KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 12, 2017

TANZANIA BARA YATHIBITISHA KUSHIRIKI CHALENJI ZOTE



Baada ya kupita miaka miwili bila kuchezwa kwa mashindano ya kuwania Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki, michuano hiyo imerejea tena msimu huu na Tanzania imethibitisha kushiriki.

Nchi wanachama Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu  Tanzania (TFF), Kidao Wilfred amethibitisha kikosi cha kwanza cha ‘Taifa Stars’ kushiriki na matarajio ya kufanya vema michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Novemba 25, 2017 hadi Desemba 9, mwaka huu.

Kidao amesema kwamba uteuzi wa timu za kwanza kwa kila nchi mwanachama wa Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ni makubaliano ya viongozi wa CECAFA waliokutana kwa pamoja huko Sudan, Septemba, mwaka huu.

Kutokana na makubaliano hayo ya kuita timu za kwanza, michuano hiyo itaathiri kidogot ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuwa wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho, wanatoka timu za VPL.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amesema: “Tutakaa kama kamati na kuangalia siku ya Jumatano na Alhamisi baada ya michuano hiyo na kupanga ratiba ya mechi ambazo zitapanguliwa wakati wa michuano ya Chalenji.”

Mbali ya michuano hiyo, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika Bujumbura nchini Burundi kuanzia Desemba 12, 2017 hadi Desemba 22, mwaka huu.

Kadhalika, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji kwa wanawake ikienda kutetea taji katika michuano itakayofanyika Rwanda mwezi Desemba, mwaka huu. Tarehe rasmi itatajwa baadaye.

CECAFA imeamua kurejesha hadhi yake kwani mara baada ya michuano ya Chalenji ya vijana huko Burundi, mwakani itakuwa ni zamu ya Tanzania ambako michuano hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 11, 2018 hadi Agosti 25, mwakani.

Wakati huo huo Kidao amethibitisha Tanzania kuwa wenyeji wa mashindano ya Vijana ya Chalenji ya CECAFA/CAF kwa vijana chini ya miaka 17 mwakani na mashindano hayo yatatumika kama sehemu ya kufanya maandalizi Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (AFCON – U17).

Michuano ya mwakani ina baraka za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa sababu shirikisho hilo linataka kutumia michuano hiyo ya vijana ya Kanda mbalimbali za Afrika kupata timu saba katika michuano AFCON – U17 ya mwaka 2019.

Kanda hizo ni CECAFA (Afrika Mashariki), COSAFA (Nchi za Kusini mwa Afrika), WAFU – UFOA (Afrika Magharibi); UNAF (Afrika Kaskazini) na UNIFFAC (Afrika ya Kati).

No comments:

Post a Comment