KLABU ya Azam imesema ipo tayari kumuuza mshambuliaji John Bocco kwa kiwango kidogo cha pesa ili iwapo atafuzu majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Super Sport United ya Afrika Kusini.
Wakala wa mchezaji huyo, Yussuf Bakhresa amesema hawawezi kumuuza mchezaji huyo kwa tamaa iwapo atafuzu majaribio hayo.
Azam imeelezea msimamo wake huo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Super Sport United inamuhitaji aende kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.
Taarifa iliyotolewa na Azam kupitia mtandao wake jana ilisema:"Azam FC imepokea barua ya mwaliko wa majaribio toka klabu ya Super Sport ya Afrika Kusini kwa mchezaji John Bocco ambapo atapaswa kusafiri Jumamosi tarehe 11/08/2012 kwenda Johannesburg, Afrika ya Kusini.
“John Bocco atatumia muda wa wiki moja nchini Afrika ya Kusini. Uongozi wa Azam FC unampongeza John Bocco kwa mafanikio haya na unamtakia kila la heri kwenye majaribio yake." Super Sport United ilivutiwa na Bocco kutokana na uwezo aliouonyesha wakati wa michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika michuano hiyo, Azam ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Yanga mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwanja huo.
Kwa mujibu wa Yussuf, wanachojali ni mchezaji huyo kupata timu itakayomlipa kiwango kizuri cha pesa na pia kuongeza kiwango chake cha soka.
“Ninachotaka ni klabu ya Super Sport kuilipa Azam, mimi sihitaji chochote,”alisema Yussuf.
Bocco alikuwa mfungaji bora wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita na katika michuano ya Kombe la Kagame alishika nafasi ya tatu nyuma ya Hamisi Kiiza na Saidi Bahanunzi wa Yanga.
No comments:
Post a Comment