KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 5, 2011

Wema Sepetu atinga tena kizimbani

MREMBO wa Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu amepandishwa kizimbani kujibu shitaka la kumtukana matusi ya nguoni Raheem Rummy (Bob Junior- Rais wa Masharobaro).
Wema (26) alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni na kusomewa shitaka lake mbele ya Hakimu Mfawidhi, Mariam Masamalo.
Akisoma shitaka hilo, Karani Sharifa Dunia alidai kuwa, Aprili 11,mwaka huu, saa 12.38 jioni huko Kinondoni, Wema alimtukana Rummy.
Wema alikiri kutukana matusi hayo baada ya kuulizwa na Hakimu Mariamu kama shitaka alilosomewa ni la kweli au si kweli.
Hakimu Mariam alimuuliza Wema sababu za kutukana matusi hayo, ambapo alisema ilikuwa ni kwa sababu ya hasira.
Haki ya dhamana kwa mshitakiwa huyo ipo wazi, ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaotia saini ahadi ya sh. 300,000.
Hadi mwandishi wa gazeti hili alipoondoka mahakamani hapo, Wema alikuwa bado hajadhaminiwa. Kesi yake imeahirishwa hadi Mei 18, mwaka huu.
Hii ni mara ya tatu kwa mlimbwende huyo, ambaye pia ni msanii wa filamu za kibongo, kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali.
Alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Februari 2009 kwa kosa la kuvunja kioo cha gari la mpenzi wake wa zamani, Steven Kanumba kilichokuwa na thamani ya sh. milioni 1.5.
Hata hivyo, kesi hiyo iliyofunguliwa kwenye Mahakama ya Kinondini, ilifutwa baada ya pande zinazohusika kukubali kusuluhishwa nje ya mahakama.
Mwaka huo huo, Wema alipandishwa tena kizimbani kwa tuhuma za wizi wa televisheni na radio akishirikiana na mpenzi wake, Jumbe Mohamed. Alidaiwa kuiba vifaa hivyo nyumbani kwao.
Kesi hiyo nayo ilifutwa baada ya pande zinazohusika kukubaliana kusuluhisha suala hilo nje ya mahakama.
Mbali na kujipatia sifa kutokana na kutwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2006, Wema alianza kung’ara kwenye fani ya filamu baada ya kucheza sinema ya A Point of No Return, akishirikiana na Kanumba.
Sinema zingine alizocheza na kujipatia umaarufu ni pamoja na Fake Pastor, White Maria na A Diary, ambayo ameicheza kwa kushirikiana na Jackline Pentzel na Rose Ndauka kupitia kampuni yao ya Jerowe.


No comments:

Post a Comment