HOMA ya pambano la watani wa jadi wa soka Simba na Yanga imeenza kupanda baada ya timu hizo kwenda kujichimbia kambini Bagamoyo mkoani Pwani na katika visiwa vya Zanzibar.
Simba na Yanga zinatarajiwa kupambana Aprili 18 mwaka huu katika mechi maalumu ya kuwania Ngao ya Hisani, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi hiyo ni maalumu kwa ufunguzi wa ligi kuu ya Vodacom.
Habari kutoka ndani ya klabu hizo zimeeleza kuwa, Simba iliondoka mjini Dar es Salam juzi kwenda kuweka kambi Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo wakati Yanga imekwenda kujichimbia Bagamoyo.
Mbali na kulikimbia jiji, viongozi wa klabu hizo wamekuwa wakiwatuma ‘mashushu’ wao kwenda kuwachunguza wachezaji wao waliopo kwenye kambi ya kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars iliyopo kwenye hoteli ya F & J Annex mjini Dar es Salaam.
Kazi ya mashushu hao ni kuchunguza mienendo ya wachezaji na kutoa taarifa kwa uongozi, hasa zinazohusu tuhuma za kupokea rushwa kutoka upande wa upinzani.
Viongozi wa klabu hizo wamekuwa na wasiwasi kwamba, upande mwingine unaweza kwenda kuwarubuni wachezaji wao ili wacheze chini ya kiwango katika mechi hiyo.
Uchunguzi huo pia ulikuwa ukifanywa na mashushu hao kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyokuwa yakifanyika aidha kwenye uwanja wa Karume na Uhuru, Dar es Salaam.
Viongozi wa klabu hizo wamepanga kuwachukua wachezaji wao mara baada ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Taifa Stars na Kenya, iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Uhuru.
Wachezaji wa Yanga waliopo kwenye kikosi cha Taifa Stars ni Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nurdin Bakari, Athumani Idd,Kigi Makasi, Abdi Kassim, Jerryson Tegete na Nadir Haroub Canavaro.
Wachezaji wa Simba waliomo kwenye timu hiyo ni Juma Kaseja, Salum Kanoni, Abdulrahim Humud, Uhuru Seleman, Mussa Hassan 'Mgosi’, Kelvin Yondani na Juma Jabu.
No comments:
Post a Comment