KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 19, 2010

Makocha wazawa, wageni nani zaidi?





WAKATI michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara inatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii, vita kali inatarajiwa kuibuka kati ya makocha wazawa na wale wa kigeni.
Kuibuka kwa vita hiyo kunatokana na makocha takriban wa timu zote 12 zitakazoshiriki ligi hiyo, kila mmoja kujigamba kwamba timu yake itafanya vizuri na kuibuka na ubingwa.
Tambo za makocha hao zimekuja, kufuatia usajili uliofanywa na kila timu pamoja na maandalizi yaliyofanywa na makocha wanaozifundisha, ambapo makocha wazawa wamepania kukata ngebe za wageni.
PATRICK PHIRI-SIMBANi kocha aliyeiwezesha Simba kupata mafanikio makubwa msimu uliopita, baada ya kutwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika na pia bila kufungwa mechi hata moja.
Phiri pia amekuwa gumzo kubwa kwa mashabiki wa soka nchini kutokana na staili yake ya ufundishaji na pia uwezo wake wa kubadili mchezo uwanjani kadri mchezo unavyoendelea.
Kama ilivyo kawaida yake, kocha huyo raia wa Zambia aliwapa wasiwasi mkubwa viongozi na mashabiki wa Simba baada ya kuchelewa kurejea nchini kutoka mapumziko kwa kisingizio cha matatizo ya kifamilia.
Katika msimu huu, Phiri ataongezewa nguvu na makocha watatu, akiwemo Syllersaid Mziray, Selemani Matola na Amri Said, ambaye alikuwa msaidizi wake msimu uliopita. Pia yupo kocha mpya wa makipa, Haroun Amour kutoka Oman.
Kikosi cha Simba msimu huu kinajivunia wachezaji wake wapya, Amir Maftah, Abdulrahim Humud, Shija Mkina, Rashid Gumbo, Gilla Joshua, Patrick Ochan, Kelvin Chale na Mbwana Samatta.
Katika kikosi hicho, wamo wachezaji watano wa kigeni walioichezea msimu uliopita. Wachezaji hao ni Joseph Owino, Hillary Echesa, Jerry Santo na Emmanuel Okwi.
Wachezaji wengine wa Simba wanaotarajiwa kuonekana katika ligi hiyo msimu huu ni Juma Kaseja, Ali Mustapha, Ramadhan Shamte, Salum Kanoni,Amir Maftah,Kelvin Yondan, Juma Nyoso,David Naftali na Mohamed Banka.
Wengine ni Nico Nyagawa,Uhuru Seleman, Amri Kiemba, Mussa Hassan 'Mgosi',Mohamed Kijuso,Kelvin Chale na Juma Jabu.
Akizungumzia ligi hiyo, Phiri alisema lengo lake ni kuendeleza rekodi ya msimu uliopita ya kushinda mechi zote na kutwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika.
Phiri alisema licha ya kuchelewa kuripoti kambini, hana wasiwasi na kikosi chake kwa vile hakina mabadiliko makubwa na kina uwezo mkubwa wa kutetea taji lake.
KOSTADIN PAPIC-YangaNi kocha aliyeanza kuinoa Yanga msimu uliopita, akichukua nafasi ya Dusan Kondic, aliyefungasha virago baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika.
Papic amelieleza gazeti la Burudani kuwa, ana hakika kikosi chake kilichosheheni nyota watatu kutoka Ghana, kina uwezo mkubwa wa kulirejesha taji la ligi hiyo kutoka kwa mahasimu wao Simba.
Kocha huyo kutoka Serbia alisema, ameshazifanyiakazi dosari zote zilizojitokeza kwenye kikosi chake msimu uliopita, hivyo hawatarajii kurudia makosa.
Katika kikosi cha Yanga msimu huu, wamo wachezaji watatu wapya kutoka Ghana, Isaac Boakye, Ernest Boakye na Kenneth Asamoah, ambaye ndiye tegemeo kubwa kwa ufungaji wa magoli. Pia yumo kipa Ivan Knezevic kutoka Serbia.
Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa na Yanga msimu huu ni Salum Telela, Stephen Mwasita, Abuu Ubwa Zuberi, Chacha Marwa, Nsa Job, Yahya Tumbo na Sunday Seme.
Mbali na sura hizo mpya, kikosi hicho pia kitakuwa na wachezaji walioichezea msimu uliopita. Wachezaji hao ni Yaw Berko kutoka Ghana, Nelson Kimathi,Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mohamed Mbegu, Nurdin Bakari, Geofrey Bonny, Kigi Makasi, Abdi Kassim, Shamte Ally, Jerry Tegete, Iddi Mbaga, Razack Khalfan na Fred Mbuna.
ITAMAR AMORIM-AZAM
Kocha huyo kutoka Brazil ameendelea kukiimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji nyota kadhaa wapya na hivyo kukifanya kiwe tishio na pia kutabiriwa kutwaa ubingwa.
Miongoni mwa nyota hao wapya ni pamoja na mshambuliaji Mrisho Ngasa kutoka Yanga, kiungo Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na mshambuliaji Jabir Azizi kutoka Simba. Itamar alisema wiki hii kuwa, wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya ligi hiyo, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki kwa lengo la kupima uwezo wa wachezaji wake.
Alisema mechi hizo zimemwezesha kupata kikosi cha kwanza, ambacho ana hakika kina uwezo mkubwa wa kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Kocha huyo wa zamani wa viungo wa timu ya taifa, Taifa Stars alisema, kikosi chake kimeimarika zaidi msimu huu kuliko msimu uliopita na ametoa onyo kwa vigogo Simba na Yanga kujiandaa kupata upinzani mkali.
Wachezaji waliosajiliwa na Azam kwa ajili ya msimu huu wa ligi ni pamoja Aggrey Morris, Ally Manzi, Daudi Mwasongwe, Erasto Nyoni,Faraj Hussein, Ibrahim Mwaipopo, Ibrahim Shikanda, Jackson Chove na Jamal Mnyate.
Wengine ni John Bocco,Kally Ongala, Luckson Kakolaki, Malika Mdeule, Mau Ally, Mohammed Binslum, Patrick Mafisango, Salum Swedi, Sami Haji ,Tumba Swedi na kipa Vladmir Niyonkuru kutoka Burundi.
Licha ya hayo,kocha huyo ameeleza kuwa ana imani kubwa kikosi chake kitakuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kuongeza nguvu katika sehemu zote ambazo msimu uliopita zilikuwa na matatizo na kuwaomba waamuzi kuchezesha kwa haki.
FRED FELIX MINZIRO-JKT RUVUKocha Fred Felix Minziro ametamba kuwa, kikosi chake kimefanya maandalizi kabambe kwa ajili ya ligi hiyo na kina uwezo wa kuwa kiboko ya vigogo vya soka nchini, Simba na Yanga.
Minziro amesema cheche za timu hiyo zimeshaanza kuonekana katika mechi kadhaa za kirafiki walizocheza, ambapo alitamba wachezaji wake walionyesha uwezo wa juu.
JKT Ruvu inaundwa na wachezaji wengi chipukizi, ambao baadhi yao ni waajiriwa wa Jeshi la Kujenga Taifa na wengine ni raia wa kawaida.
Minziro amesajili kikosi cha timu hiyo kupitia usaili alioufanya kwa wachezaji waliojitokeza kwenye mazoezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa jeshi uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
“Kikosi changu kimesheheni wachezaji wengi wenye umri mdogo, lakini kitakuwa moto wa kuotea mbali kwenye ligi. Nawatahadharisha wapinzani wetu, hasa Simba na Yanga wajiandae kupata vipigo,”alitamba.
Minziro alisema lengo lake ni kuwaonyesha makocha wa kigeni kwamba, hata makocha wazawa nao wana uwezo wa kuonyesha maajabu katika ligi hiyo. TOM OLABA- MTIBWANi kocha aliyekabidhiwa jukumu la kuinoa Mtibwa Sugar baada ya Salum Mayanga kupangiwa majukumu mengine kwenye kiwanda cha Sukari cha Mtibwa kilichopo Turiani mjini Morogoro.
Olaba, ambaye ni raia wa Kenya, aliwahi kuifundisha Mtibwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 kabla ya kuondoka na kwenda Zanzibar, ambako alikuwa kocha mkuu wa Miembeni.
Mratibu wa Mtibwa, Jamal Bayser amesema wameamua kumrejesha kocha huyo kwa lengo la kuiongezea nguvu zaidi timu hiyo. Alisema licha ya kuchelewa kuanza kazi, ana hakika Olaba ana uwezo wa kuifikisha mbali timu hiyo.
Olaba atakuwa akisaidiwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Mecky Maxime, ambaye kwa sasa ndiye aliyeachiwa jukumu la kuinoa Mtibwa baada ya Mayanja kurejea kiwandani.
Tumaini kubwa la Mtibwa katika ligi hiyo msimu huu litakuwa kwa washambuliaji wake wapya, Thomas Maurice, Yona Ndabila, Boban Zilintusa.
Makocha Jackson Mayanja wa Kagera Sugar, Peter Mhina wa Majimaji, John Simkoko wa Polisi Dodoma, Choki Abeid wa Toto African, Dan Koroso wa AFC na Charles Kilinda wa JKT Ruvu nao kila mmoja amejigamba kuwa timu yake itafanya vizuri msimu huu.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, makocha hao walisema, wamefanya maandalizi ya kutosha na kilichobaki ni ligi hiyo kuanza kutimua vumbi.
Makocha hao walisema hakuna anayependa kuiona timu yake iishuka daraja, hivyo watapigana kufa na kupona ili kuhakikisha wanabaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Wametoa tahadhari kwa waamuzi waliopangwa kuchezesha ligi hiyo, kuepuka kuzipendelea timu kubwa, badala yake waheshimu na kuzingatia sheria zote 17 za soka ili washindi wapatikane kutokana na uwezo wao.
000000
RATIBA YA MECHI ZA UFUNGUZI LIGI KUU TANZANIA BARA
TAREHE MECHI UWANJA MKOA
Agosti 21, 2010 Lyon vs Simba Uhuru Dar
Polisi Dom vs Yanga Jamhuri Dodoma AFC vs Azam S. Abeid Arusha Majimaji vs Mtibwa Majimaji Ruvuma Toto vs Ruvu S CCM Kirumba Mwanza Kagera vs JKT Ruvu Kaitaba Kagera


No comments:

Post a Comment