KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 5, 2011

Pongezi TASWA kwa kuboresha tuzo za wanamichezo bora

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), kesho kinatarajiwa kutoa tuzo kwa wanamichezo bora wa michezo mbalimbali waliofanya vizuri katika msimu wa 2009/2010.
Katika tuzo hizo, TASWA imepanga kumzawadia gari lenye thamani ya sh. milioni 13, mshindi wa jumla wa tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka pamoja na cheti.
Mbali na tuzo hiyo kwa mshindi wa jumla, TASWA pia imepanga kutoa sh. milioni moja kwa mwanamichezo bora wa kila mchezo pamoja na cheti. Jumla ya tuzo zitakazotolewa ni 18.
Uamuzi wa chama hicho kuboresha tuzo zake kwa wanamichezo bora wa mwaka unastahili kupongezwa, hasa ikizingatiwa kuwa, utasaidia kuwapa hamasa zaidi wanamichezo mbalimbali ya kufanya vizuri katika michezo wanayoshiriki.
Kabla ya kuziboresha tuzo hizo, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, TASWA ilikuwa ikiteua mwanamichezo bora wa kila mwezi na kisha kuwashindanisha ili kupata mwanamichezo bora wa mwaka.
Lakini kuanzia mwaka huu, chama hicho kimeamua kuwasiliana na vyama vyote vya michezo nchini ili kupata majina ya wanamichezo bora watatu wa mwaka pamoja na sifa zao kwa ajili ya kupigiwa kura na jopo maalumu la waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ili kumpata mshindi.
Tayari TASWA imeshatangaza majina ya wanamichezo bora watatu wa kila mchezo, waliopendekezwa na vyama hivyo na ambao ndiyo watakaopigiwa kura na kamati hiyo ili kumpata mwanamichezo bora. Upigaji huo wa kura utafanyika kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na kamati hiyo.
Tuzo zitakazoshindaniwa mwaka huu ni za michezo ya riadha, wavu, netiboli, karate, kikapu, soka, ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, baiskeli, kriketi, gofu, tennis, judo na tuzo za mwanamichezo bora chipukizi, mwanamichezo bora wa nje anayecheza nchini, mwanamichezo bora wa Tanzania anayecheze nje na tuzo ya heshima.
Vigezo vitakavyotumika kupata washindi ni pamoja na mchango wa mchezaji katika kufanikisha ushindi wa timu yake kitaifa na kimataifa, nidhamu bora ya mchezaji ndani na nje ya uwanja, uhusiano mzuri wa mchezaji na jamii, kipaji chake, mvuto na uhamasishaji wake kwa jamii.
Tuonavyo, maboresho yaliyofanywa na TASWA yamelenga kwenda na wakati na pia kuzifanya tuzo hizo ziwe na mvuto na heshima zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa, wanamichezo wanapaswa kuthaminiwa, kuheshimiwa na kuwa mfano bora wa kuigwa na jamii.
Tunaipongeza Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa uamuzi wake wa kutumia sh. milioni 80 kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo. Tunatoa mwito kwa kampuni zingine kujitokeza kwa wingi kudhamini tuzo hizo kwa vile michezo ni sehemu nzuri ya kujitangaza kibiashara.
Tunawaomba wadau wote wa michezo nchini kuiunga mkono TASWA katika utoaji wa tuzo hizo badala ya kuishushia lawama katika uteuzi wa wanamichezo bora. Cha msingi kwa wadau hao ni kutoa maoni yenye lengo la kuziboresha zaidi badala ya kushutumu pekee.

No comments:

Post a Comment