KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 8, 2011

MWANAIDI: Sikutarajia kushinda tuzo ya mwanamichezo bora 2010

MWANAIDI Hassan akiwa ndani ya gari alilozawadiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) baada ya kuibuka mshindi wa tuzo ya mwanamichezo bora wa 2010.

MAKAMU wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal (kushoto) akimkabidhi funguo za gari mwanamichezo bora wa mwaka 2010, Mwanaidi Hassan katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye hoteli ya Movenpick mjini Dar es Salaam.


MCHEZA netiboli Mwanaidi Hassan wa JKT mwishoni mwa wiki iliyopita alifanikiwa kushinda tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka 2010 wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA).
Mwanaidi alishinda tuzo hiyo kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata katika timu yake ya JKT, timu ya mkoa wa Temeke na timu ya taifa.
Mbali na kuiwezesha JKT kutwaa ubingwa wa ligi daraja la kwanza Tanzania Bara na pia mkoa wa Temeke kutwaa Kombe la Taifa, Mwanaidi pia aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.
Dada huyo mrefu, ambaye hajaolewa wala kuzaa mtoto, pia aling’ara katika mashindano ya kimataifa yaliyofanyika Singapore akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa baada ya kuibuka kuwa mmoja wa wafungaji bora.
Mwanaidi pia aliisaidia timu hiyo kufuzu kucheza fainali za dunia za netiboli na pia kubuka mfungaji bora wa mashindano ya Afrika yaliyofanyika Afrika Kusini.
Kwa kushinda tuzo hiyo, Mwanaidi alizawadiwa gari aina ya Toyota Cresta GX 100 lenye thamani ya sh. milioni 13, lililotolewa na wadhamini wa tuzo hizo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL). Pia alizawadiwa pesa taslim sh. milioni moja pamoja na cheti kwa kuibuka mwanamichezo bora wa netiboli.
Akizungumza na Uhuru mara baada ya kushinda tuzo hiyo, Mwanaidi alisema alijisikia furaha kubwa baada ya kutangazwa mshindi kwa vile hakuitarajia.
Mwanaidi alisema pamoja na kushinda tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka 2009, iliyotolewa mwaka jana, hakuwa na matarajio makubwa iwapo angeweza kuibuka tena kidedea mwaka huu.
“Nadhani kujituma kwangu uwanjani na nidhamu yangu ndani na nje ya uwanja ndivyo vilivyoniwezesha kushinda tuzo hiyo,”alisema mwanadada huyo mrefu na mwenye umbo jembamba kama waliyonayo washiriki wa mashindano ya urembo.
Mwanaidi alisema mbali na yeye binafsi kufurahishwa na tuzo hiyo, wazazi wake na viongozi wa timu ya JKT nao wamempongeza na kuonyesha kwamba wapo pamoja naye.
Alisema ushindi wake huo si tu kwamba ulimfurahisha yeye binafsi, bali hata timu yake ya JKT, ambayo imezidi kutambulika ndani na nje ya nchi.
Mwanaidi alisema tuzo za mwaka huu zina tofauti kubwa na za miaka iliyopita kutokana na kuboreshwa zaidi na pia kutolewa kwa zawadi ya gari kwa mshindi na pesa taslim sh. milioni moja kwa mwanamichezo bora wa kila mchezo.
Aliipongeza TASWA kwa kuziboresha zaidi tuzo hizo na pia Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kuongeza zawadi kwa washindi. Alizitaka kampuni zingine zaidi zijitokeze kuboresha tuzo hizo.
Amewataka wanamichezo wenzake walioshinda tuzo mbalimbali, wasibweteke, badala yake waongeze bidii zaidi ili waweze kufanya vizuri.
Pia amewataka wadau wa michezo na waandishi wa habari za michezo nchini, kuondokana na dhana kwamba mchezo wa soka ndio bora zaidi na unaostahili kutoa tuzo ya mwanamichezo bora.
Alisema Tanzania imekuwa ikipata sifa kubwa kimataifa kutokana na michezo mingine kama vile netiboli, gofu na kriketi, lakini kwa vile haipewi kupaumbele na vyombo vya habari, wadau wengi hawautambui ukweli huo.
“Michezo sio soka pekee, yote ni sawa. Ipo michezo mingine mingi, ambayo wanamichezo wetu wamekuwa wakifanya vizuri, lakini hawafahamiki,”alisema.
Mwanaidi alisema Watanzania wengi wamezoea kuona tuzo za muziki za Kilimanjaro, lakini kutokana na maboresho yaliyofanywa na TASWA, wanamichezo wamepata sehemu yao ya kujifariji na kutambulika.
Mwanadada huyo alisema hana mpango wa kuliuza gari alilozawadiwa ili apate pesa kwa sababu pesa zinatafutwa. Alisema atalitumia gari hilo kutembelea.
“Siwezi kabisa kuliuza. Nikifanya hivyo, hata walionizawadiwa wataniona sina akili,”alisema.
Kwa sasa Mwanaidi hajaolewa wala hana mtoto. Aliongeza kuwa, hana mpango wa kuolewa ama kuzaa kwa wakati huu kwa sababu bado malengo yake katika mchezo wa netiboli hayajatimia.
Alisema matarajio aliyonayo katika mchezo huo ni kufika mbali zaidi kuliko alipo sasa ili kuwapa changamoto wanamichezo chipukizi kuonyesha vipaji vyao.

No comments:

Post a Comment