'
Thursday, August 16, 2012
VIONGOZI WA NGUMI, RIADHA HAWAPASWI KUILAUMU SERIKALI
MICHEZO ya Olimpiki ya mwaka 2012 ilimalizika Jumapili iliyopita mjini London, Uingereza huku Tanzania ikitoka kapa baada ya wanamichezo wake saba kushindwa kuambulia chochote.
Katika michezo hiyo, ambayo imesifiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kwamba ilikuwa na msisimko wa aina yake na wa pekee, Tanzania ilishiriki katika michezo ya ngumi za ridhaa, riadha na kuogelea.
Kuvurunda kwa Tanzania katika michezo hiyo hakukuwashangaza watanzania wengi. Ni hali iliyobashiriwa mapema kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila chama kwa wanamichezo wake.
Kabla hata ya wanamichezo hao kwenda London, viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na wale wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) walishatoa taarifa mapema kwamba itakuwa ni miujiza kwa wanamichezo wao kutwaa medali.
Walitoa malalamiko hayo kwa madai kuwa, hakuna msaada wowote walioupata kutoka kwa serikali katika kuwaandaa wanamichezo hao na kwamba hata kambi walizowaweka kwa ajili ya maandalizi zilikuwa za kusuasua.
Na hilo limejidhihirisha baada ya kumalizika kwa michezo hiyo, ambapo viongozi wa mashirikisho hayo wametamka bayana kwamba ni ndoto kwa Tanzania kuonyesha maajabu katika mchezo huo iwapo hakutakuwa na utaratibu wa kuibua vipaji vya vijana na kuwaendelea.
Kauli hiyo ilitolewa wiki hii na Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui ambaye alisema, Tanzania inapaswa kuwekeza kwenye michezo kwa kuwaandaa vijana tangu akiwa shule za msingi.
Naye Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema itakuwa ndoto kwa Tanzania kupata medali kwenye michezo ya Olimpiki na Jumuia ya Madola bila ya kuwepo kwa uwekezaji mkubwa wa fedha katika michezo.
Pamoja na kauli hizo za utetezi zilizotolewa na viongozi hao, bado ukweli unabaki pale pale kwamba, mashirikisho hayo hayapaswi kukwepa lawama kutokana na kuvurunda huko.
Ni kweli kwamba serikali ya Tanzania haitoi ruzuku kwa vyama vya michezo nchini, lakini imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa vyama hivyo kila timu za taifa zinapokabiliwa na michuano ya kimataifa.
Tatizo lililopo kwa vyama vya michezo nchini ni kwamba, viongozi wake wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao binafsi kuliko ya michezo wanayoiongoza ndiyo sababu wanamichezo wake wanashindwa kufanya vizuri kimataifa.
Dalili za viongozi wa michezo kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi zinaanzia nyakati za uchaguzi, ambapo wagombea wake hupigana kufa na kupona katika kuomba kura na kutoa ahadi mbali mbali murua, lakini mara baada ya kushinda uchaguzi, mambo huwa yanakwenda kinyume.
Viongozi wa vyama vingi vya michezo nchini pia wamekuwa wakikumbwa na kashfa mbali mbali. Wapo wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za chama na misaada ya wafadhili na wengine wanatuhumiwa kwa upendeleo kwa baadhi ya wanamichezo katika uteuzi wa timu za taifa.
Lakini kikubwa kuliko vyote ni kwamba viongozi wa baadhi ya vyama vya michezo nchini sio wabunifu. Wamekuwa wakitegemea zaidi michango na ada za wanachama katika kuviendesha vyama vyao badala ya kubuni vyanzo vingine vya mapato kwa kutafuta ufadhili wa kampuni za biashara.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, tangu Rais Jakaya Kikwete alipotoa ofa kwa vyama vyote vya michezo nchini kutafuta makocha wa kigeni kwa ajili ya timu za taifa, na serikali itakuwa tayari kuwalipa, ni vichache vilivyoweza kuchangamkia ofa hiyo. Vingi bado vimelala usingizi wa pono.
Katika mazingira kama haya, ni aibu kwa kiongozi wa juu wa michezo kuilaumu serikali kwa kutovipatia ruzuku vyama vyao kwa ajili ya kuendesha michezo kwa sababu jukumu hilo ni lao si la serikali.
Kazi za serikali ni kuvisaidia vyama pale tu vinapokuwa vimekwama, lakini kuendesha michezo kuanzia ngazi za shule ya msingi na sekondari ni la vyama husika.
Kwa mfano, Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) limekuwa likiendesha mashindano ya mchezo huo katika shule mbali mbali za msingi na sekondari nchini kama ilivyo kwa Chama cha Mpira wa Wavu.
Vyama vingine kama vile cha gofu, tennis na kuogelea, kutokana na kushindwa kuandaa mashindano yake katika ngazi za shule za msingi na sekondari, vimekuwa vikiendesha mashindano ya vijana wa umri mbali mbali na hivyo kuibua vipaji vya vijana wengi na kuwaendeleza.
Swali la kujiuliza ni kwa nini RT ishindwe kuendesha mashindano yake katika ngazi hizo na kuendelea kuilaumu serikali? Je, viongozi wa RT wanataka serikali ndiyo iendeshe mashindano hayo katika ngazi hizo? Kama ndivyo hivyo, jukumu lao ni lipi?
Napenda kuwashauri viongozi wa RT waache kuinyooshea kidole serikali kila wanariadha wa Tanzania wanapofanya vibaya katika michuano ya kimataifa, badala yake wajitazame walikotoka, walipo na wanapokwenda na ikiwezekana wakae pembeni kama watajiona hawaja jipya katika kuliongoza shirikisho hilo.
Pengine huu ni wakati mwafaka pia kwa viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kubadili mwelekeo, hasa ikizingatiwa kuwa, viongozi wake wanakabiliwa na tuhuma nyingi nzito za ubadhirifu wa fedha zinazotolewa na ITC, ambazo zikiachwa hivi hivi, itakuwa ni sawa na kutowatendea haki watanzania.
ERICK,
MDAU WA BLOGU YA LIWAZOZITO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment