'
Thursday, August 12, 2010
Stars, Harambee hakuna mbabe
Na Deusdedit Undole
TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars jana ilishindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Kenya, Harambee Stars.
Katika mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Harambee ilijipatia bao hilo la pekee kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake nyota, MacDonald Mariga kabla ya Stars kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Mrisho Ngasa.
Mariga, anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Inter Milan ya Italia, aliifungia Harambee bao la kuongoza dakika ya 14 kwa shuti la mpira wa adhabu, nje kidogo ya eneo la hatari.
Mwamuzi Oden Mbaga wa Tanzania aliamuru ipigwe adhabu hiyo baada ya beki Kelvin Yondani wa Stars kumwangusha Dennis Oliech katika eneo hilo.
Harambee ililianza pambano hilo kwa kasi na nusura ipate bao dakika ya 11 wakati Mariga allipofumua shuti kali nje kidogo ya eneo la hatari, lakini lilipanguliwa na kipa Shabani Kado wa Stars na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.
Katika dakika za mwanzo za mechi hiyo, Harambee Stars ililisakama mara kwa mara lango la Stars, hasa washambuliaji wake, Oliech na Mariga, ambao walikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Tanzania.
Stars ingeweza kufunga bao dakika ya 39 wakati Mussa Hassan ‘Mgosi’ alipopewa pasi na Uhuru Selemani akiwa ndani ya 18,lakini shuti lake lilipaa juu ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko Harambee ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Bao la kusawazisha la Stars lilifungwa na Mrisho Ngasa dakika ya 57 baada ya mabeki wa Harambee kuzembea kumkaba wakidhani ameotea.
Oliech angeweza kuiongezea bao Harambee dakika ya 66, lakini shuti lake lilipanguliwa kifundi na kipa Kado wa Stars na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.
Mgosi itabidi aijutie nafasi aliyoipata dakika ya 75 baada ya kupewa pasi safi na Ngasa na kubaki ana kwa ana na kipa Obungu wa Harambee, lakini shuti lake lilitoka nje.
Stars: Shabani Kado, Idrisa Rajabu/ Stephano Mwasika, Shadrack Nsajigwa, Kelvin Yondani/ Aggrey Morris, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Abdi Kassim,Abdulrahim Humud, Jabir Azizi/Athumani Iddi, Uhuru Selemani/Selemani Kassim, Jerry Tegete/Mussa Hassan, Mrisho Ngasa.
Harambee: Wilson Obungu, Julius Owino, George Owino, Lloyd Wahome, Edgar Ochieng, Patrick Ooko/ Paul Welle, MacDonald Mariga, George Odhiambo/Anthony Kimani, Dennis Oliech, John Barasa/Allan Wanga, Kelvin Omondi/ James Stuma.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment