KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 23, 2011

Utata wagubika kifo cha Wanjiru

Mama yake Wanjiru na mkewe

Maiti ya Wanjiru ikiingizwa kwenye gari la wagonjwa


Wanjiru, sehemu ya nyumba yake na mkewe


Samuel Wanjiru enzi zake


Ni milionea aliyejua viatu akiwa na miaka 14
Wanawake wamfanya afe na umri wa miaka 24
Ni bingwa wa dunia wa mbio ndefu za Beijing
Alivunja rekodi ya dunia ya miaka 44
Utata wa kifo chake wazidi kutanda


SAMUEL Kamau Wanjiru, milionea wa Kenya aliyeupata utajiri akiwa na umri wa miaka 20, ambapo utajiri wake umeelezwa kuchangia kifo chake akiwa na umri mdogo wa miaka 24.

Wanjiru aliyezaliwa Jumatatu, akaoa Jumatano na akafariki dunia Jumapili, historia ya mafanikio yake inatokana na kocha wa riadha wa Japan, Sunish Kubayash aliyemuona kwenye mashindano ya riadha ya shule za msingi yaliyofanyika Kisumu, Kenya, mwaka 1999.

Mauti yalimkuta akiwa nyumbani kwake na hawara, muhudumu wa baa ya jirani na nyumbani kwake iliyo umbali wa karibu kilometa moja.

Hata hivyo mazingira ya kifo chake bado ni utata, lakini hawara aliyekuwa naye hadi mwisho wa maisha yake, Jane Nduta katika maelezo yake anaamini Wanjiru hakujiua kwa kujirusha toka ghorofani.

Mama mzazi wa Wanjiru, Hanna Wanjiru kwa upande wake anaamini mwanawe ameuawa kwa makusudi, na anamtuhumu mke wa marehemu Teresia Njeri, kwamba anahusika na mauaji hayo.

Hanna anadai kulikuwa na alama za damu kwenye chumba cha mapumziko na pia damu zingine zilionekana kwenye chumba cha kulala kilichopo ghorofani.

Wanjiru amekufa akiwa na mgogoro na mkewe Teresia na aliwahi kumtumia ujumbe wa kwenye simu kumtishia kumuua, kiasi cha Teresia kuamua kufungua kesi mahakamani kulalamikia vitisho vya mumewe vya kutaka kumuua. Pia mlinzi wake wa nyumbani aliwahi kufungua kesi kumlalamikia bosi wake aliyetishia kumuua, lakini wote Teresia na mlinzi waliondoa kesi zao mahakamani.

Mwanamke mwingine anayedai ni mke wa pili wa Wanjiru ni Judy Wambui (25), aliyezaa naye mtoto wa kike, pia alisema ana ujauzito wa miezi mitano wa Wanjiru na kwamba taratibu zote za kufunga ndoa zilikuwa kwenye hatua za mwisho, na ndoa hiyo ilikuwa ifungwe kiserikali, baada ya ndoa ya kwanza na Teresia iliyofungwa kanisani.

Siku ya kifo chake, Wanjiru aliyekuwa kwenye kambi ya mazoezi katika mkoa wa Eldoret, aliondoka huko Jumapili saa tatu asubuhi akieleza anakwenda Nyahururu kutatua matatizo ya kifamilia.

Kocha wake alisema Wanjiru aliomba ruhusa kwenda Nyahururu kwa ajili ya kuonana na wakili wake kuhusiana na kesi inayomkabili ya kumiliki bunduki ya AK47 bila kibali, kesi hiyo ilipangiwa kuendelea mahakamani Jumatatu ya Mei 23.

Saa saba nchana ya siku hiyo ya Jumapili, Wanjiru aliwasili Nyahururu ambapo alikwenda kwenye mgahawa wa Jimrock ambako alikutana na mtu aliyefahamika kwa jina la George wa benki ya Barclays, aliyekuwa na ahadi naye.

Taarifa zilisema saa 4 usiku Wanjiru aliwasili kwenye mgahawa wa Water Falls ambako alikula na kupata kinywaji, kilichoelezwa kilikuwa ni kilevi hadi saa 5 usiku alipoondoka na kwenda kwenye baa ya Kawa Falls alipokutana na muhudumu Jane Nduta aliyelezwa kuwa hawara yake.

Jane akielezea mkasa mzima wa hadi kifo cha Wanjiru, alisema mwanariadha huyo alikwenda kwenye baa anayofanyakazi saa tano usiku akiwa tayari amelewa pombe, na kwamba yeye na Wanjiru ni marafiki wa siku nyingine, ambapo mwanaridha huyo mara kadhaa amekuwa akienda nyumbani kwa Jane.

Alisema ilikuwa mara yake kwanza kwenda nyumani kwa Wanjiru na alikubali baada ya kuthibitishiwa kwamba mkewe hayupo, ambapo kabla ya kwenda nyumbani, walienda kwenye mgahawa wa Jimrock ambako Wanjiru aliongeza kunywa pombe.

Jane alisema walipofika nyumbani, Wanjiru alitoka ndani ya gari na kuzungumza na mlinzi na baadaye alirejea kwenya gari, na waliingia ndani ya eno la nyumba ambapo walishuka kwenya gari na kwenda kukaa kwenye chumba cha mapumziko wakiangalia televisheni, wakati huo ilikuwa mida ya saa sita usiku.

Alisema baada ya dakika zipatazo tano ghafla aliingia mke wa Wanjiru, na alianza kumtolea maneno makali mumewe akimuhoji kuhusu yeye (Jane) akitaka kujua ni nani.

“Aliniuliza uhusiano wangu na mumewe, nikamjibu ni rafiki yangu wa karibu na tumekuwa marafiki kwa muda mrefu, nilimwambia kama si urafiki wetu nisingekuja nyumbani kwake,” alisema Jane.

Alisema Teresia aliondoka kwenye eneo hilo ambapo baada ya muda mfupi alirejea tena na kuendeleza mzozo, ambapo aliondoka tena kwa mara ya pili, ambapo aliporudi tena kwa mara ya tatu wao walikuwa wamekwisha ingia chumbani wakiwa wamekaa kitandani.

Jane alisema Teresia aliendeleza mzozo na kuchukua jagi la maji na kutishia kumpiga nalo (Jane), ambapo alijitetea kwa kumdaka mkono, wakati huo Wanjiru alikuwa kitandani kazidiwa na ulevi kiasi cha kushindwa hata kujitetea.

Kwa mujibu wa Jane, Teresia alianza kuruhsiana maneno na Wanjiru, ambapo aliamua kuchukua funguo za mlango unaoelekea kwenye ngazi za kushuka chini na kuwafungia chumbani.

Jane alisema alifungua mlango wa kwenye veranda ya chumbani iliyopo ghorofani na kuanza kumbembeleza mkewe aliyekuwa tayari chini, arudi kuwafungulia mlango. Wakati huo yeye (Jane) alikuwa bado amekaa kitandani.

Alisema ghafla alimsikia mlinzi akipiga kelele na alikwenda kwenye veranda kuangalia kulikoni, na alipomuuliza mlinzi kilichotokea, mlinzi huyo alimuonyesha kwenye sakafu ambapo alimuona Wanjiru kalala sakafuni huku akivuja damu kichwani.

Jane kwa maelezo yake haamini kama Wanjiru alijiua, anamini ni ajali iliyomkuta kwakuwa muda wote alikuwa mwenye furaha, na hakuonekana kusongwa na mawazo.

Bingwa huyo wa mbio ndefu duniani (ambaye sasa ni marehemu) alianza kuwa maarufu alipokuwa na umri wa miaka 18, ambapo katika umri huo alimuoa Teresia Njeri, aliyefanikiwa kuzaa naye watoto wawili Anne Wanjiru mwenye umri wa miaka mine na Simon Njoroge mwenye umri wa miaka miwili.

Wanjiru alimvutia Kubayash baada ya kushinda mashindano ya riadha ya shule za msingi, akikimbia akiwa hana viatu, pekupeku, ambapo alimdhamini kwenda kusoma shule ya riadha nchini Japan kwa kipindi cha miaka miwili.

Mwanariadha huyo aliyezaliwa Novemba 10, 1986 katika mji wa Nyahururu, hakuona aibu kuelezea maisha yake duni ya utotoni, ambapo aliwahi kuhojiwa na gazeti moja na kueleza kuwa katika maisha yake alianza kuvaa viatu akiwa na umri wa miaka14, na viatu vyenyewe vilikuwa ni makobazi ya plastiki.

Alisema wazazi wake walitengana akiwa na umri wa miaka mitano, na tangu wakati huo amekuwa akilelewa na mama yake akiwa mtoto kutoka kwenye familia duni iliyoshindwa hata kumnunulia viatu.

Wanjiru anasema alipomaliza shule ya msingi mwaka 2000, wakati huo akisoma shule ya msingi ya Githunguri, Olkalau, mwaka 2002 alikwenda Japan na kujiunga na shule ya riadha ya Sendai Ikuei Gakuen iliyopo Sendai.

Alimaliza shule hiyo mwaka 2005 ambapo alijiunga na timu ya riadha ya Toyota Kyushu, ambapo aliazna kuvuna mamilioni ya fedha baada ya kushinda mara tano. Ushindi uliomfanya kuwa milionea ni baada ya kuvunja rekodi katika mashindano ya Olimpiki ya Beijing, China, iliyowekwa na mwanaridha wa Ureno, miaka 44 iliyopita.

Hadi kifo chake ana hisa katika baadhi ya kampuni nchini Japan na anamiliki magari ya kifahari, Range Rover na Toyota VX na ana mali zisizo hamishika katika miji ya Nairobi na Nakuru.

Baadhi ya marafiki zake walimuelezea Wanjiru kwamba ni mtu aliyekuwa haoni shida kugawa fedha kwa marafiki zake. Ambapo alisema alilazimika kuoa akiwa na umri wa miaka 18 ili awe na mtu wa kuangalia mali zake wakati yeye anapokuwa akiendelea na masuala ya riadha.

No comments:

Post a Comment