KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 16, 2012

Baba wa Ngasa azicharukia Simba na Yanga

BABA wa mshambuliaji Mrisho Ngasa, aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Azam, Khalfan Ngasa amezionya klabu kubwa nchini kuacha tabia ya kugombea wachezaji.
Ngasa amezitaka klabu hizo kuwekeza zaidi kwa timu za vijana badala ya kugombea wachezaji wenye majina makubwa na kuwalipa fedha nyingi.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Pamba ya Mwanza na Simba, ametoa tahadhari hiyo baada ya klabu za Simba, Yanga na Azam kugombea baadhi ya wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Simba na Azam zimekuwa zikimgombea kiungo Ramadhani Chombo Redondo wakati Yanga na Simba zimekuwa zikimgombea Mbuyi Twite kutoka APR ya Rwanda.
Simba ilitangaza kumsajili Redondo wiki mbili zilizopita kwa madai kuwa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Azam kumalizika tangu Juni mwaka huu.
Hata hivyo, Azam imekuwa ikipinga usajili huo kwa madai kuwa mkataba kati yao na Redondo unatarajiwa kumalizika Juni 2013.
Simba na Yanga pia zimekuwa zikimgombea Twite kila moja ikidai kuwa, imeshaingia naye mkataba na kufuata taratibu za uhamisho na hivyo kusababisha utata katika usajili wake.
‘Kwa kweli nimekuwa nikishangazwa sana na tabia hii ya viongozi wa Simba na Yanga kugombea wachezaji wa kigeni badala ya kuwekeza kwenye soka ya vijana. Tunapaswa kubadilika, ‘ alisema nyota huyo wa zamani wa Simba.
Ngasa alisema tabia hiyo imekuwa ikichangia kuwavunja nguvu wachezaji wazalendo kwa kujiona hawana thamani mbele ya viongozi wao wakati ambapo mchango wao kwenye timu ni mkubwa.
Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na hazina kubwa ya wachezaji wenye vipaji , lakini wanashindwa kutokana na klabu kutokuwa na utaratibu wa kufuatilia vipaji vya vijana na kuwaendeleza.

No comments:

Post a Comment