KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 12, 2011

Azam yaanika bunduki zake

UONGOZI wa Azam umetangaza kikosi cha wachezaji 21, ambacho hadi sasa wamesajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Taarifa iliyotolewa na tovuti ya klabu hiyo jana imeeleza kuwa, kwa sasa klabu hiyo imebakisha nafasi tatu za kusajili, ambazo ni beki wa kati na mshambuliaji kutoka nje na beki mwingine wa kati wa hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, beki wa kati na mshambuliaji kutoka nje, watasajiliwa kutoka nchini Ghana. Hata hivyo, tovuti hiyo haikutaja majina ya wachezaji hao.
Hivi karibuni, Azam ilifanikiwa kumsajili mshambuliaji Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast, ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Tusker Chalenji iliyofanyika mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Kusajiliwa kwa mchezaji huyo kumeifanya Azam iwe imesajili wachezaji wa kigeni watatu hadi sasa. Wengine ni nahodha Ibrahim Shikanda, aliyebakishwa kwenye usajili na kipa wa zamani wa Yanga, Obren Circovic kutoka Serbia.
Azam imesema katika usajili wake wa msimu ujao, imeamua kusajili wachezaji wapya saba na kuwaongezea mikataba wachezaji wa zamani 14.
Wachezaji wengine wapya ni kipa Mwadini Ali Mwadini na waziri Salum Omar kutoka Mafunzo ya Zanzibar, Ghulam Abdallah kutoka Chuoni Zanzibar, kiungo Abdulhalim Humud kutoka Simba,Zahor Pazi kutoka African Lyon, Said Murad kutoka Kagera Sugar na Khamis Mcha Vuai kutoka Ocean View ya Zanzibar.
Katika usajili wake huo, Azam pia imempandisha daraja kipa Daudi Mwasongwe na kuendelea kuwapa nafasi wachezaji chipukizi,Himid Mao, Salum Abubakar na Jamal Mnyate.
Wachezaji wengine walioendelea kufunga pingu na Azam kwa ajili ya msimu ujao ni mabeki Aggrey Moris, Malika Ndeule, Lackson Kakolaki na Erasto Nyoni. Viungo ni Ramadhani Chombo, Ibrahim Mwaipopo, Seleman Selembe, Kalimangonga Ongala, Jabir Azizi na Mrisho Ngassa wakati mshambuliaji pekee aliyebakishwa ni John Bocco.

No comments:

Post a Comment