KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 29, 2012

KALALA: NIMERUDI NYUMBANI

MWIMBAJI nyota wa zamani wa bendi ya Mapacha Watatu, Kalala Junior amesema ameamua kurejea Twanga Pepeta kwa vile bendi hiyo ni kama nyumbani kwake.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Kalala alisema amefurahi kuona kuwa amepokelewa vyema na wanamuziki wa bendi hiyo na kumpa ushirikiano mkubwa.
Kalala amejiunga na Twanga Pepeta, akitokea kundi la Mapacha Watatu, ambalo alishiriki kulianzisha mwaka jana akiwa na Jose Mara na Khalid Chokoraa.
Wakati alipotangaza kujitoa Mapacha Watatu miezi miwili iliyopita, mwanamuziki huyo alisema anataka kumpumzika kwa muda, hali iliyosababisha kuwepo na hisia kwamba, huenda alitaka kujiunga na bendi ya Mashujaa.
Kalala anatarajiwa kutambulishwa rasmi kesho wakati Twanga Pepeta itakapofanya onyesho kwenye ukumbi wa Mango Garden uliopo Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika onyesho hilo, Kalala anatarajiwa kutambulisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la Nyumbani ni nyumbani.
Kalala amejigamba kuwa, amepania kuwapa mashabiki wa bendi hiyo vitu vipya, ambavyo walikuwa wakivikosa kwa muda mrefu.
“Nimerudi Twanga Pepeta nikiwa na vitu vipya, ambavyo nitaanza kuvionyesha siku ya utambulisho,”alisema mwimbaji huyo, ambaye ni mtoto wa mkongwe wa muziki nchini, Hamza Kalala.
Kalala alitambulishwa rasmi na uongozi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika wiki iliyopita.
Wakati wa utambulisho huo, Kalala aliwaambia waandishi wa habari: “Koti lilikuwa linanibana nilipokuwa Mapacha Watatu, nimeamua kulivua na kuacha kuendelea kulivaa.”
Kalala alisema amefurahi kujiunga tena na Twanga Pepeta na kuongeza kuwa, amekuja na zawadi ya nyimbo mbili, wa kwanza ukiwa Nyumbani ni Nyumbani, ambao unaelezea mambo aliyokutana nayo katika maisha yake kimuziki.
Mwimbaji huyo mwenye makeke alisema uamuzi wake wa kurejea Twanga Pepeta haukutokana na kulazimishwa, bali mapenzi yake mwenyewe, hasa akikumbuka fadhila alizopata kutoka ASET.
“Nawaomba wadau wa Twanga Pepeta wakae mkao wa kula kwani nimerejea kivingine na watarajie kupata mambo mengi mazuri,” alisema Kalala.
“Nitafanya zaidi ya yale niliyoyafanya zamani, lengo ni kuendelea kushika hatamu katika muziki wa dansi,” aliongeza mwimbaji huyo, ambaye vionjo vyake vimewashika mashabiki wengi wa muziki wa dansi nchini.
Ofisa Habari wa ASET, Mohamed Pizaro alisema ujio wa Kalala katika bendi hiyo umetokana na mpango wao waliouanzisha unaojulikana kwa jina la ‘Amsha Amsha Twanga Pepeta Nyumbani ni Nyumbani’.
Pizaro alisema wamempokea Kalala kwa roho moja na kwamba Twanga Pepeta ni chimbuko la watu na hivyo akitoka mtu ni lazima arudi, kutokana na raha na burudani za bendi hiyo.
Alisema Kalala amepokelewa kwa mikono miwili na wana imani kubwa kwamba watashirikiana naye ipasavyo kuifanya bendi hiyo izidi kunoga.

No comments:

Post a Comment