KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 12, 2011

Birmingham yaafiki kukipiga na Simba, Yanga

Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage (kulia) akimkabidhi vipeperushi mbalimbali vinavyoonyesha Utalii wa Tanzania, Kocha Msaidizi wa timu ya Barningham City ya Uingereza, Andy Watson wakati walipokutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO Jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kuzungumzia ujio wa timu hiyo nchini. ( Picha na Mwanakombo Jumaa wa MAELEZO)



UONGOZI wa klabu ya Birmingham City ya England, umekubali kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu za Simba na Yanga.
Uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kukubali kucheza mechi hizo, umekuja baada ya kuridhishwa na ubora wa Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam na hospitali ya Agakhan.
Mabingwa hao wa Kombe la Carling wamesema, kikosi chao kitatua nchini mwanzoni mwa mwezi Julai kwa ajili ya mechi hizo, ambazo watazitumia kujiandaa kwa michuano ya Ligi ya Ulaya na Ligi Kuu ya England.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mjini Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Andly Watson alisema wameridhishwa na mazingira ya Tanzania pamoja na masharti waliyotoa kwa uongozi wa Simba.
Alisema kikosi chake kinatarajiwa kuja nchini na nyota wake wote na kwamba kitaanza kucheza mechi yake ya kwanza Julai 12 dhidi ya Simba kabla ya kuvaana na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Yanga, Julai 14, mwaka huu.
Andly alisema katika msafara huo, timu yake inatarajiwa kuongozana na mashabiki wapatao 1,000 na baada ya kucheza michezo hizo, watatembelea mbuga mbalimbali za wanyama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage alisema, maandalizi kwa ajili ya mechi hizo za kirafiki yamekamilika na kwamba wao kama Simba, wamejiandaa kikamilifu.
Rage alisema baada ya Birmingham kucheza michezo hiyo, wachezaji na viongozi wake watapata fursa ya kutembelea vivutio vya kitalii kama vile mbuga za wanyama za Serengeti na Mikumi.
Alisema ujio wa timu hiyo nchini, utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa sababu utasaidia kutangaza vivutio vya kitalii katika nchi za Ulaya na kwingineko duniani.

No comments:

Post a Comment