KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 5, 2011

Wawili wapigwa stop Kombe la Taifa

WACHEZAJI Nurdin Mponda wa mkoa wa Temeke na Kudura Maguta wa mkoa wa Kinondoni wamezuiwa kuzichezea timu hizo katika mashindano ya Kombe la Taifa, yanayotarajiwa kuanza keshokutwa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wachezaji hao wamezuiwa kushiriki kwenye mashindano hayo kufuatia usajili wao kukiuka kanuni namba 33.
Kwa mujibu wa Wambura, Mponda msimu huu aliichezea Villa Squad ya Kinondoni hivyo hana sifa ya kuichezea Temeke wakati Maguta aliichezea Moro United ya Ilala hivyo hana sifa ya kuichezea Kinondoni.
Wambura alisema kanuni za mashindano hayo zinataka wachezaji wa madaraja mengine, kuichezea mikoa ambayo timu zao zimesajiliwa na si vinginevyo.
Ofisa huyo alisema pia kuwa, kwa mujibu wa kanuni namba 42 ya michuano hiyo, makocha wakuu wa timu za mikoa wanatakiwa kuwa na cheti cha ngazi pevu wakati wasaidizi wao wanatakiwa kuwa na cheti cha ngazi ya kati.
Michuano ya Kombe la Taifa, imepangwa kuchezwa katika vituo sita tofauti. Vituo hivyo ni Lindi, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mwanza na Tabora. Hatua ya robo fainali hadi fainali itachezwa kituo cha Arusha.
Wakati huo huo, michuano ya soka ya ligi ya taifa, inayowashirikisha mabingwa wa mikoa, imepangwa kuanza Juni 11 mwaka huu katika vituo vya Kigoma, Mbeya, Pwani na Singida.
Wambura alisema jana kuwa, usajili wa wachezaji kwa ajili ya michuano hiyo umepangwa kuanza Mei 10 hadi 25 mwaka huu wakati pingamizi zitawekwa kuanzia Mei 26 hadi Juni 3.
Usajili wa timu hizo utapitishwa Juni 4 na kwamba ada ya ushiriki kwa kila timu ni sh. 70,000 na ada ya kadi ya kila mchezaji ni sh. 6,000.
Mikoa, ambayo imewasilisha rasmi TFF mabingwa wao ni Dodoma (Majengo FC), Kigoma (Kasulu United), Kilimanjaro (Lang’ata Bora FC), Morogoro (Tumbaku) na Mwanza (Geita Veterans).
TFF imeiagiza mikoa, ambayo haijawasilisha majina ya mabingwa wao, kufanya hivyo haraka na kwamba iwapo itashindwa kufanya hivyo, ligi itaanza bila timu zao kuwemo.

No comments:

Post a Comment