KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 18, 2011

CHIOMA: Fani ya filamu inalipa Nigeria


LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI nyota wa kike wa filamu nchini Nigeria, Chioma Akpotha amekiri kuwa, kazi hiyo inalipa na imemwezesha kupata vitu vingi, ambavyo hakuvitarajia katika maisha yake.
Chioma aliueleza mtandao wa Nigeriafilms wiki hii kuwa, kwa sasa anaweza kuishi maisha ya kutanua, ambayo huko nyuma hakuweza kuyamudu na pia amepata tuzo na zawadi nyingi.
“Nimepata tuzo nyingi kiasi kwamba ziwezi kuzitaja moja moja. Licha ya kuwa mwigizaji, ninafanya mambo mengi, ambayo sipendi kuyataja,”alisema.
Mwanadada huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, pamoja na Nigeria kupiga hatua kubwa kimaendeleo katika fani hiyo, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ili kuiboresha zaidi.
Alisema licha ya nchi hiyo kushika nafasi ya tatu duniani kwa utengenezaji wa filamu nyingi, wanahitajika kuwa makini zaidi hasa katika masuala ya kiufundi.
Alilitaja tatizo lingine kubwa linaloikumba fani hiyo kuwa ni wizi wa kazi za sanaa. Alisema licha ya kuwepo kwa sheria ya hakimiliki, bado haijaweza kufanyakazi yake sawa sawa katika kupambana na wahalifu hao.
Chioma alisema hadi sasa hajaweza kutengeneza filamu yake mwenyewe, lakini yupo katika mchakato huo na kwamba hivi karibuni huenda mambo yakawa safi.
Alipoulizwa ni kwa nini amekuwa akipewa nafasi nzuri pekee katika uigizaji wa filamu za Nollywood, Chioma alisema huo ni uamuzi wa watayarishaji wa filamu.
“Sielewi kwa nini napewa nafasi nyingi za aina hiyo, lakini nafikiri ni kwa sababu ndizo ninazozimudu zaidi. Katika fani hii, waongozaji filamu wanapogundua wewe ni mzuri katika nafasi fulani, wanakupatia hiyo hiyo,”alisema.
“Nitakupa mfano. Mkongwe Patience Ozorkwor, ambaye alianza kucheza filamu kwa kupewa nafasi za kawaida na kufanya vizuri, lakini alipojaribiwa katika nafasi ya mama mkwe mwenye roho mbaya, ameendelea nayo kwa sababu alifanya vizuri zaidi,”aliongeza.
Chioma alisema tangu alipojitosa kwenye fani hiyo mwaka 1998, amekuwa akivutiwa na Kate Henshaw-Nuttall, aliyempa moyo wa kujiunga nayo pamoja na wacheza filamu, Joke Silva na Ramsey Nouah.
Mwigizaji huyo, ambaye ameolewa na kuzaa mtoto mmoja alisema, fani hiyo haijaathiri maisha ya familia yake kwa vile anao muda wa kutosha kuihudumua.
“Huwa ninahakikisha kuwa, naihudumia familia yangu kwanza kabla ya kwenda kazini, hasa kama ni nje ya mji. Kama ambavyo siku zote nimekuwa nikisema, mimi natoka familia ya kikristo,”alisema.
Vilevile alisema fani hiyo imemwezesha kuteuliwa kuwa balozi wa Afrika katika kampuni ya mawasiliano ya Globacom na pia kutwaa tuzo mbalimbali. Miongoni mwa tuzo hizo ni ule ya mwigizaji bora wa kike wa mwaka 2007.
Jambo pekee, ambalo Chioma halipendi katika maisha yake ni wizi. Alisema anachukia wizi na kamwe hawezi kukutwa akiiba kitu chochote.

No comments:

Post a Comment