'
Wednesday, August 18, 2010
MWASITI: Sikutegemea kufika hapa nilipo
MSANII nyota wa kike wa muziki wa bongo fleva nchini, Mwasiti Almasi amekiri kuwa, kibao chake cha kwanza cha ‘Nalivua pendo’ndicho kilichompandisha chati na kumpatia umaarufu mkubwa kimuziki.
Akihojiwa katika kipindi cha televisheni cha Mambo Yoyo cha ITV mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwasiti alisema kibao hicho kimetungwa na mtayarishaji maarufu wa muziki nchini, aliyemtaja kwa jina la Abuu.
Mwasiti alisema alitunga kibao hicho tangu mwaka 2007, lakini alifanikiwa kukirekodi mwaka jana baada ya mashairi yake kupitiwa na kuandikwa upya na Abuu.
Alisema mtayarishaji huyo wa muziki, ambaye hapendi kujulikana kwa watu wengi, amekuwa akimpatia msaada mkubwa katika kuandika na kuhariri maishairi ya nyimbo zake.
Mwasiti alisema baada ya kibao hicho kuanza kutamba kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini, hakuamini masikio yake kwa vile hakuwa na matumaini hayo.
“Wanawake wengi walikuwa wakinipigia simu kunipongeza wakisema, ‘afadhali umewaeleza ukweli watu wenye tabia hiyo’,” alisema mwasiti.
Kufuatia kutamba kwa kibao hicho, Mwasiti alisema alianza kupata mialiko mingi ya kutumbuiza kwenye hafla mbalimbali ikiwa ni pamoja na safari ya kimuziki nchini Ethiopia.
Alisema alikwenda katika nchi hiyo akiwa na wasanii Joseph Haule ‘Profesa Jay’ na Richard kutoka kundi la Tanzania House of Talent (THT) kwa ajili ya kushiriki kwenye kongamano la tano la maendeleo ya Afrika lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa.
Kabla ya kwenda Ethiopia, Mwasiti alisema yeye na wasanii wenzake hao watatu walitunga na kurekodi kibao kimoja cha ‘Songa mbele’, ambacho walikiimba kwa lugha ya Kiswahili na Kimasai.
Mbali na Abuu, amemtaja mtu mwingine, ambaye amekuwa akimsaidia kupitia mashairi yake, kuyarekebisha na kumpa ushauri kuwa ni mama yake mzazi.
“Wakati niliporekodi kibao cha ‘Nalivua pendo’, mama hakuamini kama mashairi yale ni ya kwangu. Aliniambia haiwezekani Mwasiti, huyu siye wewe,”alisema Mwasiti.
Mwasiti alisema wakati mwingine mama yake amekuwa akimshauri kupunguza makali ya maneno katika mashairi yake kila alipoyaona mazito ama yana mwelekeo usiovutia.
Alivitaja vibao vingine vilivyompandisha chati kuwa ni ‘Niambie’, ‘Yelele Mama’ na ‘Daima milele’, ambavyo alivirekodi akiwa katika kundi la Tanzania House of Talent (THT).
Alimtaja msanii Judith Wambura ‘Lady JayDee’ kuwa ndiye aliyemvutia na kumfanya ajitose katika fani hiyo kabla ya kurekodi naye kibao chake cha pili.
Alisema licha ya JayDee kuwa msanii maarufu na nyota nchini, anapenda kuwasaidia wasanii wanaochipukia na kuwapa misaada ya aina mbalimbali ili wapate mafanikio.
“Namkubali sana JayDee. Amenisaidia sana. Hana maringo na ana moyo wa kupenda kuwasaidia wasanii wengine,”alisema.
Mwasiti hajawahi kupokea tuzo yoyote ya muziki hapa nchini, lakini aliwahi kupata tuzo ya mwanamuziki bora wa kike wa Tanzania iliyotolewa mwaka jana nchini Kenya.
Alisema kushindwa kwake kupata tuzo hapa nchini hakumkatishi tamaa kwa vile anaamini yeye ni mmoja wa wasanii wanaokubalika kwa mashabiki, lakini bado hajapata bahati hiyo.
Alisema wasanii wote waliowahi kushinda tuzo za muziki hapa nchini ni wazuri kutokana na muziki wao, japokuwa washindi wa tuzo hizo hujulikana mapema.
Mbali na kufanya vizuri hapa nchini, Mwasiti amewahi kupanda jukwaani na baadhi ya wanamuziki nyota wa Afrika kama vile Angelique Kidjo wa Benin na Zola wa Afrika Kusini.
Mwasiti alimemshukuru Mungu kutokana na mafanikio aliyoyapata hadi sasa kwa vile wapo wasanii wengi wa muziki huo, ambao bado hawajapata njia ya kutokea hadi sasa.
”Nimepata nafasi ya kufanya mahojiano na kituo Cha televisheni cha Afrika Kusini cha Chanel O na video ya wimbo wangu wa ”Niambie’ imeonekana kukubalika na wengi,” anasema binti huyo.
Tayari Mwasiti amesharekodi vibao vinane kwa ajili ya albamu yake binafsi, itakayojulikana kwa jina la ‘Niambie’. Alisema albamu hiyo inaandaliwa chini ya usimamizi wa kundi la THT.
Amewataka wasanii zaidi wenye vipaji na nia ya kweli ya kuutumia muziki kama mwelekeo halisi wa maisha yao, kujitokeza kwa wingi na kujiunga na kundi la THT kwa sababu si mahala pa kupotezea muda, bali ni kazi mtindo mmoja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment