KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 29, 2012

SUMA MNAZARETI :SIJAFUKUZWA MTANASHATI

SIKU chache baada ya kutangazwa kuwa ametimuliwa katika kundi la Mtanashati, msanii Suma Mnazareli ameibuka na kukanusha vikali taarifa hizo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Suma alisema hakutimuliwa kwenye kundi hilo bali aliamua kujiondoa mwenyewe.
“Nimeamua kujitoa Mtanashati sababu kubwa ikiwa ni kukosa kile nilichokuwa nikikitarajia,”alisema msanii huyo.
“Nilikwenda Mtanashati kufanyakazi, sikufuata pesa zake. Nilichokuwa nadhani ningekipata, hakipo. Bosi anatafuta zaidi sifa na umaarufu Tanzania na mimi muziki ni kazi yangu,”aliongeza.
Suma alidai kuwa, kiongozi wa kundi hilo, Ustaadh Juma Namusoma anaweza kugawa mamilioni kwa wasanii ili atajwe kwenye nyimbo zao, lakini anashindwa kulipa pesa za kutengeneza video ya msanii wake.
Alidai kuwa, kuna wakati kiongozi huyo alimpatia sh. 300,000 kwa ajili ya kurekodi video, ambazo alisema hazitoshi na zinadhihirisha wazi kuwa, hana dhamira ya dhati ya kuwainua wasanii wake.
“Unadhani tutaweza kushindana na video za wasanii kama AY za milioni 30? Nimeuza hadi simu yangu ya Blackberry ili kuongeza pesa kwa ajili ya kukamilisha video yangu,”alisema msanii huyo akionekana kuwa na masikitiko makubwa.
“Hii ndiyo sababu iliyonifanya nijiondoe Mtanashati kwa sababu sioni faida yoyote ya kuendelea kuwepo kwenye kundi na mimi muziki kwangu ni maisha na nataka nifike mbali zaidi,”alisisitiza.
Wiki iliyopita, Ustaadhi Namusoma alitangaza kuwa, amewatimua Suma na meneja wake, aliyemtaja kwa jina moja la Maneno kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Kundi la Mtanashati linaundwa na wasanii wengi maarufu nchini akiwemo Dogo Janja, Amazon na PNC.

No comments:

Post a Comment