KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 2, 2011

Fatma Dogodogo wa TOT afariki dunia



MSANII nyota wa taarab wa kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), Fatma Ali Salim, maarufu kwa jina la Fatma Dodogodo amefariki dunia.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa TOT, John Komba imesema, Fatma alifariki dunia jana saa nane mchana katika hospitali ya Mwananyamala, mjini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Fatma alilazwa kwenye hospitali hiyo tangu wiki iliyopita kutokana na kusumbuliwa na kansa ya kizazi.
Fatma alijiunga na TOT mwaka 1998 akitokea kikundi cha sanaa za maonyesho cha Wizara ya Utamaduni ya Zanzibar.
Katika uhai wake, Fatma akiwa na TOT alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na uimbaji wake mahiri wa nyimbo mbalimbali za taarab.
Mwimbaji huyo alizaliwa Juni 11, 1962 katika wilaya ya Mjini Magharibi mjini Unguja. Ameacha mtoto mmoja na wajukuu watatu.
Komba alisema kifo cha Fatma kimeacha pengo kubwa katika kikundi cha TOT kwa vile alikuwa mchapakazi mahiri na asiyekuwa na majivuno.
Mazishi ya Fatma yanatarajiwa kufanyika leo saa saba mchana kwenye makaburi ya Mwananyamala kwa Kopa.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.

No comments:

Post a Comment