MWANAMUZIKI wa zamani wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra, Hussein Jumbe amesema kamwe hawezi kuidharau na kuidhihaki bendi hiyo kwa sababu ndiyo iliyomfikisha alipo sasa.
Akizungumza mjini Dar es Salaam hivi karibuni, Jumbe alisema alipata umaarufu na ujanja wa kimuziki akiwa Mlimani Park, maarufu kwa jina la Sikinde, hivyo anaiheshimu pamoja na kuwaheshimu wanamuziki wake.
Jumbe alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa habari hii kuhusu uamuzi wake wa kufanya maonyesho ya pamoja na bendi hiyo hivi karibuni.
Mwimbaji huyo mwenye sauti maridhawa, ambaye kwa sasa anamiliki bendi yake ya Talent, alishiriki kwenye maonyesho mawili ya Sikinde yaliyofanyika kabla ya kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Katika maonyesho hayo, Jumbe alitia fora na kuwa kivutio kwa mashabiki baada ya kupewa nafasi ya kuimba vibao vya ‘Adha ya chumba kimoja’, ‘Nipeni pole’, ‘Kijakazi’, ‘Naomi,’ ‘Mwanangu Isaya,’ ‘Nachechenea’ na ‘Kumbuka fadhila’.
“Sikinde ni nyumbani kwangu, ndiko nilikojifundishia ujanja na ndiyo iliyonifikisha hapa nilipo, ndiyo iliyonilea, hivyo sija ujanja kwa Sikinde,”alisema mwanamuziki huyo, ambaye pia aliwahi kuimbia bendi ya Msondo Ngoma.
“Kuna watu waliotaka kunigombanisha na wanamuziki wenzake kama vile Shabani Dede na Hassan Bitchuka, lakini ukweli ni kwamba sina matatizo nao, nawaheshimu na wao wananiheshimu,” aliongeza.
Jumbe alisema ataendelea kushirikiana na bendi hiyo kila itakapomuihitaji kwa vile bado anaipenda na anaweza kurudi wakati wowote.
Kwa upande wake, Dede alisema Jumbe ni mwanamuziki mwenzao na kwamba hawana matatizo naye kwa sababu Sikinde ni nyumbani kwake.
Dede alisema kamwe Jumbe hakuwahi kutimuliwa katika bendi hiyo kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti hivi karibuni, bali alitoka mwenyewe kwenda kutafuta maisha Msondo Ngoma.
“Ndio maana unaona leo tuko pamoja naye na tutaendelea kuwa naye wakati wa maonyesho ya sikukuu ya Iddi,”alisema.
No comments:
Post a Comment