KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 16, 2012

KANGEZI: LENGO LETU NI KUUZA WACHEZAJI NJE

WAKATI baadhi ya timu zikihaha kusajili wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, klabu ya African Lyon imeweka wazi kuwa, haina malengo ya kutwaa taji hilo kwa sababu halina thamani kwao. Hayo yameelezwa na mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo, Rahim Kangezi alipozungumza na blogu ya liwazozito mjini Dar es Salaam wiki hii.
SWALI: Wewe ni mmoja kati ya wamiliki wa klabu ya African Lyon inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania na hivi karibuni mliwahi kumpeleka mshambuliaji Mrisho Ngasa kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa Marekani, hebu tueleze matokeo ya majaribio hayo?
JIBU: Ni kweli tulimpeleka Ngasa kufanya majaribio Marekani na alipata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki katika timu ya Seattle Sounders dhidi ya Manchester United, lakini viongozi wa timu ile ya Canada walishauri arudi nchini kwanza ili ajiweke sawa kiafya na kuwa fiti zaidi.
Japokuwa kwa sasa Ngasa amehama Azam na kujiunga na Simba, bado mipango hiyo ipo pale pale na muda wowote anaweza kuitwa tena Marekani, hilo halina mjadala.
Lengo letu ni kuona wachezaji wengi wa Tanzania wanapata nafasi ya kufanya majaribio nje ya nchi ili wapate nafasi ya kucheza soka ya kulipwa na kuingiza mapato mengi zaidi kutokana na soka. Hilo ndilo lengo hasa la African Lyon.
SWALI: Hivi karibuni mmemleta kocha mpya kutoka Argentina badala ya Jumanne Chale. Kwa nini mmeamua kufanya mabadiliko hayo katika benchi lenu la ufundi?
JIBU: Ni kweli tumeamua kumleta kocha mpya, Pablo Ignacio Velez kuchukua nafasi ya Jumanne Chale. Lengo letu kubwa ni kuongeza nguvu kwenye benchi letu la ufundi baada ya kubaini kuwepo kwa mapungufu mengi katika misimu miwili iliyopita.
Pamoja na kufanya mabadiliko hayo, tunamshukuru sana kocha wetu Jumanne kwa sababu amefanyakazi kubwa na nzuri katika kuinoa timu yetu ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kubaki kwenye ligi kuu. Tuna hakika chini ya kocha wetu mpya, tutafanya vizuri zaidi msimu huu kwa sababu tunao wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji.
Unajua lengo la timu yetu sio kutwaa ubingwa wa ligi kuu. Lengo letu ni kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza kwa kuwatafutia timu za kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
SWALI: Unadhani kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambacho kocha huyo mpya atakuwa na timu, mtaweza kupata wachezaji wengi wa kuuza nje?
JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba tayari kazi hiyo imeshaanza kwa kuivunja timu yetu ya kikosi cha pili na kuiunda upya. Kazi hiyo itafanywa na kocha mpya kwa sababu moja ya majukumu yake ni kuibua vipaji vya vijana.
SWALI: Kwa muda mrefu umekuwa ukiupinga mkataba wa udhamini wa ligi kuu kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kwa madai kuwa, zawadi wanazotoa kwa timu ni ndogo. Unadhani nini kifanyike ili kuuboresha mkataba huo?
JIBU: Hata wewe ukiutazama mkataba huo, utagundua kwamba una kasoro. Haiwezekani timu itumie gharama kubwa kusajili wachezaji kila mwaka, kuwalipa mishahara na posho muda wote wa ligi kisha timu bingwa inapata shilingi milioni 40.
Gharama ambazo klabu zinatumia kusajili wachezaji wapya ni kati ya sh. milioni 120 hadi 150. Haiingii akilini ni kwa nini TFF imekubali kuingia mkataba huu na Vodacom wakati fedha za zawadi ni ndogo. Ni vyema mkataba huo utazamwe upya.
Nashukuru kuona kuwa baadhi ya viongozi wenzangu wa timu za ligi kuu wameshaibaini kasoro hiyo na kuniunga mkono, hivyo tunatarajia kuundwa kwa kampuni ya ligi kutasaidia kufanyika kwa mabadiliko hayo.
SWALI: Kwa maana hiyo unataka kusema kwamba, uchache huu wa zawadi zinazotolewa na Vodacom ndio umewafanya msiwe na malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu?
JIBU: Sera ya klabu yangu ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana na kuwauza nje ndio sababu tumeingia mkataba na kocha huyu mpya, ambaye tunamlipa pesa nyingi kwa ajili ya kazi hiyo. Tukisema tusubiri pesa za Vodacom, ambazo hadi kuzipata kwake inachukua muda mrefu, hatuwezi kufika mbali.
Tuna hakika kwamba ujio wa kocha huyu utafungua ukurasa mpya kwa African Lyon kwa sababu tayari vijana wengi wameshaanza kujitokeza kwa ajili ya kufanyiwa majaribio na baada ya muda si mrefu tutakuwa na kikosi kikali cha timu ya pili.
SWALI: Usajili wenu unaonekana kufanyika kimya kimya. Je, tangu kuwasali kwa kocha huyu mpya, ameshawafanyia majaribio wachezaji wangapi na kupendekeza wasajiliwe?
JIBU: Amewahi kuwajaribu baadhi ya wachezaji nyota kama vile Chacha Marwa kutoka Yanga, lakini hakuvutiwa naye na anadhani wachezaji waliopo ni wazuri zaidi.
Wapo wachezaji wengine kadhaa, ambao tunatarajia kuwafanyia majaribio mwishoni mwa wiki hii wakati African Lyon itakapocheza na Yanga katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
SWALI: Kitu gani kingine kipya kilichojitokeza kwenye timu yenu?
JIBU: Tunatarajia kumtangaza mkurugenzi wetu mpya hivi karibuni. Mkurugenzi huyu ni mwanamke na tutamtangaza rasmi wakati wa mechi yetu dhidi ya Yanga.
SWALI: Katika kikosi chenu cha sasa, kuna wachezaji wa kigeni kutoka nje?
JIBU: Wapo wachezaji watatu, ambao bado mwalimu wetu anawafanyia majaribio. Nadhani kati ya leo na kesho atakuwa amemaliza kuwafanyia majaribio na kutoa ushauri kwetu kama wanafaa kusajiliwa au la.

No comments:

Post a Comment