KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 12, 2011

Ngasa hauzwi ng'o-Azam


UONGOZI wa klabu ya soka ya Azam FC umeweka wazi kuwa, hauna mpango wowote wa kumuuza mshambuliaji Mrisho Ngasa kwa klabu ya Yanga.
Msimamo huo ulielezwa jana na Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrisa alipokuwa akizungumza na Burudani kuhusu maombi ya Yanga kutaka kumsajili mchezaji huyo.
Nassor alisema kwa sasa, hawatarajii kuuza mchezaji yeyote kwa sababu wamepania kutengeneza kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
“Tumeamua kwamba, hatutaki kuuza mchezaji yoyote katika kipindi hiki na Ngasa ni miongoni mwa wachezaji waliomo kwenye mipango yetu ya baadaye na tunaamini mchango wake bado unahitajika,”alisema Nassor.
Katibu Mkuu huyo wa Azam alisema, wameshaiandikia barua Yanga kuijulisha kuhusu uamuzi wao huo na kusisitiza kuwa, sera ya klabu yake ni kuuza wachezaji wao nje ya nchi.
“Tunaposema sera yetu ni kuuza wachezaji wetu nje, maana yake ni kwamba tunataka kupata pesa za kununua wachezaji chipukizi, ambao wataweza kuisaidia timu yetu na nchi kwa jumla,”alisema.
Nassor alisema wameshangazwa na hatua ya viongozi wa Yanga kukutana kwanza na mchezaji huyo na kuzungumza naye kabla ya kufanya hivyo kwa viongozi wa Azam kama kanuni za usajili zinavyosema.
"Ngasa ana mkataba na Azam FC wa miaka mitatu, kamwe hatupo tayari kuona taratibu zinavunjwa kwa mchezaji wetu kukutana au kuzungumza na timu yoyote bila ridhaa yetu,"alisema kiongozi huyo.
Msimamo huo wa Azam umekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kuripoti kuwa, mchezaji huyo amekubali kurejea Yanga.
Hata hivyo, Ngasa aliwataka viongozi wa Yanga kufanya mazungumzo kwanza na uongozi wa Azam ili waweze kufikia makubaliano.
Ngasa alisajiliwa na Azam msimu uliopita kwa dau la sh milioni 58 na ameisaidia timu hiyo kumaliza michuano ya ligi kuu msimu huu ikiwa nafasi ya tatu na pia kuibuka mfungaji bora.

No comments:

Post a Comment