KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 26, 2017

SIMBA PUNGUFU YAIDUWAZA YANGA


LICHA ya kucheza ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, Simba jana ilionyesha maajabu baada ya kusawazisha na kuibwaga Yanga mabao 2-1 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ililazimika kumaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10, baada ya beki wake wa kushoto, Javier Bokungu kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Obrey Chirwa wa Yanga.

Kabla ya Bokungu kutolewa, Yanga ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kuifanya Simba iwe kwenye wakati mgumu wa kutafuta bao la kusawazisha huku mashabiki wake wakiwa wamenyong'onyea.

Iliwachukua Yanga dakika tano kuhesabu bao kwa njia ya penalti baada ya beki Novatus Lufunga wa Simba kumkwatua Chirwa ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilifungwa na Simon Msuva.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Joseph Omog wa Simba kipindi cha pili, yaliongeza uhai kwa timu hiyo licha ya kubaki ikiwa na wachezaji 10. Kocha huyo aliwaingiza Jonas Mkude, Saidi Ndemla na Shiza Kichuya.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo aliisawazishia Simba dakika ya 66 baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Kichuya.

Kichuya aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 80 kwa shuti kali la mbali lililompita kipa Deo Munishi wa Yanga na mpira kujaa wavuni.

Kutokana na ushindi huo, Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 54, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 49, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi.


HATA KWA BAO LA MKONO LAZIMA TUIBUKE WASHINDI GABON-NAPE
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema hata kwa goili la mkono ni lazima Serengeti Boys warejee nyumbani wakiwa ama na kombe au wakiwa wamefuzu kushiriki kombe la dunia kwa kuwa moja ya timu mbili zinazohitajika.

Kauli ya Waziri Nape ameitoa leo asubuhi wakati akifungua mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 safari kuelekea Anfield ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu benki hiyo kuanzishwa mwaka 1917 yaliyoanza kutimua vumbi katika viwanja vya JK Park Kidongo Chekundu, Gerezani.

Alisema haiwezekani taifa hili kuwa na Waziri mjanja kama Nape halafu Serengeti Boys inakosa kombe huko Gabon na nafasi ya ushiriki Kombe la dunia.

Pamoja na kauli yake hiyo Waziri Nape aliiomba Benki ya Standard Chartered kushiriki katika jukumu la kuhakikisha kwamba Serengeti Boys ama inarejea na kombe au inafuzu miongoni mwa timu mbili zitakashiriki Kombe la Dunia.

Wednesday, February 22, 2017

KESI YA WEMA SEPETU KUTAJWA TENA MACHI 15 2017.


Msanii Wema Sepetu akitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi yake ya kuahirishwa hadi March 15 mwaka huu.Kesi hiyo imeaihirishwa na Hakimu Mkazi Thomas Simna baada ya wakili wa Serikali Constantine Kakula kuieleza mahakama kuwa upelelezi dhidi ya kesi hiyo bado haujakamilika.

MASOGANGE APANDISHWA MAHAKAMA YA KISUTU,AACHIWA KWA DHAMANA
Mrembo anayepamba video za wasanii nchini, Agnes Gerald Waya maarufu kama Masogange au Deal (28), amepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kutumia dawa za kulevya.

Mrembo huyo anayeishi Makongo Juu ambaye alikuwa akitumia muda mwingi kujiziba sura yake kwa mtandio na miwani ya Giza alisomewa tuhuma zake mbele ya Hakimu Mkazi Willbard Mashauri. Hata hivyo, ameachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama.

Mahakama ilimtaka Masogange kuwekwa dhamana ya milioni kumi hali kadhalika na wadhamini wake wawili nao walitakiwa kuwekwa kiasi hicho cha fedha.

Aidha mahakama imemuamuru kutosafiri nje ya Dar ea Salaam bila ya kupata kibali cha Mahakama.Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa serikali, Constantine Kakula amedai kuwa kati ya Februari 7 na 14 mwaka huu katika Eneo na Wilaya isiyojulikana lakini ndani ya jiji la Dar es salaam, Masogange alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Katika hatua ya pili, Mshtakiwa Masogange siku na mahali pasipojulikana alitumia dawa za kulevya aina ya OXazempam.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.Masogange amekana kujihusisha na tuhuma hizo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 21, mwaka huu.

KASEJA MCHEZAJI BORA WA JANUARI LIGI KUU YA VODACOM


Golikipa wa timu ya Kagera Sugar, Juma Kaseja Juma amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom wa mwezi Januari kwa msimu wa 2016/2017.

Kaseja aliwashinda wachezaji Mbaraka Abeid pia wa Kagera Sugar na Jamal S. Mtengeta wa Toto African.

Katika mechi tatu ambazo timu ya Kagera ilicheza kwa mwezi huo, Kaseja ambaye alicheza kwa dakika zote 270 alikuwa kiongozi na mhimili wa timu na aliisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo yote ambapo ilikusanya jumla ya pointi 9 zilizoifanya timu hiyo kupanda nafasi mbili katika msimamo wa ligi kwa mwezi huo wa Januari (kutoka nafasi ya 5 hadi ya 3).

Katika michezo hiyo mitatu, Kagera Sugar ilifunga mabao sita na Kaseja alifungwa bao moja tu na alionesha nidhamu ya hali ya juu ikiwemo kutopata onyo lolote (kadi).

Kwa kushinda tuzo hiyo, Kaseja atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania.

WAZIRI WA MICHEZO NAPE KUZINDUA MFUKO WA KUSAIDIA SERENGETI BOYS


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Nape Nnauye (Mb) kesho Februari 23, 2017 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa miguu kwa vijana na wanawake.

Uzinduzi huo utakaofanyika saa 5.00 asubuhi, utahudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo, Yussuph Singo. Utafanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Courtyard, Upanga jijini Dar es Salaam.

Mfuko huo uko chini ya Mwenyekiti Bw. Tido Mhando ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Azam Media wakati Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo ni Bw. Dereck Murusuri.

Wajumbe wake ni Bi. Beatrice Singano, Bw. Ephraim Mafuru, Bw. Tarimba Abbas, Bw. Joseph Kahama, Bw. Salum Rupia na Bw. Meshack Bandawe. Majukumu ya Kamati ya Mfuko huo ni kukusanya rasilimali kwa ajili ya kuendeshea program za TFF za maendeleo ya mpira wa vijana wa wanawake.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, mfuko huu ni huru, una sekretariet yake, akaunti yake benki na ofisi zake zinazotarajiwa kuwa Mikocheni, Dar es Salaam.

Tuesday, February 21, 2017

SERIKALI YAZIONYA SIMBA NA YANGA


Ndugu Watanzania Jumamosi, tarehe 25/02/2017 saa 10.00 jioni Uwanja wa Taifa tutakuwa na mchezo mkubwa wa kati ya Simba SC na Yanga FC.

Ikumbukwe kuwa mchezo uliopita wa timu hizi uliochezwa kwenye uwanja huu tarehe 1/10/2016 zilitokea vurumai zilizosababisha Serikali kuufungia Uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu.Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo uvunjifu wa viti,mageti na mbaya zaidi baadhi ya watu walijerehuliwa.

Tunaomba waandishi na wadau wote tushirikiane kuelimisha umma wa wapenda michezo kuwa Michezo ni Furaha, Amani na Upendo.

Kuelekea mchezo ujao tungependa kueleza yafuatayo:-

Tunawaomba wadau wote tujenge utamaduni wa kununua tiketi mapema kwani mpaka sasa tiketi zinapatikana kupitia SELCOM. Hii itaondoa msongamano na lawama zisizo za lazima.

Tunafahamu kuwa kuna changamoto za matumizi ya mfumo wa Ki- elektroniki lakini hatuna budi kuendelea kuelimishana na kujifunza kwani huko ndiko Dunia ilipo,tutakua watu wa ajabu leo tukisema hatuwezi kutumia mfumo huu kisa changamoto hizi ndogondogo zinazojitokeza.

Tujiepushe na vurugu za aina yoyote siku ya mchezo kwani Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayepelekea uvunjifu wa amani siku ya mchezo.

Kutakua na ulinzi wa kutosha ndani na nje ya Uwanja hasa ukichukulia kuwa kuna kamera zenye uwezo wa kumuona kila mtu anayeingia Uwanjani na kila anachokifanya.Tutapiga picha na kuzirusha kwenye TV kubwa ya Uwanja kwa wale wote watakaobainika kuashiria/kutenda vurugu sheria itachukua mkondo wake.

Tunatoa rai kwa waamuzi waliopewa dhamana ya kuchezesha mchezo huu,wajue kuwa wana dhamana kubwa hivyo ni vyema wakafuata kanuni na sheria za mchezo husika ili kuepusha malalamiko.

Mwisho napenda niwatakie mchezo mwema kwa timu zote wajue kuwa Watanzania wanategemea burudani nzuri kutoka kwao,na niwaombe mashabiki wakumbuke kuwa wajibu wao mkuu ni kuzishangilia na kuzipa hamasa timu zao na si vinginevyo.

HUSSEIN MACHOZI KUVUNJA UKIMYA NA ‘NIPE SIKUACHI’ CHINI YA COMBINATION SOUND


Baada ya kukaa kimya kwa miezi mingi bila kuachia wimbo, Hussein Machozi anatarajia kuachia wimbo mpya wiki chache zijazo. Wimbo huo unajulikana kwa jina la ‘Nipe Sikuachi.’

Wimbo huo umetayarishwa na mshindi wa tuzo ya mtayarishaji bora wa Bongo Flava katika miaka tofauti, Man Walter kupitia studio zake za Combination Sound.

“Combination yangu ya mimi na Man Walter, sidhani kama kuna kitu cha mchezo hapo,” anasema Machozi ambaye amethibitisha kuanza kufanya kazi rasmi kwa uangalizi wa label ya mtayarishaji huyo mashuhuri nchini Tanzania.

“Man Walter ni mshkaji kitambo, tumekutana tukakubaliana kufanya kazi na tukaona kabisa kwamba sisi tukifanya kazi wawili itakuwa kazi na ndicho kilichofanyika japo tuna makubaliano ya kusaini. Kwahiyo ni mimi tu nirudi Tanzania tuje tukae tusaini, lakini ukweli ni kwamba mimi nafanya kazi chini ya uongozi wa Kombinega,” amesema.

“Video pia imefanyika Italy, Gressoney Italy. Kuna mabadiliko makubwa ukiangalia location ambazo tumezizoea, ukiangalia video ambazo kila siku tunaziona Tanzania za magari na majumba,” amesisitiza muimbaji huyo.

Machozi ambaye anafahamika kwa vibao vingi vilivyowahi kufanya vizuri kwenye vituo vya redio na runinga ndani na nje ya Tanzania vikiwemo ‘Utaipenda’, ‘Kwaajili Yako’, ‘Addicted’ na zingine, amedai kuwa ukimya wake ulitokana na majukumu mengine ya kimaisha.

“Kama unavyojua, hakuna mtu anapenda kuwa kimya, na ukifuatilia vizuri kuna kazi kadhaa nilishawahi kuziachia lakini hazikufika nilikotarajia nadhani kwasababu ya ukosefu wa management.

Kwa sasa Hussein anaishi nchini Italia baada ya kuwa ameenda kusoma, lakini hiyo haimaanishi kuwa ameupa kisogo muziki, kitu anachoamini alizaliwa kukifanya.

“Ilikuwa ni kozi fupi ambayo kwa sasa imeisha na nafanya shughuli za kawaida kujipatia riziki,” anaeleza.

Machozi anakikisha kuwa ujio wake mpya utakuwa wa tofauti.

“Kinachokuja kuonekana sasa hivi, hakijawahi kuonekana katika macho ya watu na nimejaribu kufanya hivyo kwasababu mimi mwenyewe nahitaji mabadiliko, nifanye kitu ambacho ni kipya zaidi hata kwenye macho yangu mimi, kwahiyo nimekikubali kwamba  ni kipya, video ni mpya, audio ni mpya kabisa.”

Anasema tarehe rasmi ya kutoka kwa video na wimbo itatangazwa hivi karibuni.

Thursday, February 16, 2017

DIAMOND AKAMATWA NA POLISI, ATOZWA FAINI


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond', jana alitiwa mbaroni na kikosi cha polisi cha usalama barabarani.

Manji alifikishwa kwenye kituo hicho kwa kosa la kuendesha gari huku akiimba wimbo wake wa Marry You' huku akiwa akiachia usukani mara kwa mara, akiwa hajafunga mkanda wa gari.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye kituo hicho cha polisi, Diamond anadaiwa kutenda kosa hilo Jumamosi iliyopita, siku ambayo mwanawe wa pili wa kike alikuwa akitimiza umri wa siku 40.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga, alikuwa miongoni mwa maofisa wa polisi walioshiriki kumuhoji msanii huyo.

Kamanda Mpinga alikiri kukamatwa kwa msanii huyo na kutiwa hatiani kwa makosa mawili, moja la kuendesha gari akiwa ameachia usukani na la pili kutofunga mkanda.

"Imebidi alipe faini kwa sababu makosa hayo mawili adhabu yake ni kulipa faini. Amelipa faini shilingi 60,000 kwa sababu kila kosa adhabu yake ni faini ya shilingi 30, 000,"alisema.

Kamanda Mpinga alisema makosa aliyokutwa nayo Diamond, yamekuwa yakifanywa na watu wengi wanapoendesha magari hivyo kukabiliwa na adhabu hizo.


Wednesday, February 15, 2017

MALINZI AIPONGEZA LIPULI KUPANDA DARAJARais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameuandikia barua uongozi wa Lipuli ya Iringa kwa mafanikio ya kupanda daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimuwa 2017/18.

Lipuli ya Iringa imepanda daraja baada ya kupita miaka 17 na Rais Malinzi amesema katika barua yake hiyo kwenda kwa Katibu Mkuu wa Lipuli, akisema: “Nitumie fursa hii kukupongeza wewe, uongozi wa klabuy ako, benchi la ufundi na wadau wote wa timu ya Lipuli kufuatia kupanda daraja kwenda Ligi Kuu.

“Bila shaka ni kazi kubwa imefanyika ikihusisha kujitolea kwa ari na mali kuhakikisha mnafika hapa mlipo,” ilisema barua hiyo na kuongeza: “Rai yangu kwenu ni kuongeza juhudi na kuendesha klabu kwa weledi mkubwa zaidi ili muweze kuwa washindani wa kweli katikal igi.”

Lipuli iliyo kuwa kundi “A” imepanda daraja na kuzipiku timu zaK iluvya United ya Pwani, Pamba ya Mwanza, African  Sports yaTanga, Polisi Dar, Ashanti United, Friends Rangers, Mshikamano za Dar es Salaam.

LIGI YA WANAWAKE SITA BORA TANZANIA BARA KUANZA FEBRUARI 18


Baada ya timu sita (6) kutinga hatua ya Sita Bora yaLigi Kuu ya Wanawake ya Shirilkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufahamika,ratiba rasmi ya michuano hiyo, imetoka na inaonyesha kuwa hatua hiyo ya kutafuta bingwa wa msimu, itaanza Februari 18, mwaka huu.

Timu sita zilizofanikiwa kufika hatua ya Sita Bora ni JKT Queens ya Dar es Salaam, Mlandizi Queens ya Pwanina Fair Play ya Tanga kutoka Kundi “A” wakati kutoka Kundi “B” zimo Marsh Acedemy ya Mwanza, Sisterz ya Kigoma na Panama ya Iringa.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kutakuwa na mechi mbili kila siku katika kituo kimoja kwa mujibu wa kanuni. Kituo hicho ni Uwanja wa Karume, ulioko Ilala jijini Dar es Salaam ambako mchezo wa kwanza utaanza saa 8.00 mchana wakati mwingine utaanza saa 10.00 jioni.

Ratiba inaonesha kwamba siku ya Februari 18,mwaka huu kutakuwa na mchezo Kati ya JKT Queens na Mlandizi saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 kutakuwa na mchezo kati ya Fair Play na Sisterz.

Februari 20, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Panama saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Mlandizi na Fair Play.

Februari 22, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Sisterz na Marsh Academy saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Panama na JKT Queens.

Februari 24, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Fair Play na JKT Queens saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Academy na Mlandizi Queens.

Februari 26, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Panama na Sisters saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya JKT Queens na Marsh Academy.

Februari 28, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Sisters na Mlandizi Queens saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Panama na Fair Play.

Machi 2, mwaka huu kutakuwa na mchezo kati ya Marsh Acedemyna Fair Play saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni kutakuwa na mchezo kati ya Mlandizi na Panama.

Machi 3, mwaka huu kutakuwa na mchezo mmoja tus aa 10.00 jioni ambako JKT Queens watamaliza na Sisterz.

SIMBA YAPANIA KULIPA KISASI DHIDI YA AFRICAN LYON KOMBE LA AZAM FC


Raundi ya Sita ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup – 2016/17, itaanza Februari 16, 2017 badala ya Februari 24, mwaka huu. Mchezo huo awali ulipangwa kufanyika Machi mosi, 2017.

Kutakuwa na mchezo mmoja kabla ya kuendelea tena Februari 24, mwaka huu, kwa michezo minne kuchezwa kwa siku hiyo kuanzia saa 10.00 jioni kasoro mchezo mmoja tu utakaopigwa saa 1.00 jioni.

Michezo hiyo kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT Ruvu yaP wani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilihali Azam naMtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala – mchezo utakaofanyika saa 1.00 usiku.

Jumapili Februari 26, mwaka huu timu yaM bao FC itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United kwenyeUwanja waTaifa jijini Dar Es Salaam.

MAYANGA AKABIDHI PROGRAMU YA MIEZI SITA YA TAIFA STARS KWA TFF


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limepokea programu ya miezi sita ya timu ya taifa, Taifa Stars kutoka kwa kocha wa muda, Salum Mayanga, anayekaimu nafasi iliyoachwa wazi na Charles Boniface Mkwasa ambaye kwa sasa ni Katibu wa Yanga SC.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema kwamba programu hiyo itahusisha kambi za mazoezi na michezo ya kirafiki.
Mapunda amesema kwamba kwa ujumla Mayanga amewasilisha programu ya maandalizi ya kufuzu kwa Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
“Michezo ya kirafiki ni kocha Mayanga ndiye atapendekeza ichezwa nje ya nchi au ndani, lakini pia programu hiyo inaelezea juu ya maandalizi ya mechi ya CHAN ya 2018 na AFCON ya 2019 Cameroon,”amesema Lucas.
Taifa Stars itaanza na Rwanda katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchni Kenya na mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya Julai 14 na 16 kabla ya timu hizo kurudiana Uwanja wa Amahoro, Kigali kati ya Julai 21 na 23.
Ikifanikiwa kuitoa Rwanda, Tanzania itamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19 na 20, mwaka huu.
Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu fainali za CHAN, ambayo ilikuwa ni mwaka 2009 zikifanyika kwa mara ya kwanza kabia.
Kwa upande wa AFCON, Taifa Stars imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho.
Mshindi wa kila kundi atafuzu moja kwa moja AFCON ya 2019, wakati timu nyingine tatu zitakazomaliza nafasi ya pili na wastani mzuri zaidi ya nyingine zitafuzu kama washindi wa pili bora.
Tanzania imewahi kucheza mara moja tu fainali za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa hatua ya makundi.

Monday, February 13, 2017

YANGA YAWATEMBEZEA KICHAPO KIKALI WACOMORO


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya klabu bingwa Afrika, Yanga jana walianza vyema michuano hiyo baada ya kuitandika Ngaya FC ya Comoro mabao 5-1 mjini Coron.

Wafungaji wa mabao ya Yanga walikuwa Justin Zullu, Amis Tambwe, Juma Mahadhi, Simon Msuva na Obrey Chirwa.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inahitaji sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano ili iweze kusonga mbele katika michuano hiyo.

Timu mbili hizo zinatarajiwa kurudiana Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


TAMASHA LA BUSARA LAFANA ZANZIBAR

Vijana wa Rico & the band ya zanzibar wakitumbuiza siku ya pili ya Tamasha la sauti za Busara kwenye ukumbi wa Ngomekongwe mjini Zanzibar jana.

Msanii Mirza wa Rico & the band ya zanzibar akichekecha muziki kwenye ukumbi wa Ngomekongwe jana.
Wanamuziki wa bendi ya Loryzine kutoka Reunion wakicheza kwenye jukwaa mbele ya mashabiki kwenye ukumbi wa Ngomekongwe mjini Zanzibar jana.
Wapenzi wa muziki wakiwashangilia vijana wa Loryzine jana usiku.

AROBAINI YA DIAMOND YAFANA DAR, AMUONYESHA MTOTO WAKE HADHARANI
Sunday, February 12, 2017

SIMBA YAREJEA KILELENI LIGI KUU


SIMBA imerejea kwenye uongozi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibugiza Prisons mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyoonekana kuwa ya upande mmoja, Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo, hasa safu ya kiungo kutokana na Kocha Joseph Omog kuwapanga wachezaji wengi wa safu hiyo.

Iliwachukua Simba dakika 18 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Juma Luizio baadaya kuunganisha wavuni krosi kutoka kwa beki Javier Bokungu.

Ibrahim Ajib aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 28 baada ya gonga safi kati yake na Laudit Mavugo. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Mavugo aliihakikishia Simba ushindi dakika ya 68 baada ya kufunga bao la tatu, akisindikiza wavuni krosi kutoka kwa Ajib.

Wednesday, February 8, 2017

KEMONDO SUPER FC KUSHUSHWA DARAJATimu ya Kimondo Super SC imeshushwa madaraja mawili (hadi Ligi ya Mkoa), na matokeo ya mechi zake zote ilizocheza katika kundi la B yamefutwa kwa kushindwa kufika uwanjani kucheza mechi dhidi ya JKT Mlale bila sababu za msingi.

Mechi hiyo namba 47 (JKT Mlale vs Kimondo Super SC), ilitakiwa kuchezwa Januari 28, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, lakini Kimondo Super SC haikutokea uwanjani wala kutoa taarifa yoyote hadi Februari 1, 2017 ilipotuma taarifa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), na kutoa sababu ambazo hazikukubaliwa na Kamati.

 Pia Kimondo Super SC imetozwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambapo kati ya hizo sh. 1,000,000 (milioni moja) itachukuliwa na TPLB, na sh. 1,000,000 (milioni moja) italipwa JKT Mlale. Adhabu dhidi ya Kimondo Super SC ni utekelezaji wa Kanuni ya 28(1) na (2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

RAUNDI YA SITA AZAM SPORTS FEDERATION CUP 2016/2017

Raundi ya Sita ya mechi za kuwania Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) yaani Azam Sports Federation Cup – 2016/17, itaanza Februari 24, 2017 kwa michezo minne kuchezwa kwa siku hiyo kuanzia saa 10.00 jioni kasoro mchezo mmoja tu utakaopigwa saa 1.00 jioni.

Michezo hiyo kwa mujibu wa ratiba inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), itakuwa ni kati ya Madini FC ya Arusha na JKT Ruvu ya Pwani watakaocheza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wakati Kagera Sugar itacheza Stand United ya Shinyanga Uwanja wa kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine itakuwa ni kati ya The Mighty Elephant ya Ruvuma na Ndanda FC ya Mtwara zitakazopambana kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ilihali Azam na Mtibwa Sugar watacheza Chamanzi –Mbagala – mchezo utakaofanyika saa 1.00 usiku.

Jumapili Februari 26, mwaka huu timu ya Mbao FC itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City zote za Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Jumatano Machi 1, 2017 Simba SC itacheza na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam wakati Machi 7, mwaka huu Young Africans SC itacheza na Kiluvya United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.

KOCHA MOROCCO AFUNGIWA MECHI TATUKamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72), imemfungia Kocha wa Stand United, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kushiriki michezo mitatu uwanjani na faini ya Sh 500,000 (laki tano).

Katika mechi Na. 160 ya Ligi Kuu ya Vodacom uliozikutanisha timu za JKT Ruvu na Stand United iliyochezwa Januari 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Morocco aliondolewa kwenye benchi (Ordered off) kwa kosa la kupiga maamuzi ya mwamuzi na kutoa lugha chafu.

Kamati hiyo ya Saa 72 imechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 40 (11) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Makocha. Morocco hata kama atakuwa amemaliza mechi tatu nje ya benchi, hataruhusiwa kukaa kwenye benchi hadi awe amelipa faini hiyo.

Adhabu hiyo ya Morocco itaendelea kumhusu hata kama utakuwa umehamia kwenye timu nyingine na katika msimu mwingine wowote.