KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 8, 2011

Banza Stone aangukia mikononi mwa Choki


WASWAHILI wana msemo unaosema: ‘Ndugu wanapogombana, chukua jembe ukalime, wakipatana chukua kapo ukavune’.
Msemo huo ulijidhihirisha mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kiongozi wa bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, Ally Choki kumwajiri hasimu wake, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ kwenye bendi yake.
Banza amejiunga na Extra Bongo akitokea bendi ya Rufita Connection, ambayo ni mwasisi wake na pia alikuwa kiongozi mkuu.
Kabla ya kujiunga na Rufita Connection, Banza alikuwa kiongozi na mwasisi wa Bambino Sound, ambayo ilikuwa ikifa na kufufuka mara kwa mara.
Mashabiki wengi wa muziki nchini wanatambua wazi kwamba, Banza na Choki walikuwa hawaivi chungu kimoja. Wamewahi kukorofishana mara kadhaa miaka ya nyuma, ikiwa ni pamoja na kutoleana lugha za kukashifiana kwenye vyombo vya habari.
Hali ya kutokuelewana kati ya wanamuziki hawa wawili ilianza kujionyesha baada ya Banza kuihama Twanga Pepeta mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kujiunga na TOT Plus.
Kabla ya Banza kuhama Twanga Pepeta, watunzi na waimbaji hao wawili nyota nchini, walidumu kwenye bendi hiyo kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuipandisha chati na kuifanya iwe tishio.
Hakuna aliyetarajia iwapo ipo siku Banza anaweza kufanyakazi akiwa chini ya Choki kwa sababu alishaanzisha na kumiliki bendi mbili tofauti. Pia aliwahi kuwa kiongozi wa bendi ya TOT Plus.
Je, ni kipi kilichosababisha Banza afungashe virago Rufita Connection na kujiunga na Extra Bongo?
Hiyo ni siri kubwa, ambayo Banza hapendi kuitoa kwenye vyombo vya habari. Lakini amekiri kuwa, hayo ni maisha ya kawaida kwa mwanamuziki. Leo yupo hapa, kesho yupo kule.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam wiki iliyopita, Banza alisema ametia saini mkataba wa mwaka mmoja wa kufanyakazi na Extra Bongo.
Kwa mujibu wa Banza, baada ya mkataba wake huo kumalizika, ataamua iwapo aendelee kuitumikia bendi hiyo au la.
Banza alisema lengo lake kubwa katika kujiunga na bendi hiyo ni kuiongezea nguvu zaidi, ikiwa pia ni njia mojawapo ya kukuza kipaji chake badala ya kukiacha kidumae.
“Kila kitu kipo sawa. Watu wategemee mambo mazuri kutoka kwangu kwani kama ilivyo kawaida yangu, siku zote sibahatishi katika anga za muziki wa dansi," alisema Banza. Mwimbaji huyo mwenye kipaji, alianza kuitumikia rasmi bendi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Hata hivyo, atatambulishwa rasmi Mei 26 mwaka huu, makao makuu ya bendi hiyo, Bamaga, Sinza mjini Dar es Salaam. Utambulisho huo umepangwa kuwa wa aina yake.
Banza alisema tayari ameshaanza kutengeneza nyimbo mbili kwa ajili ya utambulisho wake na kuongeza kuwa, zinatarajiwa kuanza kusikika hivi karibuni.
Akizungumzia ujio wa Banza katika bendi yake, Choki alisema umelenga kuiongezea nguvu zaidi bendi yake.
Choki alisema amemchukua Banza kwa sababu ya umahiri wake katika kuimba na pia kutunga nyimbo zenye mvuto. Alisema anaamini Banza atatoa mchango mkubwa katika kuipaisha bendi hiyo.
Banza alianza kujipatia umaarufu kimuziki katika bendi ya Twanga Pepeta kabla ya kuhamia TOT Plus. Pia aliwahi kuwa kiongozi wa bendi ya Twanga Chipolopolo.
Baadaye alianzisha bendi yake binafsi ya Bambino Sound, ambayo haikudumu kwa muda mrefu kabla ya kujiunga na Rufita Connection.

No comments:

Post a Comment