Makocha watano kutoka timu ya Chelsea ya Uingereza ndiyo watakaoongoza kambi maalumu ya kimataifa ya Copa Coca-Cola yenye wachezaji 140 kutoka nchini 15 itakayofanyika jijini Pretoria kuanzia Agosti 28 hadi Septemba 8 mwaka huu.
Robert Luke Udberg, Russel William Banyard, Oliver Staurt Woodall, Shane Jason Hughes na Dean Aaron Steninger kutoka Chelsea FC Foundation ndiyo wanaounda jopo hilo la makocha litakalowanoa vijana hao wenye umri chini ya miaka 17.
Wachezaji wanaounda Dream Team iliyotokana na michuano ya Copa Coca-Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 24 hadi Julai 15 mwaka huu ni Abrahman Said Mohamed (Zanzibar), Ayubu Alfan (Dodoma), Baker Hamad (Tanga), Edward Joseph (Ruvuma), Hassan Kabunda (Temeke) na Joseph Chidyalo (Dodoma).
Wengine ni Mtalemwa Katunzi (Morogoro), Mwarami Maundu (Lindi), Nankoveka Mohamed (Ilala), Nelson Peter (Morogoro), Rajab Rashid (Mwanza), Said Ramadhan (Kagera), Shiza Kichuya (Morogoro), Shukuru Msuvi (Temeke), Tanganyika Suleiman (Kigoma) na Tumaini Baraka (Kilimanjaro).
Nchi nyingine zitakazokuwa na washiriki katika kambi hiyo ni wenyeji Afrika Kusini, Burundi, Cameroon, Congo Brazzaville, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Swaziland, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Hii ni mara ya sita mfululizo kwa kampuni ya Coca-Cola kupeleka Dream Team kwenye kambi za kimataifa. Mwaka 2007 na 2008, timu hiyo ilikwenda Brazil wakati mwaka 2009, 2010 na 2011 ilikuwa Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment