KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, May 25, 2011

K-One atambulisha moja mpya

MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Karim Othman amedhihirisha kuwa ni moto wa kuotea mbali baada ya kuanza kung’ara katika kibao chake kipya cha Yule.
Karim, maarufu zaidi kwa jina la K-One, amerekodi kibao hicho kwa kushirikiana na msanii nyota wa kike wa muziki huo, Maunda Zorro.
Kibao cha Yule, ambacho kimepigwa katika miondoko ya zouk, kimeshaanza kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni pamoja na kupigwa kwenye vituo vya radio nchini.
K-One amerekodi kibao hicho katika studio za Baucha zilizopo Magomeni, Dar es Salaam wakati picha za video zimepigwa na kampuni ya 01 Video chini ya Dk. Tonee.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, K-One alisema ameamua kutoa kibao hicho kwa ajili ya maandalizi ya ujio wa albamu yake ya kwanza.
“Huu ni utambulisho wangu tu kwa mashabiki kabla ya kuzindua albamu yangu ya kwanza,”alisema msanii huyo, ambaye pia hushiriki kuonyesha mavazi.
K-One alisema baada ya kibao cha ‘Yule’, anatarajia kukitambulisha kibao chake cha pili kinachojulikana kwa jina la ‘Ngoja niseme’, alichokirekodi kwa kushirikiana na msanii mkongwe, Chege Chigunda.
Msanii huyo machachari alisema, anatarajia kuzindua albamu yake ya kwanza mwezi ujao, ikiwa na vibao vinane, alivyovirekodi kwa kushirikiana na wasanii mbalimbali wakongwe.
Mbali na ‘Yule’ na ‘Ngoja niseme’, alivitaja vibao vyake vingine, vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Dhahabu’ alichomshirikisha Ali Kiba na ‘Niwaambie’ alichorekodi na Madee.
Vibao vingine ni ‘Muelewe’ alichomshirikisha Tundaman, ‘Bora’ alichorekodi na Top C, ‘Weekend Special’ alichomshirikisha Baker na ‘Sina hakika’ alichorekodi peke yake.
“Namshukuru Mungu kwamba kibao changu cha kwanza hadi sasa kimepokewa vizuri, nasubiri kuona mambo yatakuwaje katika kibao changu cha pili na baada ya hapo ndipo nitafanya uzinduzi wa albamu yangu,”alisema.
Kwa mujibu wa K-One, iwapo mashabiki watampokea vizuri kwenye gamu, uzinduzi wa albamu hiyo utafanyika mapema mwezi ujao.
Amemshukuru Mkurugenzi wa Studio za Baucha Records, Ally Baucha kwa kukubali atumie nembo yake.

No comments:

Post a Comment