KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

HUSSEIN MACHOZI: Mambo yangu sasa safi




BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Rashid, maarufu kwa jina la Hussein Machozi, ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Mizimu.
Kibao hicho ni sehemu ya maandalizi ya ujio wa albamu ya tatu ya msanii huyo, baada ya kutesa katika albamu zake mbili za mwanzo za ‘Promise’ na ‘Kwa ajili yako’.
Akihojiwa katika kipindi cha Native Agenda cha televisheni ya TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Machozi alisema ameamua kuachia kibao hicho kwa lengo la kuwadhihirishia mashabiki kwamba bado yupo.
Machozi alisema ukimya wake wa muda mrefu uliwafanya mashabiki wengi wahoji mahali alipo na wengine kujenga hisia kamba ameishiwa kiusanii.
“Mimi bado nipo na nitaendelea kuwepo. Kuwa kimya kwa muda mrefu hakuna maana kwamba nimeishiwa. Yalikuwa maandalizi ya kuibuka na vitu vipya na mambo mapya,”alisema.
Katika kibao hicho, Machozi anasimulia kisa cha kijana msomi aliyeitwa kijijini na babu yake kwa lengo la kurithishwa mikoba ya uchawi, lakini akagoma kwa kile alichoeleza kuwa atapoteza hadhi na miaka mingi aliyosomea udaktari.
Hatimaye, baada ya kukataa kurithi mikoba hiyo, kijana huyo akaanza kutokewa na mauzauza mbalimbali, yaliyomfanya achanganyikiwe na kurukwa na akili.
Machozi, ambaye anafanyakazi zake chini ya lebo ya Respect ya Chifu Kiumbe, amewataka mashabiki wake wamvumilie kwa vile ukimya wake ulilenga kuwatayarishia vitu vya uhakika.
Msanii huyo, ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Singida alisema, anamshukuru Mungu kwamba hivi sasa maisha yanamuendea vizuri baada ya kuishi kwa dhiki kwa miaka kadhaa.
“Kwa kweli namshukuru sana Mungu kwani baada ya kuishi maisha ya dhiki, sasa naweza kuishi vizuri mimi na mama yangu, pesa ya kula na kununua hiki na kile hainipigi chenga,”alisema.
Machozi alikanusha madai kuwa, ametengana na promota wake wa zamani, Kid Boy, ambaye ndiye aliyemtoa kimuziki. Alisema hana tatizo lolote na Kid na kwamba bado wanaendelea kufanyakazi pamoja.
Alisema aliamua kuachana na Kid na kufanyakazi peke yake baada ya kujiona amekua na anastahili kujitegemea kwa kila kitu yeye mwenyewe.
“Nilitengana naye kwa sababu mtoto anapokua, anataka ajitegemee. Lakini hadi sasa bado namtegemea sana, anaendelea kunipa ushauri juu ya mambo mbalimbali. Naweza kusema hakuna mtu anayenifahamu vizuri zaidi ya Kid Boy,” alisema.
Machozi alisema kabla ya kujitosa katika fani ya muziki, alikuwa akicheza mpira na kiwango chake kilikuwa cha juu, lakini alilazimika kuachana na mchezo huo baada ya kuona hakuna maendeleo.
Alisema kutokuwepo kwa ufuatiliaji wa vipaji vya vijana na kuwaendeleza ni miongoni mwa sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kufifia kwa vipaji vya vijana wengi chipukizi, hasa waliopo vijijini.
Msanii huyo alianza kujihusisha na muziki tangu akiwa mdogo kwa kutunga na kuimba nyimbo za kaswida alipokuwa madrasa.
Alianza kung’ara kimuziki mwaka 2008 baada ya kurekodi wimbo wake wa kwanza, unaokwenda kwa jina la ‘Kafia ghatto’. Baadaye aliibuka na kibao cha ‘Full Shangwe’, alichomshirikisha Ambwene Yesaya ‘AY’.
Nyimbo hizo pamoja na ‘Maji yakimwagika’, ‘Niambie’ na zinginezo, zinapatikana katika albamu yake ya kwanza, aliyoitoa mwaka huo, inayojulikana kwa jina la ‘Promise’.
Baadaye, Machozi aliibuka na albamu yake ya pili, inayokwenda kwa jina la ‘Kwa ajili yako’, aliyoirekodi kwenye studio za Tetemesha zilizopo mjini Mwanza.
Machozi pia amewahi kushirikishwa katika kibao cha ‘Nimekosa nini’ cha msanii mwingine nyota wa muziki huo, H. Baba. Msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1986 wilaya ya Manyoni mkoani Singida, bado hajaoa.

No comments:

Post a Comment