YANGA imeifanyia umafia mkubwa Simba baada ya kumteka na kumsainisha beki Mnyarwanda mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mbuyu Twite ambaye Mwenyekiti wa Wekundu hao, Ismail Aden Rage alimsainisha pia mjini Kigali wiki iliyopita ili atue Msimbazi.
Mbuyu ni miongoni mwa wachezaji wapya wa Simba waliotajwa kwenye tamasha la Simba Day, Jumatano iliyopita ingawa hakuwepo nchini.
Mashabiki wa Simba waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa walionyeshwa jezi namba 4 ambayo Mbuyu atakuwa akivaa akiwa Simba.
Wapenzi wa Simba walishangilia wakijua kwamba tatizo limekwisha kwenye safu ya ulinzi kwani Mbuyu atasimama na Juma Nyosso, lakini sasa hali imebadilika.
Simba ilimpa mchezaji huyo dola 30,000 (Sh 45 milioni) na kumalizana naye kwa vita iliyodumu zaidi ya saa nane jijini Kigali, Rwanda ambayo ilipewa jina la Eight Hours in Kigali, ingawa sasa filamu hiyo imeingia katika sehemu ya pili ukipenda unaweza kusema Eight Hours in Kigali-2.
Baada ya Yanga kuchakazwa katika sehemu ya kwanza ya filamu hiyo, waliendelea kupambana vita ya msituni kupitia kwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallaa Binkleb na kufanikiwa kumshawishi mchezaji huyo ili arudishe fedha Simba na apewe kitita kikubwa zaidi.
Mbuyu aliwapigia simu viongozi wa Simba jana Ijumaa asubuhi akiwaambia kuwa amemtuma mtu arudishe fedha zao kwani anataka kurudi kuichezea timu yake ya zamani ya Lupopo ya Congo.
Hata hivyo ilivyofika mchana ilikwishafahamika kuwa ameshaini Yanga kwa kitita kikubwa zaidi.
Inadaiwa kuwa amesaini Yanga kwa kitita cha dola 50,000 (Sh 75 milioni)
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Yanga na kigogo wa kamati ya usajili Abdallah Binkleb aliiambia Mwanaspoti wiki hii kwamba lazima alipize kisasi kutokana na nyodo za Simba iliyotangaza kumsainisha Mbuyu Twite kwa kumgaragaza yeye katika vita ya saa nane mjini Kigali.
Binkleb alitamka kuwa; "Simba wanasema mimi ni bwana mdogo siwawezi kwa fitna na ujuzi wa mambo ya mpira, wanasema sina uzoefu wowote kwenye mambo ya mpira, sasa ninachosema ni kwamba huyo Rage nimemsoma na lazima nilipize kisasi, siwezi kuvumilia maneno yao.
Wanaongea sana mpaka vitu vingine ambavyo havipo kabisa,"alisisitiza Binkleb na kudai kuwa yupo Kampala lakini Mwanaspoti liligundua baadaye kwamba alikuwa amejificha Kigali akipanga mikakati mpaka jana Ijumaa alipomaliza mambo.
Mwanaspoti lilimtafuta pacha wa Mbuyu, Kabange baada ya kumkosa Mbuyu na akasema: "Nipo Kinshasa nafanya mambo yangu, lakini nimeongea na Mbuyu aliniambia anakuja kucheza Tanzania, sijajua kama ni Simba au Yanga, nikiongea naye baadaye ndio atanihakikishia.
"Lakini mimi sina tatizo popote atakapoamua kucheza iwe Simba au Yanga ni sawa, hizo timu zote ni kubwa na zina mafaranga (fedha) nyingi, yeye anaenda kutafuta na mimi nitaenda kutafuta, si lazima tucheze timu moja kama siku zote,"alisema Kabange ambaye amenusurika kwenye rungu la APR lililopanga kuondoa wachezaji wote ambao si wazaliwa wa Rwanda.
APR imewatema Logbo Landry Didier (Ivory Coast), Alex De Avila Peixoto, Oliviero Alves na Douglas Lopes Carneirn (Brazil).
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Rwanda(Ferwafa), Michel Gasingwa ameiambia Mwanaspoti kuwa; "Hatuna taarifa yoyote mpya kuhusiana na huyo mchezaji kujiunga na Simba au Yanga au kuondoka APR."
Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema walichokifanya Yanga ni uhuni ambao haukubaliki katika soka.
Kaburu alisema tayari beki huyo alishaini Simba mjini Kigali mbele ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, viongozi wa Chama cha Soka Rwanda (Ferwafa) na maofisa wa APR.
"Tulifanya makubaliano na Mbuyu wakati wa michuano ya Kombe la Kagame. Tulikubaliana kila kitu. Akaomba arudi Rwanda kumalizia mkataba wake na ndipo wiki iliyopita mwenyekiti wangu Rage alipokwenda kumsainisha mkataba wa miaka miwili mjini Kigali mbele ya maofisa wa APR na Ferwafa," alisema Kaburu.
"Baada ya kusaini aliomba kurudi kwenda kubadilisha pasipoti yake kwao Congo kabla ya kuja Dar es Salaam kuungana na wachezaji wa Simba, lakini tunashangazwa na mambo yanavyoendelea.
Tunadhani ametekwa na watu wa Yanga kwa sababu hata simu yake ameibadilisha.
Kaburu alisema kuwa walimpa kitita cha dola 30,000 (Sh 45 milioni), lakini Yanga wamempa fedha zaidi.
Kaburu alisema kuwa katika jambo la kushangaza Yanga wameomba ITC kupitia Congo, ambako mchezaji huyo amewahi kuchezea klabu ya Lupopo tofauti na kanuni zinavyosema kuwa leseni ya uhamisho wa kimataifa huombwa katika nchi ambako mchezaji amecheza kwa mara ya mwisho yaani Rwanda.
Kaburu alisema Simba nao haijakaa kimya kwani imeomba ITC kwa Ferwafa na kwamba hawatakuwa tayari kukubali kushindwa katika hilo.
Kiongozi mmoja wa Lupopo ya Congo, ambaye hakutaka jina lake litajwa gazetini kwa sababu si msemaji alisema kuwa Mbuyu ni mchezaji wao na alikuwa amekwenda APR kwa mkopo tu.
"Ni kweli Yanga wamekuja hapa Congo, tumewapatia barua ya kuwaruhusu kumsajili Mbuyu na tumeipeleka nakala kwa Chama cha Soka Congo. Hivyo Yanga wanaweza kuomba ITC kupitia chama chetu hapa Congo," alisema kiongozi huyo.
Habari ambazo zilipatikana baadaye Mwanaspoti ikienda mtamboni zinasema kuwa tayari Yanga walikuwa wamepata uhamisho huo wa kimataifa kutoka Congo.
CHANZO CHA HABARI:MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment