KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 19, 2010

SIMBA PWAAAAAA!

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga (kulia) akikabidhi Ngao ya Hisani kwa nahodha wa Yanga, Fred Mbuna mara baada ya timu hiyo kuishinda Simba kwa penalti 3-1 katika mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo).

SHABIKI maarufu wa Yanga kwa jina la Shabani Ramadhani 'Mpogoro' akikimbia uwanjani kwa furaha mara baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo).


KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri (kushoto) akitoa maelekezo kwa wachezaji wake, Emmanuel Okwi na Mohamed Banka wakati wa pambano hilo. (Picha zote na Emmanuel Ndege).


KIPA wa Simba, Ally Mustapha 'Barthez' akipatiwa huduma na daktari wa timu hiyo baada ya kugongana na mchezaji Kenneth Asamoah wa Yanga wakati wa pambano hilo huku wachezaji wenzake wakipeana ushauri.

BEKI Juma Jabu wa Simba (kushoto) akimkwatua mshambuliaji Nsa Job wa Yanga wakati wa pambano hilo.


KOCHA Kostadin Papic wa Yanga akifuatilia pambano hilo kwa makini


KIKOSI cha Yanga kilichomenyana na Simba jana



KIKOSI cha Simba kilichomenyana na Yanga jana.

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Simba jana walianza vibaya msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Yanga katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya timu hizo mbili kongwe nchini kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.
Dalili za Simba kufungwa zilianza kuonekana mapema baada ya kupoteza penalti tatu mfululizo zilizopigwa na Emmanuel Okwi, Uhuru Selemani na Amri Kiemba wakati Yanga ilipoteza penalti moja iliyopigwa na Ernest Boakye.
Penalti zilizoiwezesha Yanga kutoka uwanjani kifua mbele, zilifungwa na Geofrey Bonny, Stephano Mwasika na Isaack Boakye. Penalti pekee ya Simba ilifungwa na kiungo wake, Mohamed Banka.
Hii ni mara ya pili kwa Yanga kuishinda Simba katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2001 wakati Yanga ilipoichapa Simba mabao 2-1.
Ushindi huo pia ulikuwa wa kulipiza kisasi kwa Yanga kufuatia kuchapwa mabao 4-3 na Simba katika mechi ya mwisho ya ligi kuu iliyochezwa kwenye uwanja huo Aprili 18 mwaka huu.
Mwaka jana, Yanga ilishindwa kutamba katika mechi nyingine ya kuwania ngao hiyo baada ya kuchapwa idadi hiyo ya mabao na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Kwa kawaida, mechi ya kuwania Ngao ya Hisani huchezwa kila mwaka kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, inayotarajiwa kuzishirikisha timu 12 msimu huu. Ligi hiyo inatarajiwa kuanza keshokutwa.
Timu hizo zililianza pambano hilo kwa tahadhari kubwa huku kila upande ukiusoma mwingine. Katika dakika hizo za mwanzo, kila timu ilifanya mashambulizi ya kushtukiza na kuwa makini katika kuokoa mipira ya hatari.
Yanga nusura ipate bao dakika ya tatu wakati Athumani Iddi ‘Chuji’ kupokea pande safi kutoka kwa Nsa Job, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Ally Mustapha.
Simba ilijibu mapigo dakika ya 39 wakati Emmanuel Okwi alipowatoka mabeki wawili wa Yanga na kufumua shuti kali lililotoka sentimita chache nje ya lango.
Dakika mbili baadaye, Nsa alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao Yanga baada ya kuwazidi mbio mabeki Juma Jabu na Juma Nyoso wa Simba, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko ya wachezaji. Yanga iliwapumzisha Kenneth Asamoah na Chuji, ambao nafasi zao zilichukuliwa na Jerry Tegete na Geofrey Bonny. Simba iliwaingiza Amri Kiembe na Shija Mkina kuchukua nafasi za Jerry Santo na Nico Nyagawa.
Katika kipindi hicho, kasi ya mchezo iliongezeka kwa kila timu huku zikishambuliana kwa zamu, lakini umaliziaji mbovu ulikuwa kikwazo kwa timu zote mbili kupata mabao.
Abdi Kassim ‘Babi’ angeweza kuifungia Yanga bao dakika ya 54 alipofumua shuti kali akiwa nje kidogo ya eneo la hatari la Simba, lakini lilimbabatiza beki Nyoso na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.
Dakika moja baadaye, beki Jabu wa Simba alipanda mbele kusaidia mashambulizi na kutoa pande safi kwa Okwi, lakini wakati akijiandaa kufunga, kipa Yaw Berko wa Yanga alitokea na kuudaka mpira miguuni kwake.
Kipa Mustapha wa Simba alidhihirisha kuwa ni moto wa kuotea mbali dakika ya 71 baada ya kupangua shuti kali la Nsa kabla ya beki Joseph Owino kutokea na kuondosha mpira kwenye eneo la hatari.
Simba itaijutia nafasi aliyopata Uhuru dakika ya 82 alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Berko wa Yanga. Okwi naye alipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga dakika ya 83 na 88 baada ya mashuti yake kutoka nje ya lango.
Katika pambano hilo lililochezeshwa na mwamuzi Ramadhani Kibo Ibada kutoka Zanzibar, wachezaji sita walionyeshwa kadi za njano kwa makosa ya kucheza rafu mbaya. Wachezaji hao ni Nadir, Isaack na Ernest Boakye wa Yanga na Santo na Mussa wa Simba.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic alisema anashukuru timu yake kupata ushindi na kwamba sasa anaelekeza akili yake katika michuano ya ligi kuu.
Papic alisema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na kwamba pambano lilikuwa gumu. Alisema atarekebisha dosari zilizojitokeza kwa wachezaji wake kabla ya kuanza ligi keshokutwa.
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri alisema wamekubali kushindwa na kuongeza kuwa, kipigo hicho kilikuwa cha bahati mbaya kwa timu yake, iliyotawala sehemu kubwa ya pambano hilo.
SIMBA: Ally Mustapha, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyoso, Joseph Owino, Jerry Santo/Amri Kiemba, Nico Nyagawa/Shija Mkina, Mohamed Banka, Mussa Hassan/ Patrick Ochan, Emmanuel Okwi, Uhuru Selemani.
YANGA: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa/ Fred Mbuna, Stephano Mwasika, Nadir Haroub, Isaack Boakye, Ernest Boakye, Nurdin Bakari, Athumani Iddi/Geofrey Bonny, Kenneth Asamoah/ Jerry Tegete, Nsa Job, Abdi Kassim/Yahya Tumbo.




No comments:

Post a Comment