KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 18, 2010

FERGUSON: Nilimsajili Bebe bila kumuona


LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amefichua kuwa, Bebe ni mchezaji wa kwanza kwake kumsajili bila hata kumuona akicheza kwenye televisheni.
Ferguson alimsajili Bebe (20) wiki iliyopita kutoka klabu ya Vitoria de Guimaraes ya Ureno. Usajili wake uliigharimu Manchester United pauni milioni 7.4 za Uingereza.
Usajili wa Bebe umewashtua mashabiki wengi wa soka wa England, hasa ikizingatiwa kuwa, alidumu na klabu ya Vitoria kwa wiki tano.
Kabla ya kujiunga na Vitoria, mshambuliaji huyo chipukizi alikuwa akiichezea klabu ya daraja la tatu ya Estrela da Amadora.
Ferguson hakuwahi kupata nafasi ya kumuona Bebe akicheza kupitia DVD, lakini alimtuma Mtendaji Mkuu wa Manchester United, David Gill kwenda Ureno kukamilisha usajili wa mchezaji huyo.
“Sikuwahi kumuona kwenye video, ni mara ya kwanza. Kwa kawaida, kama ilivyokuwa kwa Javie (Hernandez) na Chris (Smalling), niliona video zao kadhaa kabla ya kuwasajili,”alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 68.
“Baadhi ya wakati unapaswa kuwaamini wafanyakazi wako na wafuatiliaji wetu wa vipaji nchini Ureno walitushauri tufanye haraka kumsajili,”aliongeza. “Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa klabu zingine na ni hapo unapaswa kufanya maamuzi ya haraka katika maisha yako na sijisikii vibaya kuhusu hilo. Pia nilizungumza na Carlos Queiroz (msaidizi wake wa zamani) kuhusu Bebe,” alisema Ferguson.
Naye Bebe alisema ana hakika atamvutia kocha huyo kwa sababu ana uwezo mkubwa uwanjani ikiwa ni pamoja na kuwa na kasi, kupiga mashuti na kufunga mabao.
Mbali na Manchester United, Bebe pia alikuwa akiwaniwa na klabu za Real Madrid ya Hispania na Benfica ya Ureno kabla ya kuzidiwa kete na Ferguson.
Wakati Manchester United ikimsajili Bebe, mahasimu wao Manchester City walifanikiwa kuwanyakua wachezaji Mario Balotelli kutoka AC Milan ya Italia na James Milner wa Aston Villa.
Ferguson ameuponda usajili wa Manchestet City kwa madai kuwa wamiliki wake wamekuwa wakitumia fedha nyingi kusajili wachezaji kiholela.
Wamiliki wa Manchester United walikaririwa hivi karibuni wakisema kuwa, bado Ferguson analo fungu la kutosha kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya. Usajili wa Bebe umeifanya klabu hiyo hadi sasa iwe imetumia pauni milioni 25 kusajili wachezaji wapya msimu huu.
Ferguson pia alitumia kiasi kidogo cha pesa kusajili wachezaji wapya msimu uliopita baada ya kumuuza Cristiano Ronaldo kwa pauni milioni 80 kwa klabu ya Real Madrid.


Santos yamwekea ngumu Neymar kuhamia Chelsea

KLABU ya Santos ya Brazil imemuomba mshambuliaji wake nyota, Robinho de Souza kumshawishi mchezaji mwenzake, Neymar afute mpango wake wa kujiunga na Chelsea ya England.
Mbali na Robinho, klabu hiyo pia imemuomba mwanasoka nyota wa zamani wa nchi hiyo, Pele na Waziri wa Michezo wa Brazil, Orlando Silva kuingilia kati suala la mchezaji huyo.
Tayari Kocha Mkuu wa sasa wa timu ya taifa ya Brazil, Mano Menezes na kocha wa zamani wa timu hiyo, Mario Zagallo wameshamtahadharisha chipukizi huyo na kumtaka abaki nchini humo. Mchezaji huyo mwenye kipaji ameonekana kuchanganyikiwa kuhusu mustakabali wake, kufuatia vyombo kadhaa vya habari kuripoti kuhusu uhamisho wake.
Akizungumza na vyombo vya habari juzi, kuhusu ushauri aliopewa na Zagallo na Menezes, Neymar alisema hadi sasa haelewi iwapo atabaki nchini humo ama ataondoka.
“Kuna mambo mengi ambayo bado hayajawa wazi. Lakini siwezi kuondoka nikaenda mahali na kusugua benchi. Bila shaka nitautafakari kwa makini ushauri wa Mano na Zagallo. Inawezekana ni mapema mno kuondoka,”alisema.
Maneno yake hayo yameipa matumaini makubwa klabu ya Santos, ambayo viongozi wake wamepanga kukutana na baba wa mchezaji huyo pamoja na wakala wake, Wagner Ribeiro.
Kuna habari kwamba, Santos inataka kumuongezea mkataba Neymar ili aendelee kubaki kwenye klabu hiyo. Mkataba wa sasa wa Neymar unatarajiwa kumalizika mwaka 2014.
Chelsea ilitenga kitita cha pauni milioni 17 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo, lakini Santos ilizitolea nje pesa hizo. Kufuatia kukataliwa kwa ofa hiyo, Chelsea imeongeza dau na kufika pauni milioni 25.
Santos, ambayo imetishia kuishtaki Chelsea kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), imesisitiza kuwa haiwezi kumuuza mchezaji huyo chini ya pauni milioni 30, ambacho ni kiwango chake cha kuvunja mkataba.
Zagallo alikaririwa wiki hii akisema Neymar hayuko fiti kuweza kukabili mikikimikiki ya ligi kuu ya England, ambako ni wachezaji wachache kutoka Brazil wanaocheza nchini humo.
“Nafikiri ni mapema kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 17, 18 au 19 kuondoka Brazil,”alisema Zagallo, ambaye alishinda Kombe la Dunia akiwa na mchezaji wa Brazil mwaka 1958 na 1962 na akiwa kocha mwaka 1970.
“Ni wazi kwamba sikuzote pesa ndicho kishawishi kikubwa kwa wachezaji kutaka kuondoka, lakini kwa suala la Neymar, atakwenda katika mazingira, ambayo si mazuri mwili wake. Anahitajika kuongeza uzito, hivyo ni bora aondoke akiwa na umri wa miaka 21 au 22,”aliongeza.
Menezes, ambaye alimwita Neymar kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Brazil, ilipoibwaga Marekani mabao 2-0 wiki iliyopita, aliunga mkono maoni ya Zagallo.

No comments:

Post a Comment