KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 18, 2010

Lyon yaigeuka Simba

KLABU ya African Lyon imesema itawazuia wachezaji wake, Mbwana Samatta na Rashid Gumbo kuichezea Simba msimu huu kwa vile klabu hiyo haijakamilisha taratibu za kuwahamisha.
Mmoja wa viongozi wa Lyon, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini alisema jana kuwa, hawatambui iwapo wachezaji hao wamesajiliwa na Simba.
Kiongozi huyo alisema, wanachotambua ni kwamba Gumbo na Samatta bado ni wachezaji halali wa Lyon hadi hapo Simba itakapofuata taratibu katika kuwasajili.
Aliongeza kuwa, uongozi wa Simba umetangaza kuwasajili wachezaji hao kinyemela bila kufuata taratibu za uhamisho zilizowekwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Gumbo na Samatta kila mmoja ana mkataba wa kuichezea Lyon kwa miaka mitatu na mikataba yao imesajiliwa na inatambuliwa na TFF.
“Tutawazuia wachezaji hao kuichezea Simba katika michuano ya ligi kuu, inayotarajiwa kuanza Jumamosihadi taratibu za usajili zitakapofuatwa,”alisema.
Simba na Lyon zimepangwa kukata utepe wa michuano ya ligi hiyo msimu huu katika mechi itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Simba,Godfrey Nyange ‘Kaburu’ alisema waliwasajili wachezaji hao kwa kufuata taratibu zote ndio sababu wameidhinishwa na TFF.
Kaburu alisema madai hayo yaliyotolewa na Lyon hayana msingi na kuongeza kuwa, yamelenga kuuchafua uongozi wa Simba.
Naye Ofisa Habari wa TFF, Florian Kaijage alisema masuala yote yanayohusu ligi na usajili wa wachezaji, yatatolewa ufafanuzi leo wakati wa kikao cha kamati ya utendaji ya shirikisho hilo.
Kaijage alisema kikao hicho pia kitajadili ajira ya katibu mkuu wa shirikisho hilo ili kujaza nafasi ya Fredrick Mwakalebela, aliyemaliza mkataba wake.

No comments:

Post a Comment