KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 26, 2011

Simba yakata rufani nyingine


UONGOZI wa klabu ya Simba umesema utakata rufani nyingine kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kupinga kupambanishwa na Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya klabu bingwa Afrika.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha michezo cha Radio One.
Rage alisema, wameamua kuwasilisha rufani hiyo CAF kwa vile baadhi ya vifungu vya kanuni za mashindano hayo, vinaonyesha kuwa walipaswa kuingizwa moja kwa moja kwenye hatua ya nane bora.
Kikosi cha Simba kikiwa na wachezaji 18 na viongozi kadhaa, kilitarajiwa kuondoka mjini Dar es Salaam jana usiku kwa ndege kwenda Misri kwa ajili ya mechi hiyo.
Simba na Wydad Casablanca zinatarajiwa kuteremka dimbani keshokutwa mjini Cairo katika mechi itakayoamua timu itakayofuzu kucheza hatua hiyo katika kundi B.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, kikanuni hawakupaswa kucheza na Wydad Casablanca katika mechi hiyo kwa vile Wamorocco hao walishatolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
"Hawa Wydad walishatolewa na TP Mazembe, na sisi tuliwakatia rufani TP Mazembe na kushinda, kwa hiyo tulitakiwa kucheza hatua hiyo. Nikifika tu Cairo, nitakwenda makao makuu ya CAF, tutacheza 'under protest' ili lengo letu lifanikiwe,"alisema kiongozi huyo.
Rage alisema safari yake ya kwenda makao makuu ya CAF itakuwa na lengo la kutaka kupata ufafanuazi ili kujua wanachopaswa kufanya iwapo kanuni zitakuwa zimekiukwa.
Akizungumzia mchezo wa keshokutwa, Rage alisema kikosi chao kipo fiti na kusisitiza kuwa, wamejipanga vyema kukabiliana na mbinu zote wanazoweza kufanyiwa na wapinzani wao ndani na nje ya uwanja.
Rage alisema wamewapa wachezaji wao mafunzo maalumu ya kisaikolojia ili kuhakikisha wanacheza mpira wa kiwango cha juu na kukwepa jazba.
Iwapo Simba itafanikiwa kuitoa Wydad Casablanca, itapangwa kundi B pamoja na timu za Al Ahly ya Misri, MC Algers ya Algeria na Esperance ya Tunisia.

No comments:

Post a Comment