.
Mchezaji Asha Rashid wa Twiga Stars aliibuka mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa kike, Karama Nyilawila aliibuka mshindi wa tuzo ya bondia bora wa ngumi za kulipwa wakati Selemani Kidunda alishinda tuzo ya bondia bora wa ngumi za ridhaa.
Washindi wa tuzo nyingine ni Lilian Sylidion (mwanamichezo chipukizi), Marco Joseph (riadha-wanaume), Mary Naali (riadha-wanawake), Kevin Peter (wavu- wanaume), Hellen Richard (wavu-wanawake), George Otto (kikapu-wanaume), Faraja Malaki (kikapu-wanawake).
Wengine ni Hamisi Clement (baiskeli-wanaume), Sophia Anderson (baiskeli-wanawake), Kassim Nassor (kriketi-wanaume), Mariam Said (kriketi-wanawake), Masoud Amour Kombo (judo), Hawa Wanyeche (gofu-wanawake), Frank Roma (gofu-wanaume).
Washindi wa kila tuzo walipatiwa zawadi ya pesa taslim sh. milioni moja pamoja na cheti. Pesa hizo zilitolewa na wadhamini wa tuzo hizo, SBL.
Akizungumza wakati wa sherehe hizo, Dk. Bilal aliipongeza TASWA kwa kutambua mchango wa wanamichezo na kuwaenzi kwa kuwapa tuzo na pia kamati ya tuzo hizo kwa kufanyakazi yake kwa uadilifu mkubwa.
Dk. Bilal pia alimpongeza Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kutunukiwa tuzo ya heshima kutokana na mchango wake katika kukuza sekta ya michezo nchini.
Alisema Mkapa alistahili tuzo hiyo kutokana na ukweli kwamba uwanja mpya wa taifa ni urithi mkubwa kwa watanzania na utaiwezesha Tanzania kuandaa michuano mbalimbali ya kimataifa.





















No comments:

Post a Comment