MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi alirejea nchini juzi na kujiunga na klabu yake ya Simba. Okwi amerejea nchini akitokea Austria, alikokwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Red Bull Salzburg. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, mchezaji huyo anaelezea mipango yake ya baadaye katika soka.
SWALI: Wiki mbili zilizopita ulikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa nchini Austria? Nini matokeo ya majaribio hayo?
JIBU: Ni kweli nilikwenda Austria kwa lengo la kufanya majaribio katika klabu ya Red Bull Salzburg, lakini nilishindwa kutimiza lengo hilo baada ya kuugua.
Niliugua ugonjwa wa malaria na kusababisha nishindwe kufuzu majaribio hayo na kuamua kurejea nyumbani Uganda. Lakini viongozi wa timu hiyo wamenieleza kwamba wataniita tena wakati wowote kwa ajili ya kuendelea na majaribio hayo.
Mipango yangu ya kufanya majaribio haipo kwa klabu hiyo pekee. Mawakala wangu wamepeleka video zangu kwenye klabu zingine kadhaa za Ulaya, hivyo nasubiri taarifa kutoka kwao ili kujua wapi kwingine ninakohitajika.
SWALI: Unataka kusema kwamba inawezekana ukaondoka tena wakati wowote kwenda kufanya majaribio katika klabu nyingine ya Ulaya?
JIBU: Ni kweli naweza kuondoka wakati wowote, lakini napenda kuweka wazi kwamba, hayo yote yatafanyika kama nitapata baraka za viongozi wangu wa Simba kwa sababu bado nina mkataba na klabu hiyo.
SWALI: Wakati ulipokuwa Austria na baadaye Uganda, kulikuwepo ta taarifa hapa nchini kwamba una mpango wa kujiunga na Yanga. Hebu tueleze ukweli kuhusu habari hizi?
JIBU: Kusema ule ukweli, sijawahi kukutana na kiongozi yeyote wa Yanga na kuzungumzia jambo hili. Nimepata taarifa hizi mara baada ya kurejea hapa nchini leo (juzi) na pia kusoma baadhi ya magazeti.
Jambo la msingi ambalo mashabiki wa soka wanapaswa kutambua ni kwamba, bado nina mkataba na Simba hadi mwaka 2013 na kuna vipengele vingi, ambavyo vinanizuia kufanya mazungumzo na klabu nyingine kuhusu usajili.
Moja ya vipengele hivyo kinaeleza kwamba, siruhusiwi kufanya mazungumzo na klabu yoyote hadi mkataba wangu utakapokuwa unakaribia kumalizika na ni lazima nipate ridhaa ya viongozi wa Simba.
SWALI: Lakini kuna habari kwamba ulikutana na mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji ya Yanga ukazungumza naye na ukampa masharti magumu ya kujiunga na klabu yake, je kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Mimi ni mtu mzima na ninaelewa vyema sheria na kanuni za usajili, hivyo nisingeweza kufanya hivyo. Mkataba ni kitu muhimu sana hivyo unapaswa kuheshimiwa na pande zote.
Ninachoweza kusisitiza ni kwamba kwa sasa bado mimi ni mchezaji wa Simba, siwezi kujiunga na klabu nyingine yoyote zaidi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
SWALI: Kuna habari pia kuwa klabu ya Azam nayo ilikuwa inakuhitaji ujiunge nayo kwa ajili ya msimu ujao, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Kama nilivyosema awali, sijawahi kuzungumza na viongozi wa klabu zingine kuhusu suala hilo kwa vile akili yangu yote kwa sasa ni kwenda kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
Hata kama itatokea klabu nyingine kutaka kunilipa pesa nyingi, sintakuwa tayari kuzipokea. Kama ni kucheza soka Tanzania, muda niliocheza unatosha na sasa akili yangu ni Ulaya.
SWALI: Simba imefanya vibaya katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Kagame, unazungumziaje hali hii?
JIBU: Nimesikitika sana Simba kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo, lakini nina hakika zilikuwepo sababu zilizochangia hali hiyo.
Moja ya sababu hizo ni kwamba baadhi ya wachezaji wageni walikuwa bado hawajazoea mfumo wa uchezaji wa timu yetu kwa vile walikuwa wamejiunga na timu kwa muda mfupi.
Lakini baada ya kushuhudia mazoezi ya leo, nina matumaini makubwa kwamba Simba itaendelea kuwa tisho kwa sababu wachezaji wengi ni wazuri na hata mimi nitalazimika kupigania namba kikosi cha kwanza.
SWALI: Unazungumziaje ujio wa Mrisho Ngasa kwenye kikosi cha Simba?
JIBU: Nimefurahia sana kusajiliwa kwa mchezaji huyu kwa sababu ana uwezo mkubwa na ataweza kuisaidia Simba kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya ligi na kimataifa.
No comments:
Post a Comment