KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 26, 2010

BINTI WA MEXICO ASHINDA TAJI LA MISS UNIVERSE 2010


Hellen Dausen

LAS VEGAS, Marekani
MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la Miss Universe 2010, Hellen Dausen juzi alishindwa kung’ara baada ya kutolewa hatua ya awali.
Katika shindano hilo lililofanyika mjini hapa, mrembo Jimena Navarrete (22) wa Mexico aliibuka mshindi baada ya kuwabwaga washiriki wengine 82 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Mshindi wa pili alikuwa Yendi Phillipps kutoka Jamaica wakati nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Jesinta Campbell kutoka Australia.
Hellen amekuwa mrembo wa nne kutoka Tanzania kushiriki kwenye mashindano hayo na kutolewa hatua za awali. Wa kwanza alikuwa Flaviana Matata mwaka 2007, aliyefuatiwa na Amanda Ole Sululu 2008 na Illuminata Mize mwaka jana.
Jimena alivikwa taji na mshindi wa shindano hilo mwaka jana, Stefania Fernandez wa Venezuela. Amekuwa mrembo wa pili kutoka Mexico kushinda taji hilo tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 1952. Wa kwanza alikuwa Lupita Jones, aliyeshinda taji hilo mwaka 1991.
Mara baada ya kuvikwa taji hilo, Jimena aliweka wazi mipango yake kuhusu kuitangaza Mexico kimataifa.
“Nataka dunia nzima kuifahamu nchi yangu na watu wangu,”alisema Jimena, ambaye asili yake ni Guadalajara.
“Nahisi kwamba watu wote wa Mexico kwa sasa wamepatwa na wazimu kwa furaha,” alisema binti huyo kupitia mkalimani. “Naona fahari na nina hakika nao wanaona fahari kubwa kwa ushindi wangu.”
Mrembo huyo aliyekuwa amevalia gauni refu jekundu lililomfiti vyema mwilini, alipiga picha kadhaa akiwa ameshika bendera ya Mexico kabla ya kupiga picha na mrembo wa kwanza wa nchi hiyo kutwaa taji hilo.
Akizungumzia ushindi huo, Rais wa Mexico, Felipe Calderon alisema ni faraja kubwa kwa watu wa nchi hiyo na utasaidia kuitangaza vyema kimataifa.
“Tumeshinda, idumu Mexico!” Aliandika Jimena kupitia mtandao wa Facebook, ambapo watu 218 walitoa maoni yao kuhusu ushindi wake.
Katika shindano hilo, Jimena na washiriki wenzake walipanda jukwaani wakiwa wamevaa nguo za kitaifa. Baadaye walicheza muziki wakiwa wamevaa nguo za rangi ya fedha zilizonakshiwa kwa rangi nyeusi kabla ya kutangazwa washiriki 15 walioingia fainali.
Washiriki hao 15 walipita jukwaani wakiwa wamevaa nguo za kuogelea huku kundi la muziki la Cirque du Soleil likipiga nyimbo kadhaa za mkongwe Elvis Presley, kikiwemo ‘Viva Las Vegas’.
Kwa ushindi huo, Jimena atakuwa akilipwa mshahara kila mwezi, atapewa nyumba ya kuishi mjini New York, ofa ya masomo ya mwaka mmoja katika shule ya uigizaji sinema na vitu vingine mbalimbali vya thamani.

No comments:

Post a Comment