MWENYEKITI wa Yanga, Lloyd Nchunga (kushoto) akipokea baadhi ya hati na nyaraka mbalimbali za klabu hiyo kutoka kwa mwenyekiti wa zamani, Iman Madega wakati wa makabidhiano yaliyofanyika jana makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege).
MWENYEKITI wa zamani wa klabu ya Yanga, Imani Madega ameukabidhi uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Llyord Nchunga akaunti nne za klabu hiyo zenye jumla ya sh. milioni 199.7.
Mbali na kiasi hicho cha fedha, Madega pia amemkabidhi Nchunga mabasi matatu, nyaraka mbalimbali za klabu na daftari lenye jumla ya majina ya wanachama 7,000 wa Yanga.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana mchana makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako. Katika makabidhiano hayo, Madega pia alimpatia Nchunga hati za majengo mawili ya klabu hiyo, hati za mabasi matatu, likiwemo moja aina ya Mitsubishi, ambalo linadaiwa sh. 500,000.
Yanga inazo akaunti nne katika benki ya CRDB tawi la Vijana. Akaunti hizo ni kwa ajili ya usajili wa wachezaji, mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi na akaunti ya klabu.
Moja ya akaunti hizo inazo sh. milioni 197,869, nyingine inazo sh. milioni moja, nyingine inazo sh. 795,629 wakati akaunti ya klabu haina pesa.
Madega pia alimkabidhi Nchunga nyaraka zinazohusu madeni ya klabu hiyo, likiwemo deni la sh. milioni 6.6 la hoteli ya Tamal, deni la sh. milioni 10 la Kampuni ya All Sports, deni la sh. milioni 5.6 la hoteli ya Valley View na deni la dola 30,000 za Marekani, ambalo Yanga inadaiwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Yanga inadaiwa kiasi hicho kikubwa cha fedha na CECAFA kufuatia kugomea pambano lake la kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya Kombe la Kagame dhidi ya Simba mwaka 2008.
Akizungumza katika hafla hiyo, Madega alimpongeza Nchunga na viongozi wenzake wapya kwa kushinda katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Julai 18 mwaka huu.
Alisema nyenzo alizomkabidhi Nchunga ni kwa ajili ya kazi za Yanga hivyo anapaswa kuzitunza na kuzifanyiakazi kama alivyofanya yeye na viongozi wenzake waliopita.
Madega alisema wakati uongozi wake ulipoingia madarakani mwaka juzi, alikabidhiwa katiba na kitabu chenye orodha ya wanachama 800, lakini sasa idadi hiyo imeongezeka na kufika 7,000.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga alimshukuru mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yussuf Manji kwa kuisaidia kwa hali na mali. Pia aliishukuru Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Kampuni ya African Medical Clinic. Alitamba kuwa, chini ya uongozi wake, Yanga iliweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili pamoja na Kombe la Tusker, hivyo alimtaka Nchunga ahakikishe wanafuata nyayo zao ili kuijengea heshima klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment