'
Thursday, August 26, 2010
Kikwete aahidi makubwa kwa wasanii wa Bongo
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuinua maisha ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya na wacheza filamu nchini ili waweze kunufaika na vipaji vyao.
Kikwete alitoa ahadi hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa na kuhudhuriwa na maelfu ya watu.
Mgombea huyo urais kwa tiketi ya CCM alisema, angependa kuona katika kipindi chake cha uongozi, wasanii wa muziki na filamu nchini wanafanana kimaisha na wasanii maarufu duniani.
“Ningependa kuona huko mbele wasanii wa muziki wa kisasa wanafanana kimaisha na akina Madonna, marehemu Michael Jackson na wacheza sinema wote mnaowajua duniani,”alisema.
Katika kutekeleza ahadi yake hiyo, Rais Kikwete alisema tayari ameshaagiza mitambo ya studio kwa ajili ya kurekodi muziki yenye thamani ya sh. milioni 50.
Rais Kikwete alisema pia kuwa, tayari amesharekodi nyumba kwa sh. milioni saba kwa mwaka kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo vya muziki, ambavyo vitakuwa mali ya wasanii nchini.
Alisema mara baada ya vifaa hivyo kufungwa, atakuja mtaalamu kutoka Uingereza, ambaye kazi yake itakuwa kuwafundisha wasanii jinsi ya kuitumia. Alisema mtaalamu huyo ataifanyakazi hiyo kwa miaka miwili.
“Lakini hatutaishia hapo. Watakapoanza kuimiliki mitambo hiyo, kazi itakayofuata itakuwa usambazaji wa kazi zao. Wasanii wanadhulumiwa na wanaorekodi. Wanatajirika kwa usambazaji,”alisema Rais Kikwete.
Kwa kutambua kuwepo kwa tatizo hilo, Rais Kikwete alisema wamempa kazi mtaalamu mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuandaa utaratibu mzuri wa usambazaji wa kazi za wasanii na amelipwa sh. milioni 20 kwa ajili ya kazi hiyo.
Kikwete alisema binafsi anakunwa mno na muziki wa wasanii wa kizazi kipya, hasa mashairi yao na midundo ya ala, lakini hawezi kuucheza kwa sababu ya umri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment