BRASILIA, Brazil
MSHAMBULIAJI nyota na chipukizi wa klabu ya Santos ya Brazil, Neymar da Silva ameitolea nje ofa aliyopewa na klabu ya Chelsea ya England.
Chelsea ilikuwa imejiandaa kuilipa Santos ada ya uhamisho ya pauni milioni 25 za Uingereza, kumpatia mchezaji huyo mkataba wa miaka mitano na malipo ya mshahara wa pauni 55,000 kwa wiki.
Badala yake, Neymar ameamua kuongeza mkataba wa kuichezea klabu yake ya Santos wenye marupurupu mengi zaidi kuliko ule wa awali.
Licha ya shinikizo kutoka kwa familia yake na washauri wake kumtaka ahame, Neymar aliona ilikuwa ni mapema sana kuondoka Brazil na alipatwa na mshtuko kuhusu ofa mpya aliyopewa na Santos.
Santos imemuongezea mshahara Neymar mara tatu zaidi na kufikia pauni 40,000 kwa wiki kutokana na malipo ya udhamini kama ilivyofanya kwa Robinho de Souza, aliyerejea kwenye klabu hiyo kwa mkopo akitokea Manchester City ya England.
Mwanasoka nyota wa zamani wa dunia, Pele, Robinho na Kocha mpya wa timu ya taifa ya Brazil, Mano Menezes kwa nyakati tofauti walimshauri Neymar abaki katika klabu hiyo.
Kadhalika, kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Mario Zagallo alimtahadharisha chipukizi huyo na kumtaka abaki nchini humo. Zagallo alikaririwa wiki iliyopita akisema kuwa, Neymar hayuko fiti kuweza kukabili mikikimikiki ya ligi kuu ya England, ambako ni wachezaji wachache kutoka Brazil wanaocheza nchini humo.
“Nafikiri ni mapema kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 17, 18 au 19 kuondoka Brazil,”alisema Zagallo, ambaye alishinda Kombe la Dunia akiwa na mchezaji wa Brazil mwaka 1958 na 1962 na akiwa kocha mwaka 1970.
“Ni wazi kwamba sikuzote pesa ndicho kishawishi kikubwa kwa wachezaji kutaka kuondoka, lakini kwa suala la Neymar, atakwenda katika mazingira, ambayo si mazuri kwa mwili wake. Anahitajika kuongeza uzito, hivyo ni bora aondoke akiwa na umri wa miaka 21 au 22,”aliongeza.
Menezes, ambaye alimwita Neymar kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Brazil, ilipoibwaga Marekani mabao 2-0 wiki iliyopita, aliunga mkono maoni ya Zagallo.
Kufuatia kauli zilizotolewa na wanamichezo mbalimbali, Neymar alisema: “Nimeupokea na kuutafakari kwa makini ushauri niliopewa, lakini uamuzi wa kubaki kwenye klabu ni wa kwangu.”
“Ilikuwa kazi ngumu, lakini nafikiri kwamba Mungu alinipa busara kuamua kipi kilichokuwa bora. Nina furaha kubwa kuwepo hapa na sasa nafikiria kuhusu kushinda mataji zaidi na Santos,” aliongeza.
“Pesa haziwezi kununua furaha yako na nina furaha kuwepo hapa,” alisema mwanasoka huyo, anayeshabihishwa kiuchezaji na mwanasoka nyota wa zamani wa nchi hiyo, Pele.
Santos imeamua kumuongezea mkataba Neymar ili awemo kwenye kikosi hicho hadi baada ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zinazotarajiwa kufanyika nchini Brazil.
Hata hivyo, wawakilishi wa mwanasoka huyo wameitaka Chelsea kutokukata tamaa kabisa na kuwasilisha maombi mengine ya kumsajili msimu ujao baada ya Santos kumaliza michuano ya Kombe la Libertadores, ambalo haijawahi kulitwaa tangu mwaka 1963.
Baba wa mwanasoka huyo alisema: “Sisi pamoja na rais, tumeamua kuahirisha safari ya kwenda Ulaya ili kumruhusu akue na kuendelea zaidi kisoka hapa.”
Uongozi wa Santos ulimwahidi mchezaji huyo na washauri wake kwamba, si tu utamuongezea mshahara, bali pia utamwajiri ofisa uhusiano kwa ajili ya kumuongezea uelewa wake juu ya mambo mbalimbali, hasa yanayohusu masoko katika nchi za Uingereza, Hispania na Italia.
Klabu hiyo ina ndoto za kumfanya Neymar awe mchezaji wa kwanza katika kizazi cha sasa kutambulika kama mwanasoka bora wa dunia wakati akiendelea kucheza soka nchini Brazil.
Santos pia imeahidi kufanya hivyo kwa mchezaji Paulo Henrique Ganso (20), ambaye kiu yake kubwa ni kujiunga na klabu za Manchester United, Real Madrid na Lyon.
Uamuzi wa Santos kumuongezea mkataba Neymar ni pigo kubwa kwa Chelsea, ambayo imekuwa ikimuwinda kinda huyo kwa miaka miwili iliyopita huku ikijipa matumaini ya kumnyakua baada ya kukutana na baba yake mjini New York mapema mwezi huu.
Kwa sasa, inasubiriwa kuona iwapo Santos itaendelea na tishio lake la kuishtaki Chelsea kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kwa kitendo chake cha kumsumbua mchezaji huyo, japokuwa klabu hiyo ya England inaamini haijavunja sheria.
Neymar alizaliwa Februari 5, 1992 mjini Mogi das Cruzes nchini Brazil. Alijiunga na Santos Machi 7, 2009 na kuichezea kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17, ilipoibwaga Oeste mabao 2-1.
Aliichezea timu hiyo kwa mara ya pili wiki iliyofuata na kuifungia bao lake la kwanza katika mechi dhidi ya Mogi Mirim. Ni mchezaji anayefikiwa kuwa wa aina yake kutokea katika bara la Amerika ya Kusini.
Pele na mwanasoka mwingine nyota wa zamani wa nchi hiyo, Romario walimshinikiza Kocha Dunga amjumuishe kwenye kikosi cha Brazil kilichocheza fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini, lakini kocha huyo aligoma.
Hata hivyo, baada ya fainali hizo kumalizika, kocha mpya wa timu hiyo, Menezes aliamua kumjumuisha kwenye kikosi chake kilichocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Marekani na kuibuka na ushindi, akiwa amevaa jezi namba 11. Alifunga bao moja kati ya mawili, alipounganisha kwa kichwa krosi ya Andre Santos. Brazil ilishinda mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment